The House of Favourite Newspapers

Unending Love

0

ILIPOISHIA

Mapenzi ya dhati aliyonayo Jafet kwa Anna, yanamfanya awe tayari kutoa figo yake moja na kumpa Anna ambaye alikuwa na matatizo ya figo zake kushindwa kufanya kazi. Anaamua pia kukataa kusomea upadri akiamini kwamba akimaliza shule, ataoana na Anna ili waishi kama mume na mke.

Siku zinazidi kusonga mbele huku wawili hao wakizidi kupendana mno. Hata hivyo, licha ya wema wake kwa Anna, wazazi wa msichana huyo wanaanza kumchukia Jafet hasa baada ya kufika nyumbani kwao, kijijini Rwamgasa na kujionea maisha ya kifukara waliyokuwa wanaishi Jafet na wazazi wake. Ili kumtenganisha na Jafet, Anna anatafutiwa chuo nchini Marekani.

Siku zinasonga mbele na baadaye, Anna anajikuta akiwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana kutoka familia tajiri, William. Mapenzi yao yanaendelea na baadaye Anna anaanza kuona dalili zisizo za kawaida. Anapoenda kupima anagundulika ni mjamzito lakini kijana huyo anaonesha kukasirishwa na hali hiyo, anataka wakautoe ujauzito huo.

Anna anaamua kutoroka kurejea nyumbani kwao, Mwanza bila Jafet kujua chochote lakini akiwa anaelekea uwanja wa ndege, anakutana na Jafet katika mazingira ambayo hakuyategemea.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Mama Anna alichanganyikiwa, hakuamini alichokisikia kutoka kwa binti yake kwamba alikuwa mjauzito, alimwangalia mara mbilimbili huku akizunguka sebuleni pale. Maneno aliyomwambia yalikuwa mazito mno.

Anna alikuwa akilia, alijua kwamba mama yake asingeamini kile alichomwambia, kila alipomwangalia mwanamke huyo, alionekana dhahiri kuchanganyikiwa. Anna alijaribu kumuomba msamaha mama yake kwani aliamini kwamba kile kilichokuwa kimetokea kilimuumiza mno.

“Naomba unisamehe mama…” alisema Anna japokuwa hapo nyuma aliona kwamba mtu aliyesababisha hilo alikuwa mama yake.

“Una mimba?” aliuliza mama yake, alijua kwamba huo ndiyo ukweli, aliuliza kupata uhakika.

“Ndiyo mama!”

“Nitauficha wapi uso wangu mimi?” alijiuliza. Hakutaka kubaki sebuleni hapo, kilichofuatia ni kuondoka zake kuelekea chumbani.

Huo ulikuwa muda wa majuto, kwa kila kitu kilichotokea, bado aliendelea kumlaumu mama yake kwani aliamini kwamba kama isingekuwa yeye, isingewezekana kutenganishwa na Jafet ambaye alimpenda kwa mapenzi ya dhati.

Anna akaondoka sebuleni hapo na kuelekea chumbani, alipofika, akajilaza kitandani na kuendelea kulia. Ilipofika saa mbili usiku, akasikia honi ikipigwa getini, alijua kwamba alikuwa baba yake, mapigo yake ya moyo yakaanza kudunda kwa nguvu kwa kuona kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima baba yake kuambiwa ukweli.

“Mungu naomba unisaidie katika kipindi hiki kigumu,” alisema Anna.

Wala hazikupita dakika nyingi, akasikia akiitwa na baba yake sebuleni. Sauti ya baba yake ilisikika kitofauti, ilionyesha ni jinsi gani alikuwa na hasira. Anna akajikuta akiogopa, mapigo ya moyo yakaanza kumdunda kwa nguvu, hofu ikamshika na miguu kumtetemeka, akaanza kuelekea sebuleni alipoitwa.

“Unasema una nini?” aliuliza baba yake huku akimwangalia usoni, alionekana kama dubu aliyejeruhiwa kwa jinsi alivyokuwa na hasira.

“Naomba unisamehe baba….” alisema Anna huku akilia.

“Hilo si jibu, umesema una nini?”

“Nina mimba…”

“Ya nani?”

“William…” alijibu Anna huku kijasho chembamba kikianza kumtoka.

Baba Anna akatulia, alionekana kukasirishwa mno, akajikuta akiifungua tai yake na kukaa kochini, akawa kwenye lindi la mawazo, hakuamini alichokisikia. Akamwangalia Anna mara mbilimbili, alichukia kusikia binti yake amepata mimba hata kabla ya kuolewa.

“Naomba unisamehe baba…” alisema Anna, hakuridhika, akaanza kumfuata huku akitembea kwa magoti kwa kuamini kwamba ingekuwa rahisi kusamehewa.

“Umesema mimba ni ya William, si ndiyo?”

“Ndiyo baba.”

“Mwenyewe amesemaje?”

“Baba…..”

“Mwenyewe amesemaje?” aliuliza baba Anna kwa sauti ya juu na yenye ghadhabu.

“Amekataa…..”

Baba Anna akashusha pumzi ndefu na nzito, kile alichoambiwa, hakukiamini. Kwanza akaanza kumfikiria William, kwa muonekano wa nje, alionekana kijana mtulivu, mwenye hekima ambaye hakutakiwa kabisa kuikataa mimba ile.

Mbali na kumfikiria kijana huyo, pia akaanza kumfikiria Anna mwenyewe na tatizo alilokuwa nalo la kuwa na figo moja. Hapo ndipo alipogundua kwamba hata kile alichokifanya cha kuonyesha ghadhabu kilikuwa kitu kibaya kwani angemfanya binti yake kuwa kwenye presha kubwa na hatimaye kupata tatizo zaidi.

Akajikuta akitulia, akalilazimisha tabasamu lake usoni mwake kiasi kwamba kila mmoja kushangaa kwani ni sekunde chache zilizopita alikuwa na hasira kama mbogo.

“Nenda chumbani kwako,” alisema baba Anna, binti huyo akatii na kurudi chumbani, ila hakufunga mlango, alitaka kusikia wazazi wake walizungumza nini, hivyo akategesha sikio mlangoni.

“Wewe ndiye chanzo,” alisema baba Anna huku akimwangalia mkewe.

“Mimi ndiye chanzo?” aliuliza mama Anna huku akionekana kushtuka.

“Ndiyo! Wewe ndiye uliyesababisha hili,” alisema baba Anna.

Wawili hao wakabaki kwenye malumbano ya muda, baba Anna alimlaumu mkewe lakini mwanamke huyo alijitetea kwa nguvu zote kwamba hakuwa chanzo. Baada ya malumbano hayo yaliyodumu kwa dakika kadhaa, wawili hao wakafikia muafaka kwamba mimba ya Anna ilikuwa ni lazima itolewe, iwe isiwe, mimba lazima itolewe.

“Umesema mimba itolewe?” aliuliza mama Anna.

“Ndiyo! Tena haraka sana, hatuwezi kuwa na mtoto aliyekataliwa na baba yake,” alisema baba Anna.

Huko ndani, Anna alikuwa na presha kubwa. Hakuamini alichokisikia kwani aliogopa mno kutoa mimba hiyo.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatano katika gazeti la Risasi Mchanganyiko.

Leave A Reply