The House of Favourite Newspapers

Waoo…! Kama Jana Vile!

0

ILIPOISHIA RISASI JUMATANO:

Nje ya hospitali hiyo kuna kituo cha daladala, sasa zilipita kama tatu bila kusimama, mama Monica akahisi wanamwacha kwa sababu yeye ana virusi.

Daladala ya nne aliamua kuipungia mkono ili isimame, konda akamjibu…

“Chukua Bajaj bwana, we mgonjwa hutaweza humu.”

SASA JIACHIE MWENYEWE…M

ama Monica alizidi kuishiwa nguvu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya kiakili. Alijihisi mwenye dhambi kuliko binadamu wote hapa duniani.

“Yaani leo hii nimefikia hatua ya kunyanyasika hivi kwa sababu nina Virusi vya Ukimwi? Mungu atamlipia Magembe,” alisema huku akiamua kupanda usafiri wa Bajaj kwa ajili ya kwenda kwenye biashara zake.

Lakini njiani aliamua kutoka moyoni kwamba ampigie simu Magembe na kumpa ‘laivu’ ili ajue kwamba ameshapima  na majibu yametoka.

Simu ya Magembe iliita tu bila kupokelewa kwa muda mrefu kama mara tano. Mama Monica  akaamua kumtumia ujumbe wa kumtisha…

“Hata usipopokea simu, kazini kwako nimeshapafahamu na sasa niko na polisi nakuja hapo.”

Magenge aliposoma ujumbe huo almanusura apige mwereka wa nguvu kwa kiwewe. Kwanza alitafuta kichwani nani anaweza kumwonesha mwanamke huyo kazini kwake. Lakini akakumbuka haraka kwamba, kaka yake, ambaye walikutana gesti anapajua. Palepale aliamua kupiga simu…

Haloo mama Monica…”

“Umejua nakuja na polisi ndiyo unaamua kupiga simu mwenyewe…hivi wewe Magembe ni kwa nini uliamua kuniambukiza Ukimwi lakini…yaani ulijijua kabisa kwamba umenasa ukaamua kunipa na mimi…nilikukosea nini lakini wewe mwanaume…ooo…oooo…aaaa…,” alianza kulia mama Monica na kukata simu.

Upande wa pili kwa Magembe, hali ilikuwa mbaya sana. Alipiga tena lakini mama Monica hakupokea. Sasa akawa hajui kama mwanamke huyo anakwenda kazini kwake na polisi kama alivyosema au la..!

“Hapa kimenuka, ngoja niondoke,” alisema moyoni Magembe. Alitoka kuendea gari lake. Akamwambia mlinzi…

“Atakuja mwanamke fulani, mrembomrembo hivi…mwambie nimetoka na sitarudi mpaka kesho.”

“Sawa bosi,” alijibu mlinzi.

***

Dereva wa Bajaj alishindwa kujizuia, kwanza akampa pole mama Monica…

“Anti pole sana. Huyo Magembe kama ni yule ninayemjua mimi, nakupa pole. Halafu hakuna asiyejua kwamba ana Virusi vya Ukimwi…mi nashangaa sana sijui kwa nini hakamatwi,” alisema dereva huyo.

“Kumbe hata wewe unamjua?” aliuliza mama Monica.

“Sana…si zamani alikuwa na pikipiki sasa amenunua kagari?”

“Eee…”

“Namjua sana yule jamaa.”

Wakiwa bado njiani, mama Monica alimwona Magembe akiwa ndani ya gari lake walipishana kwa kasi ya ajabu…

“Yule kapita,” alisema mama Monica. Dereva wa Bajaj akaunga mkono kwamba ni kweli yeye kaliona gari lake. Mama Monica akatuma meseji…

“Kwa sababu umejua nakuja kazini kwako ukaamua kuondoka siyo? Kesho nitakudamkia. Utanikuta nakusubiri na polisi watakuwa halali yako.”

Magembe aliposoma meseji hiyo aliegesha gari pembeni. Kichwani alijua kuwa ni kweli mama Monica amefika ofisini kwake, akakosa amani…

“Sasa atakuwa amemwambiaje mlinzi? Asije akawa amemwaga mboga. Na kama amenianika aisee atakuwa amafanya jambo baya sana. Heshima yangu itakuwa imeshuka kwa sehemu kubwa. Nitauweka wapi uso wangu miyee.”

Magembe aliwaza sana, akaamua kumtumia meseji mama Monica amwambie kitu. Mama Monica aliisoma…

“Haloo mama Monica, please! Nakuomba tuonane muda huu, sehemu yoyote unayoitaka wewe mimi nitakuja lakini usiwe na polisi.”

Mama Monica, alijifikiria sana akamkatalia huku akimsisitizia kwamba, yeye atatangulia kufa kabla yake…

“Wewe Magembe lazima uanze kufa wewe ndipo nifuate mimi. Na kaa ukijua haitatokea wewe ukaanza kusikia kifo changu kabla mimi sijasikia cha kwako. Huwezi kunitenda ukatili kama huu halafu Mungu akakuachia…

“Umeniambukiza Ukimwi, imeniachanisha na mume wangu, unasababisha mtoto wangu aishi kwa shida. Haiwezekani hata siku moja. Nakutakia maisha mema.”

Meseji hiyo haikujibiwa na Magembe na si kwa kutopenda, bali ilimuumiza sana. Alijikuta kwa mara ya kwanza akimwaga machozi peke yake ndani ya gari.

Alipofika kwenye biashara zake, mama Monica aliwaita wasichana wake wa kazi na kuwaambia maneno haya…

“Maneno yangu kwenu ni mazuri leo. Nawaonya wadogo zangu kwamba isije ikatokea hata siku moja ukamkubali mwanaume kimapenzi bila kumjua historia ya maisha yake, ni hatari.

“Mimi kama mnavyojua, nimekuwa na uhisiano wa kimapenzi na yule kaka, Magembe. Lakini mwenzenu nimetoka kupima sasa hivi, nimekutwa nina Virusi vya Ukimwi.”

Aliposema hivyo tu, wale wasichana walishtuka sana na kujishika midomo kwa hofu…

“Msishtuke. Hilo nahesabia ni kosa langu. Kama mlivyokuwa mkimwona, anakuja kila siku na kunipa elfu kumikumi kumbe alikuwa anatafuta njia ya kuninasa ili aniambukize.

“Kinachoniuma ni kwamba, mume wangu amegundua jambo kubwa kwangu na ameamua kuniacha. Hapa nimetokea hospitali lakini nilianzia kwa shangazi yangu ambako mwanangu nimemwacha kule. Jamani wadogo zangu kuwa makini, msiwe kama mimi, sikupata somo hili ninalowapa nyie na mkijakuolewa, msikubali kushawishika na wanaume wa nje,” alisema mama Monica na kuanza kulia…

“Dada wanasemaga bado unaweza kuishi miaka mingi hata kama una Virusi vya Ukimwi. Jua hata wewe unapaswa kuishi miaka mingi dada. Siyo kwamba utakufa kesho,” alisema msichana mmoja lakini mama Monica akakataa kuliwazwa na kujutia maisha yake yote huku akimlaani Magembe.

MWISHO.

Leave A Reply