The House of Favourite Newspapers

Rais Magufuli Aagiza Watoza Ushuru Wafukuzwe – Video

0

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ameagiza kufukuzwa mara moja kwa watoza ushuru waliopo kwenye Soko Kuu Jipya la Morogoro.

 

 

Magufuli ametoa agizo hilo kwenye hotuba yake leo Februari 11, 2021 wakati akizindua soko hilo la kisasa mkoani Mororgoro.

 

“ Tumetoa Billioni 17 kujenga Soko hili kwa ajili ya kuwasaidia watanzania Masikini lakini nasikia kuna madalali, ambao ni watendaji wa serikali wanachangisha fedha za vizimba kwa wananchi masikini.

 

 

“Nimesikiliza shida na kero za wafanyabiashara waliopo ndani hili, nimegundua mbali na sheria nzuri zinazowekwa na bunge ili kuwalinda wananchi, lakini moja ya manispaa ambazo zinaongoza kwa kuvunja sheria hizo ni Morogoro.

 

”Nina uhakika sheria ambayo ilipitishwa na bunge kuwa mtu akibeba chini ya tani moja asitozwe pesa yoyote ya ushuru inafahamika kwa viongozi wake, lakini hapa Morogoro ni tofauti, mtu anakuja na kiroba chake anakuta mtu wa ushuru anamsubiri.

 

 

”Unaweka watu hapa wa kutoza ushuru, sasa wa nini wakati wewe Manispaa unajua kuwa kuna vizimba 900 watu wakishalipia kuna haja gani ya hao kuwepo, nataka uwafukuze mara moja, ndani ya wiki moja sitaki kusikia kero kwa wananchi, na katika uongozi wangu ni mwiko kusumbua raia.

 

“Tozo nyingi za kilimo zilifutwa ikiwemo ya kuwatoza Wakulima na Wafanyabiashara wadogo wanapochukua bidhaa zao sokoni, mwananchi akibeba mzigo wake usiozidi tani 1 hatakiwi kutozwa hela yoyote, ni utaratibu wa nchi nzima.

 

“Kitu nilichokiona kwenye hili Soko la Manispaa ya Morogoro, wapo Watu waliopewa vizimba bila tatizo ila wapo waliopewa vizimba kwa kukodishwa na madalali na baadhi ya madalali hao ni wafanyakazi wa Manispaa,” amesema Rais Magufuli.

 

Soko hilo lina maduka 304, vizimba 900, eneo la maegesho ya magari madogo 150 na magari makubwa 50, maegesho ya bajaji, pikipiki na baiskeli pamoja stoo 36 za mitumba. Soko pia lina sehemu ya kutupa takataka.

 

Leave A Reply