The House of Favourite Newspapers

Makonda Hongera Kwa Kushirikiana na Makamishna Wapya

Mkurugenzi wa GlobaL Publishers Eric Shigongo

Na ERIC SHIGONGO| GAZETI LA UWAZI| NAPASU JIPU

Mungu ni mwema na ndiye muweza wa mambo yote, mimi na wewe tumhimidi daima Baada ya kusema hayo nianze mada ya leo kwa kumpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kumteua Rogers Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya kulevya nchini.

Rais John Pombe Magufuli

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano Ikulu wiki iliyopita ilisema Sianga atasaidiana na Kamishna Mihayo Misikhela ambaye anakuwa kamishna wa oparesheni na Fredirick Kibuta ambaye amekuwa kamishna wa intelijensia.

Lazima nikiri kwamba uteuzi wa viongozi hao umekuja wakati muafaka kwa maana nyingi, kwanza wiki iliyopita wabunge wakichangia masuala ya Ukimwi walibaini kuwa kulikuwa na dosari katika sera ya madawa ya kulevya ya mwaka 2004.

Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya alisema hapingani na mapambano yanayoendelea sasa ya vita dhidi ya madawa ya kulevya lakini akamshauri rais ateue kamishna wa chombo ambacho ni mahususi kisheria kwa ajili ya kupambana na kudhibiti madawa ya kulevya ambacho ni Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini.

Najua aliyekuwepo, Christopher Shelukindo alishastaafu, hivyo uteuzi wa Rais Magufuli umekuja wakati muafaka kwani wiki iliyopita kila kona ukipita na kukuta makundi ya watu, mjadala ulikuwa ‘Makonda na vita ya madawa ya kulevya.’

Lakini uteuzi wa rais wa vigogo hao wa taasisi ya kupambana na madawa ya kulevya ulikuja siku tatu tu baada ya Makonda kutaja watu kuhusiana na madawa ya kulevya, ikielezwa kwamba hiyo ilikuwa ni awamu ya pili baada ya awali kuwataja wasanii mbalimbali.

Najua kwamba hivi karibuni rais alisema bila kujali wadhifa wake kwenye jamii, kila anayejihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ni lazima akamatwe, hilo Watanzania wote tunaunga mkono. Kwa maoni yangu, sasa vita ya madawa ya kulevya tutakuwa tunapigana na kuongozwa na chombo mahususi kisheria  chenye mamlaka ya kupiga vita hivyo badala ya hali ilivyo sasa.

Najua Watanzania wengi wapo pamoja nami nikisema kwamba biashara hii haramu ya madawa ya kulevya kwa sasa nchini imefikia katika hali mbaya na kwamba kuna baadhi ya mitaa madawa haya yanauzwa kama njugu mitaani na wauzaji na watumiaji bila kujali chochote.

Tulizoea kuona biashara hiyo haramu ikifanyika kwa kificho miaka ya nyuma na polisi walikuwa wakifanya kazi kubwa kuwabaini wahusika, lakini siku hizi mitaani watu wanaonekana wakiwa wamelewa madawa ya kulevya na kuna baadhi ya mitaa watu huwa wanaogopa kupita kuwahofia watumiaji wa madawa hayo ambao wengi wao huwa ni vijana.

Naamini vita yoyote ni lazima iwe na majemedari sasa mamlaka ya kupambana na madawa ya kulevya ilikosa makamanda lakini sasa wapo, tena naambiwa ni wachapa kazi kwelikweli ambao ni Sianga na wasaidizi wake, Kamanda Misikhela na Kamanda Fredirick Kibuta.

Nichukue nafasi hii kuwapongeza makamanda hao kwa kuaminiwa na rais, hiyo ni ishara ya wazi kwamba kiongozi wa nchi anawaamini katika kuinusuru nchi na balaa la kuwa taifa la vijana ‘mateja.’ Nisiwafiche makamanda hao kwamba Watanzania wana imani kubwa kwao kwa sababu vijana ambao ni nguvukazi ya taifa hasa wa mijini wanateketea kwa kubwia ‘unga’ kwa kasi kubwa.

Niwakumbushe tu aliyowahi kuyasema aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Godfrey Nzowa kwamba changamoto kubwa ya jemedari wa vita ya mihadarati ni hatari kwa maisha, hivyo mnaweza kumpata yeye akawaongezea maarifa ya vita hiyo. Naamini majemedari walioteuliwa wanaweza kutumiwa vizuri na Makonda tumeona jana akikabidhi jalada lenye orodha ya watu 97.

Hii ni vizuri na ndivyo tulivyokuwa tukishauri. Naamini orodha hiyo itafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na makamanda waliopewa jukumu la kuchunguza na kubaini ukweli kwa sababu kuu moja, kwamba hawa ni watu waliobobea katika uchunguzi kwa miaka mingi.

Kama alivyosema Makonda vita hii ni ta watu wote bila kujali itikadi na naamini ikiwa wote tutashirikiana na kuacha unafiki, tutashinda. Hakina Sianga atakata mzizi wa fitina kwa sababu kazi ya uchunguzi itafanyika kitaalamu zaidi. Ashirikiane nao ataona faida yake na haya tuliyoyaona, hatutayaona tena. Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Comments are closed.