The House of Favourite Newspapers

Leicester Byebye, Tutaonana

Na WAANDISHI WETU| CHAMPIONI JUMATANO|MICHEZO NA BURUDANI

LEICESTER City ndiyo ilikuwa timu tishio zaidi msimu uliopita, hakuna hata mmoja anayeweza kukataa hilo.   Ilianza kuonyesha moto wake kuanzia kwenye michezo ya mwanzoni ya Ligi Kuu England huku kila mmoja akiipa nafasi ya kufanya vizuri mwishoni jambo ambalo lilitimia.

Leicester walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza kwenye historia yao baada ya kumaliza kileleni kwa tofauti ya pointi kumi dhidi ya Arsenal ambao ilishika nafasi ya pili.

Kweli ilikuwa timu tishio na msimu huo iliruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu tu, mara moja walifungwa na Liverpool na mara mbili walifungwa na Arsenal, lakini kwenye michezo mingine yote msimu huo waliambulia pointi.
Leicester ile ya msimu uliopita ndiyo hiyo ambayo leo inapambana kuhakikisha haishuki daraja.

wa sasa Leicester ni timu ya kiwango cha chini sana pamoja na kwamba ina wachezaji wengi walewale huku ikimpoteza kiungo wao, Ng’olo Kante ambaye alijiunga na Chelsea. Kiwango cha Leicester cha msimu huu hakionyeshi hata kidogo kuwa ni timu ambayo ilitwaa ubingwa msimu uliopita kabla ya michezo mitatu ligi imalizike. Kwa sasa timu hiyo inashika nafasi ya 17 ikiwa na pointi 21, baada ya kucheza michezo 25 kwenye ligi hiyo.

Msimu uliopita Leicester wakiwa wameshacheza michezo 25 walikuwa wamejikusanyia pointi 50, hivyo ni zaidi ya mara mbili ya zile ambazo msimu huu wamejikusanyia hadi sasa.

Hii ina maana kuwa Leicester wameporomoka na kama wangekuwa kwenye kiwango kama cha msimu uliopita kwa sasa wangekuwa na pointi 50 sawa na Arsenal na Tottenham Hotspur ambao wapo kwenye nafasi ya tatu na nne. Timu hii chini ya kocha Claudio Ranieri, imekuwa na safu mbaya ya ulinzi msimu huu, ikiwa imesharuhusu nyavu zake kutikiswa mara 43, huku wenyewe wakiwa wamefunga mabao 24 tu hadi sasa.

Kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Swansea City, juzi kilionyesha kuwa Leicester wapo pointi moja tu mbele ya timu zinazoweza kushuka daraja msimu huu na kocha wa timu hiyo ameshakiri kuwa hali yao ni mbaya tofauti na jinsi walivyokuwa wakifi kiri mwanzoni.

 

Baada ya kichapo cha juzi ina maana kuwa sasa Leicester wamecheza michezo sita mfululizo bila kufunga bao lolote hali ambayo inaonyesha ni wakati mgumu kwa washambuliaji wa timu hiyo akiwemo staa wao Jamier Vardy ambaye hadi sasa ameshafunga mabao matano tu.

“Kila siku naamini kuwa ligi ndiyo inaanza kwetu lakini mambo yanabadilika, nafi kiri tunatakiwa kupambana na kuonyesha kuwa sisi ni watu wa namna gani.

“Zimebaki mechi 13, bado tupo chini sana kwenye ligi na hali hii inatishia maisha yetu kwenye ligi, kama hali inaweza kwenda kama inavyokwenda sasa tunaweza kuporomoka zaidi na zaidi.

“Siyo vyema kama tutakaa kimya, nafi kiri sasa kila mmoja anatakiwa kupambana kuonyesha kuwa hali hii inamsumbua na siyo nzuri kwenye timu yetu.

“Timu yetu ina matatizo mawili makubwa, kutofunga mabao na kuruhusu kufungwa mabao, lazima tuzungumze pamoja na kutafuta jinsi ya kupambana na hali hii,” alisema Ranieri raia wa Italia.

Hata hivyo, pamoja na kocha huyo kuonekana kuwa anaweza kutimuliwa, wachezaji wa timu hiyo wamemkingia kifua na kusema kuwa wapo nyuma yake na makosa yanayotokea uwanjani ni ya kwao na yeye hayamhusu.

“Tupo nyuma ya kocha kwa asilimia 100, haya yanayotokea ni matokeo ya uwanjani na kocha hahusiki nayo, tutapambana pamoja mpaka mwisho wa msimu,” alisema kiungo Danny Drinkwater.

Wachezaji mastaa wa msimu uliopita Jamie Vardy ambaye msimu huo alifunga mabao 19 na Riyad Mahrez ambaye alikuwa Mchezaji Bora wa England, kwa msimu huu wameonekana kushuka na kila mchezo wamecheza chini ya kiwango.

Ng’olo Kante ambaye alionyesha kiwango cha juu msimu uliopita ndiye amekuwa kilio cha mashabiki wa Leicester msimu huu kuwa kuondoka kwake kumemaliza ushirikiano kati yake na mabeki Wes Morgan na Robert Huth.

Ingawa msimu uliopita wakati akiwemo hakuna aliyekuwa anaona umuhimu wa kiungo huyo ambaye alicheza karibuni michezo yote ya timu hiyo, sasa pengo lake limeonekana moja kwa moja. Safu ya ulinzi ya Leicester imeonekana kuwa ovyo kuliko hali ilivyokuwa kwenye miezi tisa iliyopita.

Lakini ukiachana na safu ya kiungo bado timu hiyo imeonekana kuwa mbovu, pia washambuliaji hawana makali yale ambayo walikuwa nayo msimu uliopita. Wakati msimu uliopita hali ilikuwa nzuri kwa Vardy lakini tangu Desemba 17, mwaka jana hadi Februari mwaka huu, mshambuliaji huyo hajapiga shuti lililolenga lango hata moja kwa timu pinzani. Hii inaonyesha kuwa ameporomoka kwa asilimia 100 kutoka kwenye kiwango chake cha msimu uliopita.

Hata hivyo, unaweza kusema kuwa wameamua kutofanya vizuri makusudi kwa kuwa mwishoni mwa msimu uliopita waliomba kuondoka na kujiunga na Arsenal, lakini klabu hiyo ikagoma.

Ukweli unabaki kuwa kama Leicester hawatachukua hatua za haraka kupambana na hali iliyo kwa sasa wakiwa na michezo mingi migumu imebaki, basi itakuwa rahisi kwao kushuka daraja kuliko kubaki.

Comments are closed.