The House of Favourite Newspapers

Wazo Langu Limefika; Nakushukuru Waziri Mkuu Majaliwa, Umenena

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Na ERIC SHIGONGO| GAZETI LA UWAZI| NAPASUA JIPU

NAAMINI kwamba wasomaji wote wa safu hii hamjambo, kama hivyo ndivyo basi hatuna budi kumshukuru Mungu aliyetufanya leo tuwe pamoja katika makala haya. Wiki iliyopita niliandika katika gazeti dada na hili nikishauri kwamba watuhumiwa wowote ni vema wakachunguzwa kabla ya kutangazwa hadharani kwa kuwa kufanya hivyo kunaharibu taswira ya mtu katika jamii kama tuhuma alizotuhumiwa si za kweli.

Nilimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda lakini nikamshauri kwamba atumie vyombo vya dola kuchunguza wale wote anaowatuhumu kufanya uhalifu. Wazo langu hilo nafurahi hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (pichani) ameliona na ametangaza kwa kuwaambia wakuu wa mikoa na wilaya kutotangaza majina ya watuhumiwa kabla ya kufanyika uchunguzi dhidi ya madai yao na kujiridhisha.

Kwa vyovyote waziri mkuu ameyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati alipokutana na kuzindua Baraza la Kudhibiti Madawa ya Kulevya jijini Dar es Salaam. Ni siku chache pia baada ya mkuu wetu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutaja majina ya watu wakiwatuhumu kujihusisha na madawa ya kulevya na kusababisha alaumiwe na watu tofauti kwa kitendo chake hicho, mimi pia nikatoa ushauri wangu.

Wengi waliokosoa kitendo hicho hasa wabunge walisema kutangaza majina ni kuharibu uchunguzi na pia kunachafua watu (kama nilivyoona mimi) kabla ya kuthibitishwa na chombo husika hasa mahakama ambacho ndicho chenye mamlaka kisheria ya kumtia mtu hatiani, sheria inasema hata polisi hawana mamlaka hiyo.

Ndiyo maana Kamishna Mkuu wa Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya Tanzania, Rogers Sianga alipokabidhiwa majina 97 na Makonda alifuata taratibu, bila shaka alikwenda kuyafanyia kazi kitaalamu.

Naamini kama angeyatangaza pale, balaa lake lingekuwa kubwa kwa sababu ni wazi watu wangelalamika sana na kuonekana chombo cha kutoa haki, yaani mahakama kinaenguliwa katika kutenda haki.

Zoezi la kwanza na la pili, tulishuhudia watu waliotajwa wakiwemo wasanii, wafanyabiashara, kiongozi wa dini na wanasiasa, wakipekuliwa, kulazwa ndani na kupimwa damu zao kama ni watumiaji wa mihadarati au la! Ulikuwa ni mtikisiko mkubwa katika jamii. Hakuna asiyejua kwamba Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan na wasanii kibao waliitwa polisi na kusababisha mtikisiko kwao, familia zao na hata kwa watu wanaowaongoza na marafiki zao.

Lakini Waziri Mkuu, Majaliwa wakati anazindua baraza alisema wazi kwamba wakuu wa mikoa wana nafasi nzuri ya kushiriki katika vita hiyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu. Kwa maneno yake Waziri Mkuu Majaliwa alisema, namnukuu:

“ Wakuu wa mikoa mna kazi kubwa katika kazi hii. Mkiwa wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama, mpo kwenya nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Kiongozi huyo aliyasema hayo mbele ya mawaziri ambao ni wajumbe wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Madawa ya Kulevya pamoja na wakuu wa mikoa. Waziri mkuu hakuishia hapo aliwaambia;

“ Jiepusheni kuwatangaza watuhumiwa kabla hatujawafanyia uchunguzi, itakapotokea tumefanya uchunguzi na kuwakamata watuhumiwa, msisitie kuwatangaza kwenye vyombo vya habari, msiogope, serikali inawategemea na kuwaunga mkono.”

Kwa ujumla aliyoyasema waziri mkuu yalikuwa ni maneno mazito kwani aliwaonya pia watendaji wa mamlaka ambao watachukua rushwa kwa lengo la kuwasaidia wahusika wa madawa ya kulevya. Ukweli ni kwamba hii ni vita kubwa kwa sababu inawahusisha wafanyabiasha wenye uwezo mkubwa kiuchumi na watu maarufu katika jamii.

Nami nisisitize kwamba watendaji mliopewa dhamana ya kusimamia vita hii kila mmoja afahamu kwamba ameaminiwa na taifa, hivyo ni lazima wawe na uadilifu kwani ni kazi inayohitaji umakini na uangalifu wa hali ya juu. Kutokana na Rais Dk. John Magufuli kuteua viongozi wa Mamlaka ya Kupambana na Madawa ya Kulevya na kukumbusha baraza lake na kutokana na waziri mkuu kuzunguzia vita hii ni wazi kwamba serikali ya awamu ya tano imedhamiria kupigana na kushinda.

Hatutaki Tanzania kuwa njia ya kupitishia madawa ya kulevya na pia hatufurahii kuona vijana wetu wakitumia ‘unga’ na kuharibikiwa akili kisha kuwa mazezeta, hakika wote wanaohusika wakamatwe na kila mwananchi awe askari katika vita hii kubwa, asiwepo wa kujitenga. Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Comments are closed.