The House of Favourite Newspapers

Shoga: Muandae Mzee kwa Chakula Siyo Uandaliwe!

Na SOPHIA MA`MDOGO| GAZETI LA UWAZI| LOVE & LIFE

HAYA sasa shoga wangu wa ukwee! Ni Jumanne tena kama ileee tunakutana kwenye kona yetu, kona ya kutia hamu kuiona kama siyo kuisoma! Kona ya mahaba kama siyo mashamsham! U hali gani?

Kiafya kwa upande wangu nilikuwa naumwa kidogo shoga, si unajua kubadilika kwa hali ya hewa huku ndugu, mara mvua mara jua, mara baridi mara joto, kwa wale wenzangu mnaoishi Dar mtakuwa mmenipata! Ila nawe kama ni mgonjwa siku zote nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akujalie afya njema ili uendelee na majukumu yako ya kila siku.

Shoga baada ya wiki iliyopita kuongelea raha ya mchezo kushangilia, nilipata meseji za kutosha na wengine wakiniambia wamefanyia kazi na kufurahia chakula cha usiku. Shoga mwenzako huwa nafarijika sana kama ninachokufunza hapa unakifanyia kazi na unafurahia, upo somo?

Basi baada ya hayo shoga, nikuwekee hapa kile ambacho umekisoma kwa ufupi hapo juu na kutamani ukione kwa urefu. Kama nakuona vile ulivyovuta pumzi shoga wangu mie maana si kwa kutoa macho huko, utasema si wa nchi hii! Ehhheee heeee heeiya shoga, upo? Shoga, asikudanganye mtu siku hizi kila kitu kinataka maandalizi, mfano unapokuwa mjamzito ni vyema ukafanya maandalizi ya kumlea mtoto utakayemzaa.

Mnapotaka kuanza ujenzi wa nyumba au kufungua biashara na mumeo, lazima maandalizi yawepo kwani bila kufanya hivyo mtakwama tu. Si kwa hayo tu, hata ukimpata mchumba ili muingie kwenye hatua ya ndoa lazima maandalizi yawepo ndiyo maana kuna kitchen part , send off
kisha ndoa na harusi inamalizia.

Baada ya kufuatwa na shoga yetu mmoja ambaye sitamtaja kwa jina na kunilalamikia kuhusu mumewe kutokuwa na mushawasha wa yale mambo yetu, nimegundua kinachofanya mzee asiwe na hamu naye ni kukosa maandalizi.

Shoga, hakuna jambo baya kama mwanamke kutokuwa mbunifu wa kumuandaa mzee ili akiwa kazini mawazo yote yawe kwake huku akijisemea moyoni;

“Leo usiku nitampa mambo mazuri mke wangu hadi afurahi na roho yake.”

Kauli hiyo haiwezi kuja hivihivi bila wewe mwanamke kumwandaa mzee akaandalika kweli kuanzia asubuhi anapojiandaa kwenda kazini na akiwa kazini. Kama usiku wa siku hiyo alikufurahisha na bado kiu yako haijaisha, kabla hajaondoka msifie kwa vimbwanga vyake vya usiku na mwambie kama isingekuwa kwenda kazini bado ulikuwa unamhitaji. Kauli hiyo itamfanya mzee anapoondoka kuelekea kibaruani, mawazo yote kuwa kwako na kupanga atakapomaliza kazi kutopitia kokote zaidi ya kurudi nyumbani kukufurahisha.

Akiwa kazini, mtumie meseji ya malovee kwamba umemmis sana na unatamani akufanyie mambo mazuri kama aliyokufanyia usiku.Hapo utakuwa umemroga bila kwenda kwa sangoma, na ukijua anakaribia kumaliza kazi mpigie simu zungumza naye kwa sauti ya mahabati, hapo utamfanya mzee kusisimka na atatoka huko akiwa na hasira za kukupa penzi shatashata.

Kwa leo niishie hapa shoga wangu wa ukwee maana mimi tena kwa kuachiwa nafasi kidogo natiririka kama mvua za msituni! Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine tamu zaidi, upo?

Comments are closed.