The House of Favourite Newspapers

Mchungaji Mbaroni kwa Tuhuma ya Ubakaji

DODOMA: Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste la Ipagala Manispaa ya Dodoma, Joshua Warioba, anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka mitano.

Inadaiwa kuwa mtoto huyu alikuwa ni mwanafunzi wa masomo ya ziada katika kituo cha chekechea cha Efretha English Medium Pre & Primary School, kinachomilikiwa na mchungaji huyo.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa mchungaji huyo anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuingilia mtoto huyo kila siku alipokuwa akienda masomo ya ziada (tuition) na jalada la kesi hiyo lipo kwa mwanasheria wa serikali ambaye muda wowote atapeleka hati ya mashtaka polisi ili afikishwe mahakamani.

Mama wa mtoto huyo anasema kuwa alimwandikisha mwanaye kusoma chekechea katika shule ya kanisa hilo Februari 2 mwaka huu. Baada ya mdogo wake kuja nyumbani kwake na kuuliza kama mwanaye naye huwa anahudhuria masomo ya ziada na kujibiwa kuwa hajui kama kuna masomo hayo, ndipo alipoamua kufuatilia kwa majirani wengine pia kuubaini ukweli.

Wananchi walikusanyika wakitaka kumpiga mchungaji huyo lakini aliokolewa na mwanajeshi mmoja na kukimbizwa polisi.

Kamanda Mambosasa aliwataka wazazi kutowaruhusu watoto kwenda kusoma masomo ya ziada (tuition) pasipo kuwa na uangalizi wa karibu na pia aliitaka jamii kuendelea kupiga vita dhidhi ya matendo ya udhalilishaji kwa kutoa taarifa ili hatua za kisheria zichukuliwe.

 

Comments are closed.