Aliyepeleka Mgonjwa India Aporwa

Kituo cha Treni mjini New Delhi.

Na MWANDISHI WETU| RISASI MCHANGANYIKO| HABARI

NEW DELHI: Mwanamke mmoja raia wa Tanzania, ambaye yupo India alikompeleka mwanaye mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kwa matibabu, ameporwa kiasi kikubwa cha fedha na watu waliokuwa na pikipiki katikati ya Jiji la New Delhi, Risasi Mchanganyiko limebaini.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times of India la juzi, mama huyo aliyetambuliwa kwa jina moja la Fatima, alivamiwa katika eneo lijulikanalo kama Karol Bagh, Ijumaa wiki iliyopita, siku hiyo hiyo ambayo pia raia mmoja wa Ujerumani, naye alikabwa na kuporwa na watu waliotumia nyembe za upasuaji Kaskazini mwa jiji hilo, lijulikanalo kama Kotwali.

Hata hivyo, watu waliompora Mjerumani huyo walikamatwa juzi Jumatatu wakiwa na bidhaa zote alizoibiwa. Fatima, ambaye Risasi Mchanganyiko bado linasaka habari zake, aliporwa kiasi cha dola 6,000 na kiasi kikubwa cha fedha za Tanzania na India ambazo hazikutajwa.

Tukio hilo lilitokea saa tano kasoro dakika saba usiku, wakati Fatima ambaye pia ameporwa hati tatu za kusafiria za ndugu zake zilizokuwa katika begi, akirejea hotelini alikofikia sehemu za Saraswati Marg, akitokea hospitalini. Kwa mujibu wa maelezo aliyoandikisha polisi, mwanamke huyo ilikuwa arejee nyumbani mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini ameshindwa kwa sababu ya tukio hilo.

Polisi baada ya kuchukua picha za CCTV, walisema wameshindwa kuzitambua namba za pikipiki iliyowabeba waporaji. Kwa muji wa polisi hao, mwanamke huyo alikwenda kulalamika katika Ubalozi wa Tanzania nchini India, akidai chombo hicho cha usalama hakifanyi juhudi za kutosha kuwakamata wahalifu hao.

Gazeti hili liliwasiliana na Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ili kujua kama wana taarifa hizo, lakini ofisa mmoja aliyekataa kutaja jina lake kwa maelezo kuwa siyo msemaji, alisema siyo rahisi kumuelewa Mtanzania huyo, hasa kwa kuwa jina lake halijakamilika na pia haijaelezwa mgonjwa wake anaitwaje na anatibiwa katika hospitali gani.

Hata hivyo, alisema wizara italifuatilia suala hilo katika Ubalozi wa Tanzania nchini India.

Loading...

Toa comment