The House of Favourite Newspapers

Zari Ataka Kuzichapa Kikao Cha Familia, Kisa Maamuzi ya Kushangaza

0
Aliyekuwa msiri mkubwa wa baba watoto wake huyo, Lawrence Muyanja ‘King Lawrence’ (kushoto) akiwa na Ivan enzi za uhai wake.

STORI: SIFAEL PAUL NA MTANDAO | IJUMAA | HABARI

KAMPALA: Watatoana roho Yarabi kwa mali alizoacha marehemu! Wengi walitabiri kuwa, kufuatia mtifuano mkali juu ya mali alizoziacha mumewe aliyefariki dunia Mei 25, mwaka huu, Ivan Ssemwanga ‘Don Ivan’, aliyekuwa mkewe, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, ipo siku atazichapa kavukavu na hasimu wake aliyekuwa msiri mkubwa wa baba watoto wake huyo, Lawrence Muyanja King Lawrence.

Aliyekuwa mkewe marehemu Ivan Ssemwanga ‘Don Ivan’, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’.

WATAKA KUVUNJANA SHINGO

Hicho ndicho kilichodaiwa kujiri hivi karibuni ambapo Zari na King Lawrence, ilibidi waamuliwe baada ya kutaka kuvunjana shingo kwenye kikao cha familia ya Ivan kilichofanyika nyumbani kwa marehemu, Muyenga jijini Kampala, Uganda. Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kilichoutonya mtandao maarufu wa habari za udaku nchini humo, Zari na King Lawrence walitaka kutoana roho mbele ya ndugu wa karibu waliokuwa wamekutana kujadili jinsi mali zilizoachwa na marehemu Ivan zitakavyosimamiwa.

King Lawrence (kulia) akiwa na mama yake pamoja na wadogo zake.

UAMUZI WA KUSHANGAZA

Ilidaiwa kuwa, kilichosababisha tafrani hiyo ni kufuatia familia ya Ivan kupitisha uamuzi wa kushangaza kwamba, mali hizo zisimamiwe na King Lawrence, jambo ambalo lilimfanya Zari acharuke kisha kuvaana na jamaa huyo kabla ya kuamuliwa na kikao kuvunjika kwa muda. Hata hivyo, ilielezwa kuwa, katikati ya kikao hicho, familia ilidai kutoa tamko hilo kama mapendekezo tu ili kufungua mjadala wa ishu hiyo kwa sababu King Lawrence alisemekana kujua orodha ya mali zote za Ivan, lakini Zari aligeuka mbogo na macho yake kubadilika rangi na kuwa mekundu.

 ZARI KAMA COBRA

“Sijawahi kumuona Zari akiwa na uchungu au hasira kama ilivyokuwa kwenye kikao kile. Alionekana kama cobra (aina ya nyoka mwenye sumu kali) aliyekuwa kwenye mawindo yake huku akitema sumu,” kilikaririwa chanzo hicho kikieleza ‘mudi’ aliyokuwa nayo Zari aliyekuwa na wanawe watatu aliozaa na Ivan baada ya kusikia kauli hiyo ya familia. Sosi mwingine aliyehudhuria kikao hicho alikaririwa akisema kuwa, katika kikao hicho, ulifika muda Zari akashindwa kuendelea kuwepo hivyo aliondoka huku akifoka kwa hasira. “Wewe (King Lawrence) ni maskini uliyekuwa unamganda Ivan kama kupe anavyomnyonya ng’ombe damu na sasa unajifanya kujua sana mali zake.

 ZARI: NAMCHUKIA KING LAWRENCE

“Wewe (King Lawrence) bila Ivan ulikuwa hujui utakula nini. Sasa kwa kuwa amekufa, unawaza utapata wapi chakula? Nakuchukia,” alisikika Zari huku akiondoka kwenye kikao hicho kwa hasira na watoto wake.

KING LAWRENCE: NAMCHUKIA ZARI

Ilidaiwa kuwa, awali, King Lawrence hakuwepo Uganda na hata mazishi ya Ivan hakuhudhuria kutokana na kuchelewa ndege kutoka nchini Afrika Kusini lakini alipotua tu nchini humo aliingia kwenye vita nzito na Zari juu ya umiliki wa mali alizoziacha Ivan zikitaka kuwatoa roho. “Namchukia Zari kwa sababu anafanya mambo ya kitoto na siyo kama mama,” alisema King

Lawrence katika mahojiano ya simu na chombo kimoja cha habari nchini humo baada ya kikao hicho.

KING LAWRENCE AIBUA JIPYA

Ilielezwa kuwa, King Lawrence amekuwa akisema kuwa anajua vitu vingi kuhusiana na Ivan hivyo kuibua jipya juu ya nyumba ya mojawapo ya nyumba za marehemu Ivan. King Lawrence amekuwa akidai kwamba, hata nyumba ya Ivan ya Muyenga, Kampala ambayo ndipo msiba uliopowekwa kabla ya kwenda kupumzishwa kijijini Nakalilo, siyo ya marehemu kama ambavyo watu wengi wanajua hivyo. “Ni nyumba yangu. Kama kuna watu wanabisha, wanaweza na wanahitaji kuona nyaraka, waje nitawaonesha,” alikaririwa King Lawrence aliyedaiwa kuwa ni binamu wa Ivan. Hata hivyo, kikao hicho ambacho pia kilidaiwa kuhudhuriwa na baba wa Zari, Hassan Tiale kilimalizika kwa kuundwa kamati ya watu wanne kwa ajili ya kusimamia mali za marehemu Ivan.

HATIMAYE ZARI UHAKIKA

Ilielezwa kuwa, kamati hiyo ilimpa jukumu la kwanza Zari kusimamia mali hizo hadi watoto aliozaa na Ivan watakapofikisha umri wa miaka 18. Wengine waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Ritah Ssemwanga (dada wa Ivan),

King Lawrence na George Ssemwanga ambaye ni kaka mkubwa wa Ivan. Katika makubaliano hayo, Zari alitakiwa kusimamia shule za Ivan zilizoko Afrika Kusini kikiwemo chuo chake cha Brooklyn na nyumba mbili zilizopo Sandton na Pretoria, Afrika Kusini. Pia Zari alitakiwa kuishi na watoto wake wote kwenye nyumba moja na nyingine ipangishwe ili kujipatia kipato kwa ajili ya malezi ya watoto hao.

ZARI VS KING LAWRENCE

Zari na King Lawrence wamekuwa kwenye mtifuano kwa muda mrefu hata enzi za uhai wa Ivan ambapo King Lawrence alikuwa akimtuhumu Zari kumwacha Ivan na kumsababishia ‘stresi’. Wakati Ivan akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Steve Biko huko Pretoria, Afrika Kusini, wawili hao walidaiwa kutibuana kiasi cha kutimuliwa na madaktari kwenye chumba cha wagonjwa.

IVAN; KIJANA MTAFUTAJI

Ivan alikuwa kijana mtafutaji aliyewavutia vijana wengi wakitamani kuwa kama yeye ambaye alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa shambulio la moyo na kuzikwa Mei 30, mwaka huu huko Nakalilo ambapo ameacha utajiri mkubwa ambao ndiyo unataka kuwatoa watu roho.

Leave A Reply