The House of Favourite Newspapers

Dalali: Nataka Siku Moja Niwe Rais TFF

0
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali (kushoto) akimkabidhi mkataba Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage wakati wa makabidhiano wa ofisi.

UKIWAZUNGUMZIA viongozi waliowahi kuongoza Simba kwa mafanikio makubwa, kamwe hautasita kumtaja mwenyekiti wa zamani wa Simba, mzee Hassan Dalali, maarufu hivi sasa kwa jina la Trump.

Championi Jumatano linakuletea mahojiano maalumu yaliyofanyika kwenye Kipindi cha Spoti Hausi kinachorushwa na Global TV Online kila Alhamisi saa kumi kamili jioni. Katika mahojiano hayo, Dalali alizungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo mipango yake ya kurejea kuiongoza Simba.

KWA NINI HAUKUGOMBEA URAIS TFF?

“Mimi sina sifa ya kugombea TFF kwa maana ya elimu ya digrii ambayo mimi sina, ili ugombee urais ni lazima uwe na elimu hiyo, hivyo nimepanga kuendeleza elimu yangu ili niifikie hiyo. “Hivyo basi nitagombea miaka ijayo hapo baadaye baada ya kuifikia elimu hiyo ya digrii, hayo ndiyo malengo yangu niliyojiwekea siku moja kuwa rais wa TFF. “Ukiniangalia mimi kama handsome boy, bado kijana, nina umri wa miaka 67 na watoto 18 na wajukuu 34, nikiwa na wake wawili, bado umri unaniruhusu kuongoza soka. “Nashukuru hivi sasa nimemaliza elimu yangu ya sekondari, ya kidato cha nne na nimefanya mitihani ya Necta na nikafaulu vizuri na kukabidhiwa cheti.”

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali.

VIPI UCHAGUZI UJAO, UTAGOMBEA SIMBA?

“Nitakuwa tayari kugombea Simba kama wanachama wenyewe wataniomba nirejee kuiongoza tena klabu yangu niliyoipa mafanikio makubwa. “Nimepanga kurudi TFF baada ya hivi sasa kuwa na vigezo vya kugombea urais wa Simba kwenye uchaguzi, kama unavyofahamu awali kwenye uchaguzi uliopita nilijitoa kwenye mchakato huo kutokana na elimu yangu ndogo.

“Ninashukuru hivi sasa nina sifa za kugombea baada ya kuhitimisha elimu yangu ya kidato cha nne, hivyo basi kama wanachama wataniomba nigombee urais, basi nitarejea kugombea urais Simba. “Ninaomba nisisitize kitu kuwa, mimi sijasoma ili nipate sifa ya kugombea Simba, nimesoma kwa ajili ya kuendeleza maisha yangu ili hata kama ikitokea nafasi ya kazi kwa sifa yangu ya elimu niliyonayo, inaweza kunisaidia baadaye.”

KUMBE MAFANIKIO YOTE ALIYOIPA SIMBA ALIKUWA DARASA LA SABA?

“Nikwambie kitu, mimi kwa elimu yangu ya darasa la saba kabla ya kumaliza kidato cha nne nikiwa mwenyekiti wa Simba, niliipa mafanikio makubwa Simba, sasa fikiria je, kwa elimu yangu hii niliyoiongeza, nitafanya mambo mangapi mazuri? “Nikiwa na elimu yangu hiyo ya darasa la saba, nilinunua Uwanja wa Bunju, nilianzisha Simba Day, tulichukua ubingwa bila ya kufungwa, nilikuta wanachama 500 na kuwaongeza hadi kufikia 5000 ambao nimewaacha na nilitafuta wadhamini wengi kama Breweries na Push Mobile. “Na ndiyo maana nimejiita jina jipya la Trump, ni kutokana na ujasiri wangu nilionao na kujifananisha na Trump ambaye ni rais jasiri mwenye misimamo.”

ANAMKUBALI KADUGUDA KINOMA

“Katika uongozi wangu Simba, nilikuwa navutiwa na Kaduguda (Mwina) ambaye alikuwa katibu wangu, kiukweli ni bonge la katibu mwenye misimamo yake. “Ana upungufu wake kama bin
adamu na digrii zake alizonazo, lakini ni bonge la kiongozi, hayumbishwi na yeye ni kiongozi wa kweli.”

VIONGOZI WA KLABU MNAOGOMBEA, MNAFAIDIKA NA NINI KATIKA TIMU? ”

Kwanza niwapongeze viongozi wa sasa, kwa kufanikiwa kuchukua Kombe la Shirikisho na mwakani timu itashiriki michuano ya kimataifa, kama unavyofahamu muda mrefu Simba haijashiriki michuano ya kimataifa.

“Hivyo, niwapongeze katika hilo, nakumbuka mimi katika uongozi wangu timu iliwahi kuchukua ubingwa bila ya kufungwa, namkumbuka kocha akiwa Phiri (Patrick) na nikwambie kitu tu kila kiongozi akiingia madarakani ana kitu amekifuata. “Mimi binafsi nililelewa na kuzaliwa pale Msimbazi, hivyo nilikuwa naiongoza Simba kwa mapenzi yangu ya klabu na kikubwa nilitaka kuona soka likichezwa uwanjani na sikuwa ninafaidika na chochote.

“Nikwambie nikiwa Simba, niliwahi kuuza friji moja na mafriza mawili ya nyumbani kwangu na mhasibu wangu aliuza gari lake aina ya baloon ili tulipe mishahara ya wachezaji, hivyo utaona ni jinsi gani sikuwa kimaslahi. “Mimi akili yangu ilikuwa ikifikiria mpira tu na siyo kingine na kikubwa nilikuwa nataka nione timu yangu inachukua pointi tatu katika mechi zetu, hivyo hayo mengine mimi sikuwa nayo.”

KUMBE ALIWAHI KUPEWA GARI NA WAZIRI AKAKATAA

“Katika kuonyesha mapenzi yangu na Simba, niliwahi kukataa gari nililotaka kupewa na waziri mkuu mmoja hapa nchini. “Labda nikuhadithie kuwa, siku moja nilikuwa ninaelekea Uwanja wa Kinesi kulipokuwa na mazoezi ya Simba, kipindi hicho nikiwa mwenyekiti. “Nikiwa kwenye gari, alinifuata kijana mmoja na kuchukua mawasiliano yangu na baada ya siku kadhaa nilipokea simu kutoka kwa waziri huyo na kuniambia niende Dodoma na nilipofika huko aliniuliza kwa nini ninatembea kwa miguu bila ya gari?

“Mimi nikamjibu kuwa haya ndiyo maisha yangu, basi akaniambia anipatie gari, niende sehemu nikachukue, mimi nikakataa na kumwambia kiongozi huyo sihitaji gari. “Akaniuliza kwa nini sitaki gari? Nikamjibu kuwa siwezi kuwa na gari wakati wachezaji wangu sijawalipa mishahara, kiukweli kauli hiyo ilimshtua waziri ambaye nisingependa kumtaja jina lake. “Ilikuwa ni ngumu mimi kukubali kupewa gari wakati wachezaji wangu sijawalipa mishahara, hivyo alifanikisha hilo, nashukuru na kuwapatia mishahara wachezaji, hivyo hilo ni somo kwa viongozi wengine.”
WILBERT MOLANDI| CHAMPIONI | MAKALA

Leave A Reply