The House of Favourite Newspapers

IDDI PAZI: NILIKUWA STRAIKA, BAADAYE NIKAWA KIPA BORA

0
IDDI PAZI: NILIKUWA STRAIKA, BAADAYE NIKAWA KIPA BORA
Mkongwe Idd Pazi

NI ngumu sana kutaja majina ya makipa bora waliowahi kutokea nchini Tanzania bila ya kulijumuisha jina la Iddi Pazi Shaaban maarufu kama Father ambaye kwa nyakati tofauti aliwahi kutamba na timu ya Simba. Ingawa kuna klabu nyingi ambazo alizichezea ikiwemo za nje ya nchi lakini idadi kubwa ya Watanzania wanamkumbuka zaidi wakati alipoingia Simba akitokea Majimaji ya Songea kwa lengo la kwenda kuchukua mikoba ya Athuman Mambosasa.

 

Kama kawaida yake Championi Ijumaa, limemtafuta kipa huyo wa zamani, kwa mara nyingine amefunguka mengi kuhusu soka. Pazi ambaye ni baba mzazi wa mshambuliaji, Zahoro Pazi aliyewahi kucheza Simba, hapa anazungumza kuhusu soka kama ifuatavyo:

 

ALIPOANZIA KUCHEZA SOKA

“Nilianza mwaka 1971 kwenye timu iliyokuwa chini ya Jeshi la Polisi Tanzania pale Kilwa Road, kwa wakati huo baba yangu alikuwa anafanya kazi kwenye jeshi hilo. “Lakini ilipofika mwaka 1973 nikaachana na timu hiyo baada ya baba kustaafu, tukarudi mtaani maeneo ya Majumba Sita na kujiunga na timu ya Mogo.

 

ALIKUWA MSHAMBULIAJI KIWEMBE

“Tofauti na umaarufu wangu ambao nimekuja kuupata nikiwa kipa, lakini wakati naanza soka nilikuwa nacheza nafasi ya ndani tena nikiwa mshambuliaji na nilikuwa nafunga kwelikweli, yaani wapinzani wetu walikuwa wanakoma tunapokutana.

 

NDONDO YAMBADILISHA NAFASI

“Lakini bila ya kutegemea nilikuja kubadilika nafasi ya kucheza kwenye moja ya mechi za Ndondo ambapo timu iliyotukodi ilikuwa inacheza na timu ya Kiwanda cha Sungura (Sunguratex). Sasa kwenye mechi hiyo hadi muda wa kuanza mechi unafika hakuna kipa.

 

“Sasa ikabidi mimi nibadilishe niache kucheza ndani na kukaa golini, sasa kitu cha ajabu ni kwamba nilicheza mechi ile vizuri na ikaisha kwa suluhu, baada ya hapo wapinzani wetu walipenda uwezo wangu, kesho yake nikakuta wananiambia nikaungane nao na kusajiliwa timu yao, baada ya hapo nafasi ya kucheza ndani ikafa rasmi.

 

“Lakini pia masuala haya ya ndondo yakanifanya niitwe kwenye kikosi cha Mkoa wa Pwani baada ya kufanya vizuri nikiwa na timu moja inaitwa Kisarawe, wakati huo nikiwa na rafiki yangu Ezekiel Greyson ‘Juju Man’ (baba mzazi wa Aunt, msanii wa filamu) na Ramadhan Madabida.

 

ASAJILIWA BANDARI, AKUTANA NA MZIKI WA YANGA

“Kuna mwaka tukapata safari ya kwenda Mtwara kucheza mechi ya kirafiki, nikiwa huko timu ya Bandari Mtwara ikaniona na kuamua kunisajili kuichezea timu yao kwenye ligi kuu. “Mwaka 1976 ndiyo ikawa mara yangu ya kwanza kuonekana kwenye ligi kuu nikiwa na timu hiyo na mechi yangu ya kwanza kabisa kucheza ni dhidi ya Nyota Afrika ya Morogoro ambayo kwa wakati huo ilisheheni nyota kibao waliotemwa na Yanga.

 

“Mechi hii sitakaa niisahau kwani nilikutana na watu waliokuwa hatari, kama Gibson Sembuli, huyu sifa yake kubwa ni kupiga mashuti ya mbali na kufunga akiwa katikati ya uwanja, mechi hiyo ikaisha sisi tukiwa tumefungwa mabao 2-0, yote akifunga yeye kwa aina hiyohiyo ya kupiga mashuti.

 

AITWA TAIFA STARS, ATUA MAJIMAJI

“Uwezo niliouonyesha ndani ya msimu huo ikiwemo kucheza vizuri mbele ya Simba na Yanga ukanifanya niitwe timu ya taifa, Taifa Stars, kwa mara ya kwanza baada ya kufanya vyema kwenye michuano ya sita bora (bingwa wa ligi kwa wakati huo alikuwa anapatikana kwa njia hiyo ambapo zilikuwa timu sita zinapambana).

 

“Katika mechi hizo za sita bora, ndiyo Simba iliifunga Yanga mabao 6-0, wakati huo Yanga ilikuwa na kikosi kipya baada ya kufukuza wachezaji wake takribani 14, kwa kuwa hawakuwa wamezoeana, ndiyo wakapokea kipigo hicho huku Abdallah Kibadeni akifunga mabao matatu peke yake.

 

Ilikuwa mwaka 1977. “Mwaka uliofuata 1978, nikahama kutoka Bandari Mtwara na kutua Majimaji ya Songea. Mimi na Abdallah Kibadeni ambaye alikuwa Simba, ndiyo tulikuwa miongoni mwa wachezaji wa mwanzo mwanzo kujiunga na Majimaji na kwenda kuipa mafanikio makubwa. “Nilitua Majimaji ikiwa madaraja ya chini tukaipambania hadi ikapanda ligi kuu mwaka 1981, lakini cha ajabu sasa siku ambayo tunatangazwa tumepanda ligi kuu, mimi naondoka na kutua Simba.

 

ASAJILIWA SIMBA, AFUNGIWA KUCHEZA SOKA

“Mwaka 1982 ndiyo rasmi nikawa mchezaji wa Simba, baada ya kusajiliwa kutoka Majimaji ambayo nilitoka kuipandisha daraja msimu mmoja uliopita. “Sasa unajua wakati mimi naondoka Majimaji watu wa huko hawakupendezwa na uondokaji wangu, wakatengeneza zengwe na kusema mimi mchezaji wao halali na nina mkataba nao kwa hiyo nimesajiliwa Simba kimakosa.

 

“Kutokana na suala hilo ikabidi chama cha soka wakati huo kilikuwa kikiitwa Fat, kikaamua kuchukua maamuzi ya kunifungia nisicheze soka kwa msimu mmoja ili kuwapoza watu wote wawili (Simba na Majimaji) kwa kusema kila mmoja apate hasara, hivyo nikawa nimetua Simba lakini sikuambulia kucheza hata kidogo.

 

HAWEZI KUSAHAU WALIVYOFUZU AFCON

“Kwenye moja ya matukio ambayo kamwe sitakuja kuyasahau uwanjani ni juu ya mechi zetu za kuwania tiketi ya kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), hasa ile dhidi ya Zambia. “Naikumbuka mechi hiyo tulianzia hapa nyumbani tukashinda bao 1-0 na tulipoenda kwao ilikuwa tunahitaji sare tu ili tusonge mbele, sasa hadi dakika kama 70 hivi tulikuwa tumefungwa bao 1-0, na mimi nikiwa langoni, mechi ilikuwa kali sana na ushindani mkubwa.

 

“Lakini dakika za mwisho mwisho hivi Peter Tino akafanikiwa kufunga bao, hivyo hadi mechi inaisha ikawa 1-1, tukapata nafasi ya kutinga Afcon kwa mara ya kwanza ambapo mashindano hayo yalifanyika Nigeria mwaka 1980. Unajua baada ya kutinga Afcon waliambiwa nini? Tukutane Ijumaa ijayo.

Na: Said Ally| Champion Ijumaa

Leave A Reply