The House of Favourite Newspapers

MOURINHO AMETUMIA BILIONI 384 KUSAJILI VIUNGO WAKABAJI

0
Kocha wa Manchester United, Mourinho.

DIRISHA la usajili bado halijafungwa, presha kubwa imekuwa ikiongezeka kwa makocha hasa wale wa timu kubwa. Katika Ligi Kuu ya England ‘Premier League’ fedha nyingi zimetumika kusajili washambuliaji kwa kuwa ndiyo ambao wamekuwa na nguvu kubwa ya kuifanya timu ifunge mabao mengi.

Nemanja Matic alitambulishwa kuwa mchezaji rasmi wa Manchester United kwa ada ya euro 45m.

Wiki hii Nemanja Matic alitambulishwa kuwa mchezaji rasmi wa Manchester United kwa ada ya euro 45m (Sh bilioni 117), kiwango hicho cha fedha ni kikubwa lakini kwa Kocha Jose Mourinho kwake ni cha kawaida. Matic ni kiungo mkabaji ambaye ametua kikosini hapo kuongeza nguvu kwa kocha wake huyo ambaye waliwahi kufanya kazi Chelsea na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Premier.

 

Usajili wake ni mwendelezo wa kocha huyo Mreno kusajili aina ya wachezaji wenye nguvu na wapambanaji hasa katika idara ya kiungo cha ukabaji. Mourinho amekuwa ni hodari wa kusajili wachezaji wa aina ya Matic yaani viungo wakabaji ambao ndiyo wamekuwa wakiharibu mipango ya wapinzani kwa miaka mingi katika kila timu anayoifundisha.

 

Kocha huyo ambaye ni baba wa watoto wawili, hajawahi kufeli katika idara hiyo kwa muda wote katika kila timu anayoifundisha na ndiyo ambayo imekuwa kama msingi wa mafanikio yake kiasi cha kuonekana hafundishi soka la kuvutia bali anavuruga mambo kisha timu yake inapata ushindi kiajabuajabu.

 

Mpaka sasa ameshatumia zaidi ya euro 300m (Sh bilioni 384) kusajili wachezaji katika idara hiyo tangu aanze kufundisha soka la kulipwa katika klabu kubwa, kiwango hicho ni kikubwa kuliko idara nyingine zote alizosajili ikiwemo kwenye washambuliaji.

 

Mara nyingi huwa anapenda awe na viungo wengi kisha mshambuliaji anakuwa mmoja mwenye nguvu na mpambanaji ambaye anaweza kumiliki mpira na mzuri katika kufunga. Chelsea (2004-2007) Mourinho alipewa fedha nyingi na bilionea Roman Abramovich ambaye ni mmiliki wa timu hiyo. Akamsajili Michael Essien raia wa Ghana akitokea Lyon kwa euro 38m (Sh bilioni 99).

 

Ilionekana ni fedha nyingi lakini alichokifanya kiungo huyo kinabaki kuwa historia klabuni hapo. Wachezaji wengine aliowasajili kwenye idara hiyo ni John Obi Mikel euro 20m (Sh bilioni 52), Tiago euro 12m (Sh bilioni 31) na Lassana Diarra euro 4.5m (Sh bilioni 12). Inter (2008-2010) Alitawala soka la England akiwa Chelsea, akashindwa kutamba ngazi ya Ulaya, alipotua Inter akataka kukamilisha mipango yake ya kufanya vema kwenye katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

Alifanikiwa kutimiza ndoto ya kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa mara ya pili kwake baada ya awali kufanya hivyo alipokuwa Porto. Viungo waliochangia mafanikio yake ni Thiago Motta na Wesley Sneijder. Motta alitua kwa euro 12m (Sh bilioni 31) akitokea Genoa, mwingine aliyesajiliwa ni Sulley Muntari kwa euro 16m (Sh bilioni 42) akitokea Portsmouth.

 

Real Madrid (20102013) Hapa ndipo ambapo angalau hakutumia fedha nyingi kusajili aina ya wachezaji anaowataka, alimsajili Sami Khedira katika nafasi hiyo akitokea Stuttgart kwa euro 14m (Sh bilioni 37), alikuwa jembe la Mourinho na alifanya kazi nzuri japokuwa hakuwa mchezaji kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo. Chelsea (2013-2015) Alirejea na kukuta kuna wachezaji wengi tofauti na aliowaacha wakati anaondoka, alichoamua ni kumrejesha Matic ambaye aliondolewa kikosini hapo kwa kuonekana hafai, lakini euro 25m (Sh bilioni 65)  zikamfanya arudi Chelsea akitokea Benfica na alikuwa jembe kweli kwa Mourinho.

 

Manchester United (2016-sasa) Mourinho ni shabiki wa Matic, ameamua kumsajili kwa mara nyingine, akiwa Old Trafford alifanya mabadiliko kadhaa kwenye kiungo japokuwa hakupata kile alichokuwa akikihitaji. Alimsajili Paul Pogba kwa euro 105m (Sh bilioni 274) akiwa ni kiungo mshambuliaji lakini mara kadhaa alimtumia kama kiungo mkabaji, kwenye nafasi ya kiungo mkabaji alipata tabu, akalazimika kumtumia Ander Herrera ambaye awali alikuwa kiungo wa mbele, pia alimtumia Marouane Fellaini katika nafasi hiyo.

 

Pamoja na kuwatumia wachezaji hao katika nafasi hiyo lakini ilionekana wanapata wakati mgumu kumuelewa, ndiyo maana ameamua kumsajili mchezaji ambaye anahisi anaweza kutumia kauli chache akamuelewa anachotaka.

 

Mourinho anapenda kuwa na mchezaji mwenye roho ya ‘kikatili’ hasa katika nafasi hiyo, aina ya ufundishaji wake ni kama anataka mchezaji ajitoe kwa kila kitu kwa ajili ya timu, ndiyo maana hata aina ya soka la Herrera lilibadilika alipokuwa akicheza katika nafasi hiyo, akawa mbabe na mwenye kutumia nguvu tofauti na ilivyokuwa awali.

Stori: Champion Ijumaa, Global Publishers

Leave A Reply