The House of Favourite Newspapers

NIYONZIMA: SINA MANENO MENGI, TUKUTANE UWANJANI

0
Mayanja akimnyoosha viungo, Niyonzima.

 

KIUNGO Mshambuliaji wa Simba raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima ametambulishwa rasmi katika kikosi cha timu hiyo na anatarajiwa kuwa mmoja wa wachezaji watakaoshuka dimbani leo Jumanne katika mchezo wa Simba Day dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

 

Niyonzima aliyejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga, jana Jumatatu asubuhi alifanya mazoezi kwa mara ya kwanza na timu yake hiyo mpya kabla ya kutambulishwa mchana mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Kariakoo jijini Dar.

 

Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, Niyonzima alisema yeye kwa sasa ni mchezaji wa Simba hivyo mashabiki wasubirie kuona kazi yake uwanjani. “Mimi kwa sasa ni mchezaji wa Simba, mambo mengine yataonekana uwanjani, sina cha ziada cha kuzungumza,” alisema Niyonzima.

Niyonzima (kushoto) akifanya mazoezi kwa kufuata maelekezo ya kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja.

Aidha, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema: “Tuna timu nzuri yenye wachezaji wazuri na uongozi umeweza kutupeleka kambi Afrika Kusini na tumeweza kucheza mechi mbili za kirafiki, tumeona viwango vya wachezaji wetu na mechi ya kesho ‘leo’ itatusaidia kuangalia fitnes za wachezaji wetu, na tumejiandaa vizuri kwa ajili ya ligi.”

 

Naye, nahodha wa Simba, Method Mwanjale alisema msimu huu watakuwa na kikosi kizuri ambacho kitawasaidia kuleta ushindani katika ligi na michuano mbalimbali. Aidha, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara aliyekuwa akiwatambulisha wachezaji hao, alisema Rayon Sports ilitarajiwa kuwasili nchini jana saa 3:00 usiku kwa ajili ya mechi hiyo ambayo itatanguliwa na mechi ya Simba B dhidi ya Rangers.

 

Mgeni rasmi katika Tamasha la Simba Day anatarajiwa kuwa Januari Makamba ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Anayeshughulikia Muungano na Mazingira na kudai kuwa uwanja utafunguliwa kuanzia saa 4:00 asubuhi.

 

Manara aliongeza kuwa leo itakuwa siku maalumu ya kumkabidhi Tuzo ya Mchezaji Bora ya Mashabiki beki wake, Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’.

Na: Khadija Mngwai na Sweetbert Lukonge| Champion Jumanne

Leave A Reply