The House of Favourite Newspapers

Wanaodaiwa Kumuua Mwanaharakati wa Wanyamapori Wafikishwa Kortini

0
Watuhumiwa hao wakifikishwa kortini.

WATUHUMIWA wa mauaji ya mwanaharakati wa kuhifadhi Wanyamapori raia wa Afrika Kusini, Wayne Lotter, aliyepigwa risasi na kuuawa maeneo ya nyumbani kwake, Masaki jijini Dar wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo.

Watuhumiwa hao ambao ni Rahman Almas, Mohammed Maganga na Khalid Almas Mwinyi na Rahma maarufu ‘Baby’ wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka mawili ya kukutwa na silaha pamoja na kosa la mauaji.

Watuhumiwa hao wakifikishwa kortini.

Aidha watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo hivyo hakimu, Wilbard Mashauri ameahirisha hadi Oktoba 23.

Lotter alikuwa mwanzilishi wa PAMS Foundation, shirika ambalo limekuwa katika mstari wa mbele kusaidia kupambana na uwindaji haramu na biashara ya pembe za ndovu nchini. Polisi jijini Dar es Salaam wanasema wanachunguza waliotekeleza mauaji hayo, wakati huu ikiwa bado haijafahamika ni kwa nini aliuawa na waliohusika.

Lotter.

Waliofanya kazi na mwanaharakati wa mauaji ya tembo Lotter akiwemo Jane Goodall, raia kutoka Uingereza na Michel Lanfrey raia wa Ufaransa wamemwelezea mwanaharakati huyo kama shujaa aliyefanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa uwindaji haramu unapungua nchini.

 

Inadaiwa kuwa, kabla ya kuuawa kwake, alikuwa amepokea vitisho kuhusu kazi yake lakini pia upinzani mkali kuhusu jitihada zake za kuzuia uwindaji haramu. Shirika la PAMS International linaifadhili Serikali ya Tanzania kupitia taasisi maalum ya kufanya uchunguzi na kuwakamata wawindaji haramu na takwimu zinaeleza kuwa wawindaji karibu 900 wametiwa mbaroni.

Leave A Reply