The House of Favourite Newspapers

Sh 200m Kumng’oa Ajibu Yanga

Ibrahim Ajibu.

IBRAHIM Ajibu ambaye mpaka sasa ndiye kinara wa asisti Ligi Kuu Bara akiwa kapiga sita katika mechi sita kwenye kikosi cha Yanga, tayari ameshawekwa sokoni rasmi baada ya meneja wake kutaja thamani ya mteja wake huyo.

 

Ajibu ambaye hucheza nafasi ya ushambuliaji kwenye kikosi cha Yanga, alijiunga na vijana hao wa Jangwani msimu uliopita akitokea kwa watani zao wa jadi, Simba kwa Sh milioni 70 na gari.

 

Hivi karibuni baada ya kuonyesha uwezo mkubwa kwenye ligi, Simba wanaripotiwa walianza mchakato wa kutaka kumsajili nyota huyo ili arejee ‘nyumbani’ kufanyakazi.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Meneja wa Ajibu, Athuman Ajibu ameweka wazi kuwa kutokana na kiwango kikubwa ambacho mteja wake anakionyesha sasa hivi thamani yake ni Sh milioni 200 lakini hata hivyo akatoa angalizo.

 

Angalizo lenyewe ni kwamba wanasubiri kuona kama Ajibu atafanya vizuri kwenye mechi za mikoani ambazo huaminika kuwa ni ngumu kutokana na ubovu wa viwanja, hivyo kama atafanikiwa kuonyesha kiwango kama kile alichokuwa akikionyesha wakati Yanga ikicheza Uwanja wa Taifa jijini Dar basi hakutakuwa na shida na mkwanja huo.

 

Alisema kwa sasa wamekuwa wakifanya kikao cha familia mara kwa mara na mchezaji huyo kubwa wakimsisitiza asibweteke na mafanikio aliyoyapata kwenye mechi za Dar, afanye hivyo na kwenye mechi za mikoani ili thamani yake izidi kupanda kila siku lakini pia yeye ni tegemeo ndani ya familia yao.

 

Meneja huyo pia alisema, Simba ambao pia walikuwa wakizungumza na mchezaji huyo, kwa sasa wamesitisha kutokana na suala la kutekwa kwa mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’ na watu wasiojulikana Oktoba 11, mwaka huu wakati akienda kufanya mazoezi ya gym kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar.

 

“Kwa sasa bado tunaangalia ligi hadi ifike katikati kwa kuwa mechi bado sana, tunasubiri kidogo isogee kama mechi 10 hivi, hadi atoke mikoani huko hapo ndiyo tutaangalia ni wa Taifa au na mikoani, lazima tuwe na vipimo vyote viwili.

 

“Kama akifanya vizuri mikoani basi tunaweza kucheza naye hadi kwenye Sh milioni 200. Huwa tunakaa naye kikao kama familia hasa kwa kuwa yeye ndiye nyota tunayemtegemea, tunamtaka aache utani afanye kazi asibweteke na mafanikio ya Dar na nje (mikoani) akaze pia.

“Kwa upande wa Simba hesabu zimesimama kwa sasa kwa kuwa viongozi wengi wapo bize na hii ishu ya Mo kutekwa,” alisema meneja huyo.

Stori na Lunyamadzo Mlyuka | Championi Ijumaa

Comments are closed.