The House of Favourite Newspapers

Uvimbe wa Kizazi ‘Uterine Fibroids’

VIMBE wa Fibroid pia unajulikana kwa majina kama Leiomyoma, Myomas na Fibromyomas. Uvimbe huu siyo kansa na mara chache sana unaweza kuwa kansa, unachipuka au kuota kutoka katika misuli laini ya kizazi.

Fibroid husababisha mwanamke apate damu ya mwezi bila mpangilio ambapo inaweza kuendelea katika siku zake kwa muda wa zaidi ya siku saba au ikatokea katikati ya mzunguko.

Mwanamke mwenye uvimbe wa Fibroid ambao ni mkubwa hupatwa na maumivu chini ya tumbo yanayozunguka kiuno, kuhisi uzito chini ya kitovu na kila mara huenda haja ndogo kama ana ujauzito, wakati mwingine hata choo kikubwa hupata kwa shida na ujauzito unaweza kutoka kama anao.

Uchunguzi wa Fibroid kubwa ni rahisi kulinganisha na ndogo lakini uchunguzi wa kina hufanyika hospitali kwa daktari wa magonjwa ya akina mama, pia kuhusu tiba yake tutakuja kuona kwa undani lakini imegawanyika kutegemeana na hali ya mgonjwa hasa kama ana lengo la kuzaa.

TATIZO LINAVYOTOKEA Uvimbe wa Fibroid ni maarufu sana katika jamii yetu na hasa miongoni mwa wanawake wengi, uvimbe huu huwapata takriban asilimia sabini ya wanawake waliofikisha umri wa miaka arobaini na tano ingawa pia hutokea sana chini ya umri huo.

Fibroid hutokea zaidi kwa wanawake wa Afrika kulinganisha na Wazungu, pia huwapata zaidi wanawake wanene au wenye miili mikubwa ingawa hata wa wastani pia hupata.

Inasadikiwa kwamba, mojawapo ya vigezo vinavyomfanya mwanamke aweze kuepuka kupata uvimbe huu ni kuzaa mara kwa mara na uvutaji wa sigara ambao ni hatari kwa maisha yako.

Uzazi wa mara kwa mara pia ni hatari kwa afya ya mama. Aina nyingi za uvimbe huu hutokea nje ya kizazi na ukifuatiwa ndani ya misuli ya kizazi.

Mara chache utaukuta uvimbe huu upo ndani ya kizazi. Uvimbe pia huweza kuota katika mishipa mikubwa inayoshikilia kizazi, katika mirija ya kizazi au nje ya kizazi.

Kwa kawaida Fibroid huwa nyingi, unapoona kwenye Ultrasound kama ipo moja, basi ujue zipo nyingi nyingine ni ndogo sana. Fibroid hukua taratibu na hutegemea uwepo wa homoni ya Estrogen .

Mwanamke aliye katika umri wa kuzaa, Fibroid hukua kwa kasi kulinganisha na yule ambaye umri wake wa kuzaa umeisha na wamefunga hedhi, mwanamke akifikia hapa kama amegundulika na Fibroid basi itaanza kusinyaa yenyewe.

DALILI ZA FIBROID

Mwanamke mwenye Fibroid hulalamika kutopata ujauzito au alipata ukatoka, damu ya hedhi hutoka bila ya mpangilio. Haja ndogo huenda mara kwa mara na hata haja kubwa haitoki vizuri. Mwanamke huhisi uzito chini ya tumbo, historia ya mimba kutoka zenyewe au kupatwa na uchungu mapema na kuzaa mtoto njiti vilevile uvimbe unaweza kusababisha mtoto akakaa vibaya tumboni mwa mama.

UCHAMBUZI

Kipimo cha Ultrasound ndicho hasa hutumika kuutambua uvimbe. Kipimo kingine kinaitwa ‘BPE’ au Bimanual Pelvic Examination ambacho kitafanywa na daktari bingwa kuangalia jinsi uvimbe ulivyo na tabia zake. Kipimo hiki kitafanyika kabla au baada ya Ultrasound .

BPE pia itaelekeza jinsi ya kuutibu uvimbe na kama unaweza kuzuia mimba isiingie au isikue. Vipimo vingine itategemea hali ya mgonjwa na daktari atakavyoona inafaa. Mfano endapo mgonjwa ana kila dalili ya upungufu wa damu, maambukizi kwenye kizazi au shinikizo la damu lipo juu.

MATIBABU. Tiba inategemea na endapo mgonjwa anahitaji watoto au la, endapo mgonjwa ana umri wa kuzaa au umri umeshapita na jinsi uvimbe huo unavyomuathiri mgonjwa. Daktari ataangalia vigezo hivyo na kutoa ushauri. Matibabu yanaweza kuwa dawa tu, upasuaji wa kuondoa uvimbe, tiba ya kuondoa kizazi au kuuacha tu wenyewe usinyae hasa kwa walio na umri mkubwa.

Uchunguzi na tiba hupatikana katika kliniki za madaktari bingwa wa magonjwa ya akina mama katika ngazi ya hospitali ya mkoa. Wahi hospitali.

Comments are closed.