The House of Favourite Newspapers

Ni kwa nini umfungulie mke wako  biashara?

0
Happy young woman in the shopping mall standing near cashiers desk while shop assistant packs the purchase
Happy young woman in the shopping mall standing near cashiers desk while shop assistant packs the purchase

Ni wiki nyingine tena tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba Mungu amekujaalia uzima na unaendelea vyema na mchakamchaka wa maisha kama kawaida.

Mimi nimshukuru Mungu kwa kila jambo kwani nikianza kuhesabu yale aliyonifanyia katika maisha yangu, nakosa hata maneno sahihi ya kumshukuru ila kwa kifupi niseme tu kwamba; Asante Mungu!

Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nataka kuzungumzia kitendo cha baadhi ya wanaume kuwafungulia biashara wake zao ili wasikae tu nyumbani na pia washiriki katika kujiongezea kipato.

Ni wazo zuri!

Katika maisha ya sasa yaliyotawaliwa na changamoto nyingi, itakuwa ni jambo la kushangaza endapo mwanamke atakubali kukaa tu nyumbani ili kumstarehesha mume wake.

Mwanamke anayejua maana halisi ya maisha ni lazima atakuwa mchakarikaji hivyo kama mwanaume ameoa mwanamke asiye na ajira, si jambo baya endapo atamfungulia biashara yoyote ambayo anaona anaimudu.

Kikubwa katika hili ni kuangalia biashara ambayo itafanyika bila hasara na mwanamke husika awe anaimudu.

Usifikirie kumfungulia duka, genge au saluni mkeo eti ili awe na sehemu ya kumuweka bize, ukifanya hivyo utakuwa unakosea.

Unamkuta mwanaume eti anamfungulia duka mkewe halafu anasema amemtafutia sehemu ya kuzugia, yaani lile duka ni sehemu tu ya kuzugia na siyo sehemu ‘siriasi’ ya kujiingizia kipato.

Wanaowafungulia wake zao duka kwa sababu hizo wakati mwingine hawajali kama kuna faida au hasara. Yaani ilimradi linafunguliwa na kufungwa.

Bidhaa zikiisha, mwanaume anatoa pesa zake, ananunua bila kujua faida na hasara.

Kwa kufanya hivyo si bora mkeo angebaki tu nyumbani? Kuna faida gani sasa kumfungulia biashara hiyo halafu haina faida? Eti unamfungulia saluni wakati hana uzoefu na mambo hayo, matokeo yake sasa anageuza eneo hilo kuwa la umbeya.

 

Kwa nini umfungulie biashara?

Wanaume wengi sana hujikuta njia panda pale ambapo huoa wanawake kisha wakapata wazo la kuwaanzishia biashara. Hata hivyo, kabla ya kumfungulia mkeo biashara, jiulize maswali yafuatayo;

Kwa nini umfungulie biashara na siyo kazi nyingine? Je, unadhani hiyo kazi ataimudu na kuiendesha kwa faida? Je, uzoefu anao?

Ukiacha maswali hayo, pia jiulize, biashara unayoifungua haitateteresha ndoa yenu? Kwamba endapo atakuambia ana uzoefu na biashara ya kusafiri kwenda mikoani, utakuwa tayari kumruhusu na ukabaki na amani?

Je, akikuambia ana uzoefu wa kazi ya baa, uko tayari kumfungulia? Hayo ni baadhi ya maswali ya kujiuliza na majibu yake yatakupa mwanga wa kufanya maamuzi sahihi.

Lakini ninachotaka kukutahadharisha ni kwamba, usimfungulie mkeo biashara ya duka, saluni au genge ili kumbana asikusaliti.

Nasema hivyo kwa kuwa wapo wanaotumia mbinu hiyo kuwabana wake zao.

Kama ulikuwa hujui ni kwamba, kumfungulia mkeo biashara siyo mbinu ya kumzuia asikusaliti. Akiamua anaweza kukuzunguka na usijue, tena inawezekana fedha atakazokuwa anahongwa akajumlishia kwenye mtaji.

La kuzingatia

Biashara inahitaji uzoefu. Kama mkeo anamudu mambo ya biashara, akawa tayari wewe umuanzishie, fanya hivyo lakini kama hajui mambo hayo, bora afanye kazi nyingine au ikishindikana akae tu nyumbani.

Na wewe mwanamke, kama umeona mumeo ana pesa za kukupatia mtaji, anzisha biashara ambayo unaamini itakupatia kipato. Usianzishe biashara ya saluni kisa umemuona shosti wako anayo.

Leave A Reply