The House of Favourite Newspapers

Fahamu ugonjwa wa homa ya manjano kwa watoto wachanga

LEO tunaangalia na kujadili kwa upana homa ya manjano kwa watoto wachanga. Homa ya manjano ni ugonjwa unaowakumba zaidi watoto wachanga baada ya kuzaliwa japokuwa hata watu wazima huweza kupata maradhi haya. Hali ya mtoto kuwa wa njano kitaalam inaitwa Neontal Jaundice, husababishwa na kemikali inayoitwa Bilirubin kuzalishwa kwa wingi kwenye damu ya mtoto.

Bilirubin inapokuwa nyingi humletea mtoto madhara. Watoto wa kiume ni rahisi kupata manjano kuliko watoto wa kike na asilimia 80 ya watoto njiti hupata homa ya manjano wakiwa na siku tano mpaka saba baada ya kuzaliwa. Mtoto kwa kawaida huonesha rangi ya manjano kwenye macho, paji la uso, nyayoni, viganjani, kifuani na tumboni, ukimkagua mtoto vizuri hasa kwenye mwaga wa jua utaona ana rangi ya njano kwa urahisi.

DALILI ZA HOMA YA MANJANO

Mtoto ataonesha dalili tofauti, anaweza akaonesha zote kwa pamoja au baadhi yake, kwa mfano macho ya mtoto na ngozi kubadili rangi kuwa ya njano, kuwa na homa kali, mtoto kutapika, kulala sana na mkojo kuwa wa kahawia (brown). Ukiona dalili hizi ujue kwamba ni za hatari, hivyo muwaishe mtoto hospitali akaonwe na daktari kwa matibabu.

SABABU ZA UGONJWA

Sababu zinazomfanya mtoto apate manjano zipo nyingi kama vile mtoto anapokuwa na kundi tofauti la damu (blood group) na mama yake anakuwa na hatari ya kupata manjano. Sababu ya pili ni mtoto kuwa njiti (premature) huwa ni rahisi kupata manjano, tatu; watoto waliozaliwa na matatizo ya kiafya au maambukizi (infection) na nne; akina mama wenye kundi O la damu (blood group O) wana hatari ya kusababisha mtoto wake kupata manjano.

Sababu nyingine ni mama anayepata kisukari kipindi cha mimba kitaalam Gestational Diabetes anaweza kujifungua mtoto mwenye manjano. Lakini pia mama kuzalisha maziwa machache kunaweza kumsababishia mtoto kupata manjano au mtoto mwenye matatizo ya ini naye hupata manjano.

Mtoto anapopata manjano ni vizuri kutibiwa haraka iwezekanavyo la sivyo mtoto atapata haya matatizo ya kemikali ya Bilirubin kuongezeka sana kwenye damu ya mtoto na kuathiri ubongo, kumsababishia matatizo ya kutosikia, kutoona, kushindwa kuongea na kutembea vizuri au kupata ulemavu wa kudumu au kufariki dunia.

TIBA

Manjano hutibika kwa njia tofauti na huchukua siku saba mtoto kupona iwapo hatakuwa nayo nyingi mwilini, kama ni nyingi zaidi itamchukua zaidi ya siku saba.

Maziwa ya mama ni tiba kubwa, mama anatakiwa kunyonyesha mtoto kwa wingi ili kupunguza kiasi cha Billirubin iliyozalishwa kwa wingi kwenye damu ya mtoto. Mtoto atolewe nje apigwe na jua kwani linasaidia kupunguza ile sumu.

Mtoto, akiwa na hali mbaya ya manjano akipelekwa hospitali daktari atamuwekwa kwenye kifaa kiitwacho Phototheraphy Light kwa saa 48 au zaidi mpaka daktari atakapoona sumu imeisha mwilini. Anapokuwa kwenye Phototheraphy atafunikwa macho ili ule mwanga usimwathiri macho yake, joto atakalopata huzuia mzunguko wa Billrubin kwenye damu ya mtoto. Njia nyingine ni kubadilishwa damu ila njia hii atafanyiwa iwapo hali yake inaonyesha ni mbaya zaidi.

USHAURI

Maziwa ya mama ni muhimu sana kwa mtoto, kama ana manjano hakikisha unamnyonyesha kila baada ya saa 2 ili kuondoa manjano kwa haraka na kuokoa maisha ya mtoto, ikiwa unaona dalili tulizozitaja muwahishe mtoto hospitalini. Kwa ushauri zaidi tupigie simu, lakini kama maziwa hayatoki kwa mama hakikisha unamnunulia (baby formula) maziwa ya kopo.

Ni vizuri pia mama kula miwa kipindi cha ujauzito wake kwani inasaidia kuepusha mtoto kuzaliwa na manjano

 MAKALA | AFYA

Comments are closed.