The House of Favourite Newspapers

Hivi Ndivyo Ilivyokuwa Safari ya Mwisho ya Martha – (Video + Pichaz)

DAR ES SALAAM: Baada ya kusambaa kwa taarifa za msiba wa aliyekuwa mchekeshaji maarufu wa kike Bongo, Martha Michael Mshilole ‘Boss Martha’ (24), kumeibuka mambo mengi huku mwanamuziki wa Bongo Fleva, Mbwana Yusuf Kilungi ‘Mbosso’ akiingia matatani.

Gazeti la Ijumaa limechimba.

Familia ya Martha imekuja juu na kumsaka (wanted) Mbosso kwa kile inachodai ni kupotosha umma kuwa amezaa na msanii huyo, jambo ambalo si kweli.

KABLA YA FAMILIA

Saa kadhaa baada ya taarifa za kicho cha Martha, Mbosso ambaye ni memba wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram akionesha kuguswa na msiba huo kwa madai kwamba amezaa na Martha.

Maneno hayo yalizua mjadala mpya kuwa inakuwaje yanazungumzwa baada ya Martha kufariki dunia?

MBOSSO SASA

Katika maelezo yake, Mbosso alitoboa siri kwamba aliwahi kuwa kwenye uhusiano na Martha na kupata mtoto wa kiume ila mchekeshaji huyo hakutaka suala hilo kuwa wazi kwa sababu za kifamilia.

Alisema licha ya kuwa wao walipendana, familia ya mchekeshaji huyo haikupenda Mbosso kuwa na Martha.

“Martha nilikuwa naye karibu kuanzia urafiki hadi kwenye uhusiano na kufikia hatua ya kupata mtoto ambaye ana miaka minne sasa, lakini familia yake haikuridhishwa na mimi,” alisema Mbosso na kuendelea;

“Tulipambana sana, lakini mwisho wa siku tukaamua kila mtu aendelee na maisha yake na yeye akaniomba tusiwe tunazungumzia kuhusu uhusiano wetu wala mtoto tuliyempata.”

WAKANA UHUSIANO

Mbosso alisema mwanzoni alipata shida kukubaliana na ombi hilo, lakini baadaye alielewa na wote wakawa wanakana kuhusu uhusiano wao kila walipoulizwa.

Alisema licha ya kuachana, waliendelea kuwa marafiki na kuwasiliana kwa ajili ya mtoto wao.

NENO LA MWISHO

“Niliwasiliana naye akaniambia anataka kuhama Sinza (Dar) ahamie Mbezi-Beach na akanitumia picha za nyumba lengo lilikuwa amchukue mtoto ambaye yuko Tabora kwa sasa, wahamie nyumba mpya, mimi nilikuwa bize kidogo nikamwambia na mimi nilikuwa ninahama Tegeta ninahamia Mbweni.

“Mara ya mwisho aliniambia kichwa kinamuuma, nikajua ni malaria au uchovu sikujua kama ndiyo kingechukua uhai wake,” alisema Mbosso akitokwa na machozi.

TURUDI KWA FAMILIA

Jana, Gazeti la Ijumaa lilifika nyumbani kwa wazazi wa Martha, Mbondole Kwa Mhaya, Kinyerezi jijini Dar na kuzungumza na ndugu wa Martha ambapo walichachamaa wakidai kuwa wanamsaka ili anyooshe maelezo yake vizuri.

“Huyo Mbosso huku yupo wanted (anasakwa) anyooshe maelezo kwa sababu ametuchafua sisi kama ndugu kwenye mitandao ya kijamii.

“Anasema amezaa na Boss Martha, jambo ambalo si kweli, tunamtaka aje hapa anyooshe maelezi kwa sababu tunajua ndugu yetu hakuna na mtoto,” alisema mmoja wa ndugu wao aliyeonekana kuwa na jazba kiasi cha kukataa kutaja jina lake.

MAMA MARTHA

Kwa upande wake mama wa marehemu Martha, Pendo Bariki alieleza kusikitishwa kwake na madai ya Mbosso kuwa amezaa na binti yake.

“Si kweli, mwanangu hana mtoto na huyo Mbosso na kama akija kwenye msiba labda aje kama rafiki au waombolezaji wengine na siyo kama mzazi mwenzake na mwanangu maana mwanangu hana mtoto,” alisema mama huyo na kushindwa kuendelea na mahojiano kisha kumpisha dada wa Martha azungumze na wanahabari wetu.

Kwa upande wake, dada wa Martha aliyejitambulisha kwa jina la Lucy Enosi alisema anachojua ni kwamba mdogo wake hana mtoto hivyo Mbosso aache kuchafua familia yao.

“Tumemsikia huko mitandaoni akidai amezaa na Martha, ukweli ni kwamba Martha hakuwa na mtoto,” alisema Lucy akiangua kilio na kushindwa kuendelea na mahojiano.

TUMRUDIE MBOSSO

Alipotafutwa Mbosso na kujulishwa juu ya kuchachamaa kwa familia ya Martha na kusema si kweli kwamba amezaa na mrembo huyo, jamaa huyo alisisitiza kuwa aachwe apumzike.

UNDANI KILICHOMUUA MARTHA

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kipindi cha Cheka Tu alichokuwa akifanyia kazi Martha, Coy Mzungu, msanii huyo alifikwa na umauti baada ya kuugua ghafla.

Coy alisema Martha aliugua ghafla ugonjwa wa uti wa mgongo ambao ulisababisha kupata malaria kali.

Alisema, awali Martha alilazwa Hospitali ya Sinza-Palestina kisha kuhamishiwa hospitali nyingine (Kisarawe, Pwani) ambapo ndiko umauti ulipomkutia.

Ugonjwa unaotajwa hasa kumuua Martha ni uti wa mgongo ambao ulisababisha kupatwa na malaria kisha kifo.

DAKTARI AFAFANUA

Kwa mujibu wa Daktari wa Gazeti la Ijumaa, Dk Godfrey Chale, ugonjwa wa uti wa mgongo hutokea iwapo utando unaofunika ubongo na uti wa mgongo utapatwa na maambukizi.

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya makundi ya bakteria na hata fangasi. “Tukivigawanya visababishi hivi katika makundi haya, tutaona kuwa bakteria wanaosababisha ugonjwa wa uti wa mgongo ni kama vile; bakteria wajulikanao kama Beta-streptococci, Hemophilus influenza, Escherichia coli, Listeria monocytogenes, Neisseria meningitides, Streptococci pneumoniae na Mycobacteria tuberculosis.

“Vimelea vya fangasi ambavyo hujulikana kwa kusababisha ugonjwa wa uti wa mgongo ni pamoja na wale wajulikanao kama Coccoidiodomycosis na Cryptococci meningetides.

DALILI

“Dalili na viashiria vya uti wa mgongo ni pamoja na shingo kukakamaa, mgonjwa kujihisi homa kali, maumivu makali ya kichwa, mgonjwa kupoteza fahamu, kupatwa na degedege (seizures) na mwili kukakamaa.

MATIBABU

“Matibabu ya ugonjwa huu ni pamoja na kuhakikisha mgonjwa anapumua vizuri na njia za hewa ziko wazi. “Iwapo itathibitika kuwa bakteria ndiyo wanaosababisha ugonjwa huu, mgonjwa anaweza kupewa mojawapo ya dawa za antibiotiki kama cefotaxime au Cefriaxone,” alisema Dk Chale.

ALIKIONA KIFO? Maneno ya mwisho aliyoandika msanii huyo Agosti 16, mwaka huu kwenye ukurasa wake wa Instagram wenye jina Bossmarthatz yaliwahuzunisha wengi hadi kufikia hatua ya kuamini kuwa pengine alikuwa amekiona kifo chake.

Martha aliandika; “Oh Jesus when you will call my name

I’ll be happy to say am ready to come home.”

Kwa tafsiri isiyo rasmi alimaanisha kuwa Oh Yesu utakaponiita jina langu, nitakuwa na furaha kusema niko tayari kuja nyumbani.

Maneno hayo ambayo yalisadikiwa kuwa ni sehemu ya wimbo fulani yalionekana kugusa mioyo ya rafiki zake hasa pale taarifa za kifo chake ziliposambaa.

ENZI ZA UHAI

Enzi za uhai wa Martha aliwahi kufanya kazi nyingi ikiwemo kuwa mmoja wa wachekeshaji waliokuwa wakifanya standup comedy ya Cheka Tu na kukonga nyoyo za wengi.

Shoo hiyo ya Cheka Tu hufanyika kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi.

BONGO FLEVA

Martha pia aliwahi kushiriki kwenye baadhi ya kazi za wasanii wa Bongo Fleva kama kwenye video ya Whozu yenye jina la Roboti.

MAZISHI

Mwili wa Martha aliyezaliwa mwaka 1995 jijini Mwanza, ualizikwa jana Ijumaa, katika Makaburi ya Kinyerezi jijini Dar.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina! –Mhariri.

Comments are closed.