The House of Favourite Newspapers

Kauli za JPM Akizindua Rada Dar, Amtaja Tundu Lissu- Video

RAIS John Magufuli amezindua mradi wa usimikaji wa rada katika Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam. Mradi huo unahusisha viwanja vinne vya ndege vilivyopo Kilimanjaro, Mwanza, Songwe na JNIA-Dar es Salaam.

Baadhi ya kauli za Rais Magufuli ni zifuatazo:

“Ukiona hadi watu wanakamata ndege zetu basi ujue shirika letu linafanya kazi vizuri. Ni kama ule wimbo wa Sauti Sol wanasema, wakifunika tunafunua, wakitufungia mlango, wanatukuta ndani, wakianika, tunaanua.”

 

“Nimefurahi kumuona hapa Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu. Spika nikuahidi kuwa, miradi ya maji uliyoisemea kwenye jimbo lililokuwa limetelekezwa, lilikuwa la Tundu Lissu, serikali yangu itahakikisha inapelekwa haraka, ili wale waliokuwa hawana mbunge nao wafaidi kama wengine.”

“Wakati Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) linaanza kazi, ilikuwa inamiliki asilimia tatu ya soko la ndani, lakini sasa linamiliki asilimia 75 ya soko hilo. Na tayari tumeanza safari katika soko la kimataifa, tunakwenda Afrika Kusini, India na nchi nyingine, na karibuni tutaanza kwenda nchini China.”

 

“Ndege yetu iliyoshikwa kule Afrika Kusini tumeiandika Dodoma. Sasa walipoiona kule wakajua ni Wagogo wameenda kuomba misaada. Watani zangu wagogo tutajenga uwanja mkubwa wa ndege wa kimataifa pale Msalato, Dodoma tutautafutia jina zuri, wananchi watautumia na waheshimiwa wabunge pia watautumia.”

“Kwa kweli Johari wewe ni johari kweli kwenye kazi (akimsifia Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, Hamza Johari) yaani kwenye ufanisi wa kazi yupo makini sana, ningekuwa na binti ningempa.”

 

“Namshukuru Balozi wa Ufaransa kwa kuzungumza Kiswahili kizuri sana. Huyu baba ametoka Ufaransa kule amefika hapa hivi karibuni lakini anapiga Kiswahili. Unafikiri akimfuata mwanamke atakataa kwa Kiswahili cha namna hii? Hii ndo faida ya kujua Kiswahili.”

“Nyote huwa mnajua mimi huwa sipendi kabisa miradi inayoishia njiani, na ndiyo maana leo nimefurahi sana. Naomba nimpongeze kwa dhati Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Johari, sina zawadi ya kumpa ila mwaka huu akitaka kwenda hija nitamlipia gharama ili akamshukuru Mungu.”

 

“Tukiwachekea hawa wakandarasi, tutaliwa. Kuna mtu anapenda kuliwa jamani? Kwa kuibiwa fedha zake?  Yaliwahi kutengwa mabilioni ya fedha ili kununua rada lakini haikununuliwa. Aliyehusika kule Uingereza alijiuzulu lakini huku kwetu labda watajiuzulu siku zijazo. Yawezekana ndiyo wakosoaji wakubwa na wamesahau madudu waliyoyafanya.”

Comments are closed.