The House of Favourite Newspapers

Magonjwa hatari yatokanayo na kujamiiana- 2

0

TULIANZA wiki iliyopita kueleza magonjwa hatari ya kujamiiana, leo tunaendelea kueleza tukijikita zaidi kufafanua yanavyoambukiza, tukianza na kisonono, endelea…

Mara nyingi dalili za magonjwa ya zinaa huwa hazionekani mapema kwa wanawake na hata baadhi ya wanaume.Watu wengi huhisi kuwa, kitendo cha kubusiana kwa ‘kula denda’ni salama, lakini si kama wanavyofikiria kwani baadhi ya magonjwa kama kaswende, herpes na mengine, yanaweza kuambukizwa kupitia njia hii.

Kondomu au mipira ya kiume husaidia kupunguza maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama gono, chlamydia, Ukimwi na kadhalika lakini siyo kinga muafaka ya magonjwa ya zinaa kama vile kaswende, genital herpes na genital warts.
Magonjwa haya ya ngono yapo mengi tuanze kuchambua ugonjwa wa kisonono au gonorrhoea au gono.

Kisonono ni ugonjwa kati ya magonjwa ya zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Neisseria gonorrhoea, bakteria ambao hukua na kuzaliana kwa haraka katika sehemu zenye unyevunyevu na joto mwilini kama kwenye shingo ya kizazi kwa wanawake, mirija ya kupitisha mkojo au mbegu za kiume (urethra), mdomoni na kwenye njia ya haja kubwa (rectum).

KISONONO KWA WANAWAKE
Maambukizi mengi ya kisonono au gono ikiwa ni kifupi cha gonorrhea kwa wanawake hutokea kwenye shingo ya kizazi. Asilimia 75 ya ugonjwa wa gono huwapata watu wenye umri wa kati ya miaka kati 15 hadi 30 kwani ni umri wa mhemko wa kimapenzi.

JINSI UNAVYOAMBUKIZA
Ugonjwa huu huambukizwa kupitia vitendo vya ngono kutoka kwa mtu utakayejamiiananaye, njia ya haja kubwa na kupitia mdomo na unaweza kujitokeza kwenye sehemu za siri, kwenye mdomo na kwenye njia ya haja kubwa.

DALILI
Siyo mara zote kisonono huonesha dalili, lakini kwa kawaida dalili za ugonjwa huo huanza kujitokeza kuanzia siku ya 2 hadi ya 7 baada ya mtu kupata maambukizi ya ugonjwa huo na huweza kuchelewa kuonesha dalili hasa kwa wanawake. Dalili za ugonjwa huo ni kama zifuatazo:-

DALILI KWA WANAWAKE
Dalili za ugonjwa wa gono kwa wanawake huwa si nyingi na wanawake wengi huwa hawaoneshi dalili zozote.

Lakini dalili wanazoonesha wanawake ni kuhisi maumivu au kuhisi kichomi wakati wa kukojoa, kuongezeka kutokwa majimaji ukeni, majimaji ambayo ni ya njano au yaliyochanganyika na damu.

Dalili nyingine ni kutokwa damu kabla ya hedhi kufikia wakati wake wa kawaida, kutokwa na damu baada ya tendo la ndoa, kuhisi kichefuchefu, homa na kutapika.

Itaendelea wiki ijayo

Leave A Reply