The House of Favourite Newspapers

Umetoa/ umedai talaka, mimi nitakuweza?

0

Ni siku nyingine tena kwa upendo wa Mungu tunakutana katika safu yetu ya XXLove kwa ajili ya kuzungumza maisha ya kila siku ya uhusiano.

Katika mada ya leo nitazungumzia baadhi ya wapenzi ambao wanakuwa kwenye uhusiano lakini wakati huohuo wanachepuka na kujisahau kama ni mchumba, mke au mume wa mtu na kujikuta akiomba talaka kwa nguvu ili awe huru, akiamini ni muda muafaka wa kuishi na mchepuko wake kwa kile anachoamini akilini mwake kuwa ni mchepuko sahihi na unampenda, uko tayari kuishi naye?

Mpenzi msomaji wangu, hebu kumbuka mwenza wako alikokutoa. Inawezekana alikukuta kituo cha basi ukiwa unashangaa au alikutoa shamba ukikomaa na kilimo.

Inawezekana mlianza uhusiano wenu tangu mkiwa wanafunzi, pengine alikukuta ukiwa unasumbuliwa na magonjwa sugu ambayo yalikutenga na watu wengine, jamii ilikunyanyapaa lakini yeye kwa upendo wa dhati kwako, akaamua kujitwisha mzigo huo kwa kuamini wewe ni chaguo lake.

Yawezekana ulikutwa ukiwa unalala chini lakini kwa muda mchache milango ya baraka ikafunguka kwa mambo yako kwenda sawa, cha ajabu leo, usivyokuwa na aibu na huruma, umeamua kuchepuka na kufikia hatua ya kuomba au kutaka talaka kwa mwenza wako kwa kuamini huo mchepuko wako ndiye mwenye mapenzi ya dhati na yupo tayari kukuoa au kuolewa nawe.

Kwa michepuko mingi, huwa na swali moja tu kichwani mwao, ila swali lenye mchanganuo mkubwa sana, ‘hivi kama umeweza kudai au kutoa talaka kwa mwenza wako kisa mimi (mchepuko), hivi kweli hata kama nikikuoa au nikiolewa nawe utashindwaje na mimi kunifanyia kama ulivyomfanyia mwanamke au mwanaume mwenzangu? Sina imani, hakika kabisa akitokea mchepuko mwingine, tabia na mambo yale uliyomfanyia mumeo au mkeo yatajirudia!’

Mama au baba tafadhali ume-wrong namba, nina hakika ni baadhi ya maneno ambayo wanawake au wanaume waliozisaliti ndoa au uhusiano wao tena kwa kulazimisha kutoa au kupewa talaka wamekuwa wakiyasikia sana kutoka kwa michepuko yao mara baada ya kunogewa na penzi la mchepuko na kumsahau mwenza wake. Kwa kuamini mchepuko unampenda zaidi kuliko aliyemuweka ndani, kumbe la hasha! Ni sawa na kumuomba maiti damu.

Hali hii imewafanya watu wengi kuishi kama wajane au wagane, kumbe si wajane wala wagane bali mzimu au pepo kwa kulazimisha kutoa au kupewa talaka unamwandama.

Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nzuri na yenye kuelimisha. Usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano  kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta:@mimi_na_uhusiano au kujiunga kwenye group la WhatsApp.

Leave A Reply