The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike – 6

0

maiti-cover

 ILIPOISHIA SEHEMU YA TANO

Mwanaume yule akachukua kibegi changu na kuanza kuelekea ndani ya basi moja, sikumbuki liliitwaje. Nikaingia ndani, akanipa mzigo wangu na kisha kutulia kitini. Sikuwa nikiamini kilichokuwa kikiendelea, eti Zakia mimi, leo hii nilikuwa njiani kuelekea Dar. Safari ikaanza.

Kumbuka kwamba sikuwa na ndugu yeyote ndani ya Jiji la Dar es Salaam, nilikuwa nikienda mimi kama mimi, sikujua ningefikia wapi lakini hamu yangu ilikuwa ni kufika ndani ya jiji hilo tu. Njiani, sikutaka kulala, nilikuwa macho japokuwa nilichoka sana, nilitaka kuona huko mwanzomwanzo wa jiji hilo kulionekanaje.

MWAGIKA NAYO HAPA….

“Hivi Dar kuzuri?” nilijikuta nikimuuliza mwanamke niliyekuwa naye.

“Ndiyo! Kwani hujawahi kufika?”

“Hapana kwa kweli…”
“Una ndugu huko?”
“Hapana!”

“Eeeh! Sasa unakwenda kufanya nini?”

“Nakwenda kutafuta utajiri!” nilimwambia yule mama, kwa mbali akaonekana kushangaa.

“Unakwenda kutafuta utajiri?” aliuliza kwa mshtuko.

“Ndiyo!”

Hakuuficha mshangao wake, aliniangalia kwa macho yaliyoonyesha kuwa na maswali mengi mno, sikujua alijiuliza nini lakini hata kwa kuniangalia usoni, aligundua kwamba nilimaanisha nilichokuwa nikikisema kwamba nilikwenda Dar kutafuta utajiri tu.

Hakutaka kuniuliza swali jingine tena, akanyamaza na kuendelea na mambo yake huku nikipata muda zaidi wa kuangalia dirishani. Baada ya saa moja na nusu, nikahisi kwamba ndiyo nilikuwa nikiingia ndani ya jiji hilo, nyumba nzuri zilianza kuonekana, hisia zangu zikaniambia kwamba tayari tulikuwa tukiingia ndani ya jiji hilo.

“Ndiyo tumefika?” nilimuuliza baada ya ukimya mkubwa.

“Ndiyo! Ila tunaelekea Ubungo, hapa kunaitwa Kibamba…” aliniambia.

Japokuwa sikuwa nikipafahamu huko na wala kufika sikuwahi lakini nilikuwa na hamu kubwa ya kuliona jiji hilo. Kipindi cha nyuma nilipokuwa kijijini, kila mtu alitaka kwenda huko, hawakujali kama walikuwa na ndugu au la, walichokitaka ni kujiona wanaingia ndani ya Jiji la Dar es Salaam na kufanya biashara kwa kuamini watafanikiwa.

Baada ya dakika arobaini, basi likaanza kuingia ndani ya kituo kikubwa cha Ubungo, huko, idadi kubwa ya watu ilinishangaza, haikuwa kama Morogoro, watu walionekana kuwa wengi huku wengi wao wakionekana kuwa bize wakifanya mambo yao.

Niliteremka na mwanamke yule kuondoka, sikuwa na pa kwenda, begi langu mikononi, kwa sababu humo kulikuwa na watu wengi, wa rika zote tena mbele nikiona kuna mikeka, nikasema pia ua, ilikuwa ni lazima na mimi niishi humohumo, hata kwenda huko nje, sikutaka kabisa, kama kula, nitakula humohumo, kama kufanya biashara, acha nifanye humohumo, ila kutoka ndani ya kituo cha Ubungo, nisingeweza, kwani hata kama ningetoka, ningekwenda wapi? Sikuwa na sehemu, hivyo kuishi humo niliona kuwa sulkuhisho. Na humohumo ndipo ningepata huo utajiri.

Nilipokuwa nikiingia ndani ya kituo hicho, moyo wangu uliniambia kwamba inawezekana nilikuwa peke yangu ambaye sikuwa na makazi, niliamini kwamba unapoingia usiku basi watu hao wote wangeondoka na kuelekea nyumbani kwao hivyo kubaki peke yangu kumbe kile nilichokuwa nikikifikiria hakikuwa sahihi kabisa.

Muda ulizidi kwenda mbele, ilipofika saa moja usiku, badala ya watu kupungua ndiyo kwanza walizidi kuongezeka. Nilijiuliza kilichokuwa kikiendelea ni kitu gani lakini nikashindwa kufahamu chochote kile. Mabasi kutoka mikoani yaliendelea kuingia kwa zamu, nilichoka sana, nilihitaji kulala lakini sikujua wapi pa kulala kwani kila sehemu niliyoiangalia pale kituoni ilikuwa na mizigo ya watu hivyo kuwa na wakati mgumu.

“Wewe dada!” nilimsikia mwanaume mmoja akiita nyuma yangu, nilipogeuka, macho yangu yakagongana na macho ya mwanaume huyo.

“Abee..” niliitikia, akanisogelea.

“Wewe ni mgeni mahali hapa?” aliniuliza huku akiwa amenikazia macho.

“Ndiyo!”
“Umetoka wapi?”
“Morogoro!”
“Unaitwa nani?”

“Naitwa Zakia!”

Kwa jinsi nilivyomwangalia mwanaume yule, nilijua tu kwamba alitaka kunizoea na kulikuwa na kitu kingine alichokihitaji kutoka kwangu. Kiukweli nilifanya mambo mengi mabaya, yasiyopendeza mbele ya jamii lakini wakati mwingine nilitakiwa kuyafanya hayo kwa sababu hali niliyokuwa nayo kipindi hicho, ilinilazimu kufanya hivyo.

“Utalala wapi sasa?”

“Sijajua, sina ndugu yeyote yule…” nilimjibu.

Kwanza akaonyesha tabasamu pana, lilinishangaza lakini kitu nilichokumbuka, mwanaume huyu alifanya kama alivyofanya Mudi kwamba kama sina ndugu, basi yeye angejifanya ndugu ila mwisho wa siku alihitaji penzi.

Akaniambia twende sehemu kuzungumza, kwanza niliogopa lakini sikuwa na jinsi, ningefanya nini na wakati nilihitaji msaada mkubwa kutoka kwake? Hivyo nikakubaliana naye. Tukaenda sehemu, ilikuwa pembeni ya duka moja la vinywaji, pale niliona kukiwa na mikeka zaidi ya thelathini ikiwa imekunjwa, sikujua ilikuwa ni ya kazi gani.

“Unajua mpango mzima wa kulala humu?” aliniuliza swali.

“Kulala humu? Kwani kuna watu wanalala humu?” nilimuuliza huku nikionekana kushtuka.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia kesho hapa kujua kitakachoendelea katika sehemu ya SABA.

MWANDISHI: NYEMO CHILONGANI

Global Halotel

Leave A Reply