The House of Favourite Newspapers

Accelerate Africa Tanzania, AIM Wazindua Shindano Kwa Wajasiriamali

0
Mratibu wa Accelerate Africa Tanzania, Pendo Michael Lema (kulia) akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano maalumu kwa ajili ya wajasiriamali watakaochuana ili kupata nafasi ya kuhudhuria mkutano mkubwa kule Abu Dhabi mwezi Mei na kuratibiwa na Accelerate Africa Tanzania kwa kushirikiana na AIM. Kushoto ni Mratibu Msaidizi, Junior Mushi.

Dar es Salaam, 31 Januari 2024:Mtandao wa Accelerate Africa Tanzania kwa kushirikiana na AIM startups wamezindua rasmi shindano ambalo litawawezesha wajasiriamali mbalimbali kupata ufadhili wa kuhudhuria mkutano mkubwa wa AIM yaani AIM Congress 2024 utakaofanyika  Abu Dhabi, UAE mwezi Mei mwaka huu.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa shindano hilo, Mratibu wa Accelerate Africa, Tanzana Pendo Lema alisema usaili tayari unaendelea na wajasiriamali mbalimbali sasa wanaweza kujiandikisha kabla ya tarehe ya mwisho ambayo ni Februari 16, 2024.

“Tayari usaili unaendelea kwa hivyo wajasiriamali wanaotaka kuomba ufadhili huu wanatakiwa kujiandikisha kwa kupitia mtandao wa  https://startupcompetition.aimcongress.com/event/form/ab3e7862-e0e4-41f0-86c6-dc559712b17b ili wapate nafasi ya kufanya mageuzi katika ulimwengu wa teknolojia,” alisema.

Alisema shindano hilo litawapa washiriki nafasi nzuri ya kuonesha ubunifu wao na teknolojia mbalimbali zenye kuleta mageuzi katika sekta hiyo. “Kama ndio umeanza tu au ndio umeanza kushika kasi kidogo katika biashara yako hii ndio hatua itakayokusaidia kukuza biashara yako zaidi,” alisema Pendo.

Akizungumzia baadhi ya faida za sindano hilo, alisema washiriki watakutana na wataalamu mbalimbali na pia wadau mbalimbali wenye maamuzi ya kusaidia wajasiriamali wanaoanza kupiga hatua.

Alisema washiriki watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wajasiriamali mbalimbali, wabia na waelekezaji ambao watawapa ushauri na mawazo mbalimbali ya namna ya kupiga hatua.

Alisema kupitia mkutano huo mkubwa, washiriki pia wanaweza kupata fursa ya kutafuta mitaji kwani kuna wawekezaji wengi ambao wanatafuta sehemu sahihi za kuwekeza.

“Mshindi wa shindano hili atapata faida nyingi ikiwemo kuaminika na hivi kuvutia uwekezaji,” alisema.

Kuhusu vigezo vya kushiriki alisema ni lazima biashara iwe ni changa au iliyoanza muda sio mrefu, iwe na wafanyakazi angalau watano, iwe katika sekta ya teknolojia , iwe na muundo wa kibiashara wa kibunifu na pia iwe na angalau mtaalamu mmoja katika masuala ya teknolojia.

Alisema washindi watafadhiliwa kuhudhuria AIM congress 2024, ambapo watapata malazi na chakula, Visa, banda la maonesho katika mkutano huo, nafasi ya kuhudhuria matukio yote ya AIM na fursa ya kusafiri jangwani.

Kwa kuwa kutakuwa na mshindi mmoja tu kati ya 20 watakaochaguliwa na majaji, mratibu huyo alitoa wito kwa wafadhili mbalimbali wajitokeze ili kuwafadhili washiriki ambao hawatashinda ili nao wapate fursa ya kuhudhuria mkutano huo mkubwa. “Tunatoa wito Kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali hasa yenye uzoefu wa tehama zishirikiane na Accelerate Africa ili tuweze kupeleka wajasiriamali wengi. Ufadhili wao ni muhimu,”alisema.

Accelerate Africa inaundwa na nchi zaidi ya 20 Afrika.

Leave A Reply