The House of Favourite Newspapers

ACHA MILA ZENYE MADHARA; TOKOMEZA UKEKETAJI

Kila mwaka, Februari 6 Tanzania huungana na jamii ya ulimwengu kuadhimisha Siku ya Kupinga Ukeketaji. Historia ya ukeketaji imeendelea kuwepo kwa takribani karne 21 sasa.

Baada ya kutathmini kwa kina athari za ukeketaji kwa wasichana/wanawake na jamii kwa ujumla, mwaka 2003 Baraza la Umoja wa Mataifa lilidhinisha tarehe 6 Februari kuwa siku rasmi ya kupinga ukeketaji duniani.

Ukeketaji ni kitendo kinachohusisha kukata au kuharibu sehemu ya uke wa mwanamke kwa sababu zisizo za kisayansi. Kitendo hiki pia hujulikana zaidi kama tohara kwa mwanamke ambayo hutekelezwa kwa sababu za kiutamaduni.

 

AINA YA UKEKETAJI

Shirika la Afya Duniani limeelezea aina nne za Ukeketaji;

Mosi; kutoa sehemu fulani ya uke wa kike, pili; kutoa sehemu nzima ya eneo hilo, kutoa sehemu za ndani za uke au ukataji wa sehemu yoyote ya uke.

Aina hizi zote ni mbaya kwani zinamletea maumivu makali sana mwanamke anaekeketwa na kwa Tanzania aina ya kwanza na ya pili hutumika zaidi.

 

Jamii zinazoendeleza ukeketaji ni jamii ambazo zimetawaliwa na mfumo dume na mila kandamizi kwa wanawake. Sababu nyingi ambazo hupelekea utekelezaji wa kitendo hiki cha kikatili dhidi ya watoto wa kike na wanawake ni pamoja na:

Sababu za kijamii mfano kumvusha mtoto wa kike rika kutoka kuwa msichana na kuwa mwanamke kamili. Sababu hii husababisha pia ongezeko la ndoa za utotoni na wasichana kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu kwani baada ya kukeketwa huwa tayari kwa kuolewa.

 

Sababu nyingine ni za mila na utamaduni ikiwemo kutambikia masharti ya mizimu, desturi za wazee wa mila, au kuondoa mikosi katika familia, mambo ambayo si ya kweli.

Kuna sababu za kiuchumi; kwamba umasikini umekuwa chachu ya jamii nyingi kubaki katika kitanzi cha mila ya ukeketaji kwani wazazi wa mtoto husika hutegemea kupata kipato kwa kumwozesha binti baada ya kumkeketa. Pia ngariba/mkeketaji hutegemea kipato kutokana na shughuli za ukeketaji.

 

MADHARA YA UKEKETAJI

Ukeketaji husababisha madhara makubwa kiafya kwa mtoto wa kike ikiwemo kupata athari za kisaikolojia kama msongo wa mawazo kwani watoto wengi hufanyiwa vitendo hivyo bila ridhaa yao.

Madhara ya afya ya uzazi ambayo husababisha kuongezeka kwa vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua ni sehemu ya madhara yanayotokana na ukeketaji.

 

Madhara mengine ya ukeketaji ni pamoja na maumivu makali wakati wa ukeketaji, kumwaga damu nyingi na mara nyingine hata kusababisha kifo na maambukizi ya magonjwa hususan Ukimwi. Madhara ya muda mrefu ni kama; msongo wa mawazo, kovu la kudumu sehemu za siri, hali inayosababisha atakapokuja kujifungua, uke kushindwa kutanuka hivyo kupasuka pia kutokufurahia tendo la ndoa na kupata ugumba.

 

Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania inayotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu 2017, inaonesha kwamba pamoja na jitihada za wadau mbalimbali kutokomeza ukeketaji nchini bado mikoa kadhaa imebaki juu kwa takwimu za kitendo hicho cha kikatili kwa mtoto wa kike.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey (TDHS) 2015-16 mikoa inayongoza kwa ukeketaji nchini Tanzania ni Mkoa wa Manyara unaongoza kwa asilimia 58, Dodoma 47%, Arusha 41%, Mara 32% na Singida 31%.

Ripoti hiyo imefafanua pia kuwa vitendo vya ukeketaji hufanywa kwa asilimia 86% na mangariba au wakeketaji wa jadi na kuwa asilimia 25 ya wasichana hukeketwa kabla ya umri wa mwaka mmoja na asilimia 28 ya wasichana hukeketwa katika umri wa miaka 13 na zaidi.

 

Ripoti hiyo imeeleza pia kuwa wasichana wanaozaliwa au kulelewa na mama aliyekeketwa hukeketwa pia na kuwa asilimia 95 ya asilimia 86 ya wanawake waliokeketwa hawakubaliani na kitendo hicho na wanatamani kisiwepo kabisa.

Serikali kwa kushirikiana na wadau imendelea kuboresha sheria na sera kwa lengo la kukabiliana na ukeketaji na kuwajibisha wote wanaoendeleza mila hiyo kandamizi kwa watoto wa kike na wanawake.

Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) 2017/2018-2021/2022) unaelezea ukeketaji kama njia ya kuendeleza tamaduni kandamizi zenye kutweza utu wa mtoto wa kike.

 

Sheria ya Mtoto (2009) imeendelea kusimamia maslahi mapana ya mtoto bila kubagua jinsi.

Sera ya Elimu ya 2015 imekataza kila aina ya unyanyasaji kwa mtoto wa kike na kutambua misingi ya haki na usawa kwa watoto wote wa kike na wa kiume.

Hali kadhalika, Tanzania imeendelea kuridhia na kutekeleza sera na sheria mbalimbali za Kimataifa na Kikanda zinazolenga kutokomeza ukeketaji na ukatili wa kijinsia.

 

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kutokomeza ukeketaji hususan katika mikoa iliyotajwa kuongoza kwa ukeketaji na ukatili wa kijinsia.

Kituo kimeendeleza kutoa elimu kwa jamii yote ili kukuza na kuimarisha uelewa wa kila mtu katika kupinga ukeketaji na vitendo vingine vya ukatili wa kijinsia.

Ushirikiano baina ya Kituo na Serikali, taasisi za kidini, viongozi wa kimila, asasi za kiraia, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla umesababisha kupungua kwa vitendo vya ukeketaji kwa mujibu wa taarifa ya TDHS.

 

Wadau kwa kiwango kikubwa wameendelea kupinga ukatili kwa watoto na wanawake ili kuendana na mikakati ya maendeleo endelevu ya kidunia na mikakati ya kitaifa ya kuondoa aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi watoto na wanawake. Juhudi za makusudi za Serikali bado zinahitajika ili kuhakikisha ukeketaji unatokomezwa kabisa na watekelezaji wa ukeketaji wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria husika.

 

Serikali inapaswa kuanzisha maeneo salama kwa ajili ya wasichana waliopo katika hatari, ya kukumbana na ukeketaji.

Mipango ya sekta ya afya inapaswa kujumisha mikakati ya kuzuia na kutokomeza ukeketaji, kufanya marekebisho ya sheria ili kupiga marufuku ukeketaji wa wanawake walio zaidi ya miaka 18, kuimarisha Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji juu ya Utokomezaji wa Ukeketaji na serikali iendelea kushirikiana na taasisi zisizo za kiserikali na mashirika ya kimataifa kutokomeza ukeketaji.

 

Kwa kuzingatia kauli mbiu ya maandimisho ya mwaka 2019 “Acha Mila zenye Madhara; Tokomeza Ukeketaji”. Tunaisihi jamii hasa zile zinazoendeleza mila ya ukeketaji kuachana na mila hiyo isiyo na faida yoyote kwa wanawake na kwa jamii kwa ujumla.

Tuvisihi vyombo vya dola kuwachukulia hatua kali wanaoendelea kujihusisha na vitendo vya ukeketaji.

Na Elvan Stambuli

Comments are closed.