The House of Favourite Newspapers

ACT- Wazalendo Kuadhimisha Miaka 50 ya Azimio la Arusha

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza na wanahabari. Kushoto ni Katibu wa Wanawake Taifa wa chama hicho, Esther Kyamba.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimepanga kufanya mkutano mkuu kuadhimisha mwaka wa miaka 50 wa Azimio la Arusha Machi 25 mwaka huu jijini Arusha.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Ado Shaibu, alisema Februari 5, 2017 ni siku kama ambayo Azimio la Arusha lilijadiliwa na kupitishwa na Halmashauri Kuu ya chama cha Tanganyika African National Union (TANU) iliyoketi mjini Arusha kati ya Januari 26-29, 1967 na kutangazwa rasmi Februari 5, 1967.
Amesema kuwa mkutano huo utafanyika kupitia Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia (National Democratic Congress) ambao kwa mujibu wa Ibara ya 29 ya katiba ya ACT-Wazalendo ya mwaka 2015, kila mwananchi anaruhusiwa kuhudhuria.

“Mjadala huu utakuwa ni jukwaa la kitaifa kutafakari mafanikio na mapungufu ya Azimio la Arusha na nafasi yake katika Tanzania ya leo. Mkutano huo utajadili nafasi ya siasa za kijamaa na za mrengo wa kushoto barani Afrika na duniani katika zama hizi za kukua kwa kasi kwa siasa za mrengo wa kulia:
“Pia, katika kuadhimisha miaka 25 ya kutekelezwa kwa Azimio la Arusha (1967-1992) na miaka 25 ya kutelekezwa kwake (1992-2017) Chama Cha ACT-Wazalendo kitautumia kutafakari dhana na misingi ya Azimio la Tabora linalohuisha Azimio la Arusha katika mazingira ya karne ya 21 ,” alisema.

Aidha alisema kuwa mkutano huo unatarajiwa kuwakutanisha wanasiasa wa vyama mbalimbali, wawakilishi wa asasi za kiraia, wanazuoni na wanaharakati kutoka ndani ya nje ya nchi.

“Hadi sasa chama chetu kimeshatoa mialiko na kufanya mazungumzo na vyama vya Labour (cha Uingereza), Economic Freedom Fighters-EFF (Afrika ya Kusini), Die Linke (Ujerumani) na Syriza (Ugiriki) ili viongozi wao washiriki na kutoa mada kwenye mkutano huo,” aliongeza.

…Akionyesha kitabu cha Azimio la Arusha kwa wanahabari (hawapo pichani).

Vilevile alisisitiza kuwa chama chao kitawaalika waliokuwa wanachama wa taasisi ya Ruvuma Development Association (RDA) na wananchi wengine walioishi kipindi cha Azimio la Arusha wakati huo ili waweze kutoa uzoefu wao na kwa watakaohitaji kushiriki katika mkutano huo amewaomba watume majina yao kupitia barua pepe ya actwazalendo [email protected] au namba za simu 0719847032 na 0717047574.

 

NA DENIS MTIMA/GPL

Comments are closed.