The House of Favourite Newspapers

AIBU KUBWA! MUME WA MTU ATAITIWA SKENDO KUPIGA CHABO

MOROGORO: Hii ni aibu ya mwaka! Ndiyo iliyompata mume wa mtu, Fikiri Juma ambaye ni baba wa familia, kufuatia kutaitiwa ile mbaya na kuburuzwa Serikali ya mtaa kwa skendo ya kupiga chabo (kuchungulia) wake za watu.

Tukio hilo lililoshuhudiwa na Ijumaa Wikienda na kujaza umati mkubwa huku wengi wao wakiwa ni akina mama, lilijiri wikiendi iliyopita majira ya asubuhi katika Mtaa wa River- Side Kata ya Mwembesongo mjini hapa na kusababisha mtaa kufungwa.

 

Katika hali ya kushangaza, baba huyo alidaiwa pia kumpiga chabo kiongozi wake ambaye ni mjumbe wa Serikali ya mtaa huo, Fatuma Abdallah ambaye ni miongoni mwa waathirika wa tukio hilo waliopeleka malalamiko yao kwa mwenyekiti wa mtaa huo, Hashim Bito.

“Kama unavyojua, vyoo vyetu vingi hapa mtaani vipo nje ya nyumba zetu na vipo wazi kwa juu hivyo huyu baba akisikia mtu anaoga anapanda juu na kumchungulia. “Hata mimi kiongozi wake aliwahi kunichungulia ila kwa umri wangu ulivyoenda nilijisikia aibu kupeleka malalamiko yangu kwa mwenyekiti.

 

“Sasa leo baada ya Fikiri kukamatwa nimejumuika hapa kwa mwenyekiti kutoa ushahidi,” alisema mjumbe huyo. Naye Juma Hamis ambaye ndiye aliyemnasa Fikiri akimpiga chabo mkewe alisema: “Mke wangu alikuwa akioga, nilikwenda dukani kununua vitafunwa vya chai, ile narudi ndipo nikamkuta Fikiri amepanga matofali chooni kwa nyuma anamchungulia mke wangu.

“Nimemkamata na kumleta hapa kwa mwenyekiti ambapo watu wengi wamejitokeza wakidai kwamba ndiyo mchezo wake wa kula chabo. “Huwa anabahatisha, siku moja alichungulia chooni akakuta mwanaume anaoga akashuka ghafla. Jamaa aliyekuwa anaoga alijua ni mwizi, akavaa nguo harakaharaka, alipotoka alimshuhudia Fikiri akitokomea kusikojulikana,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Bito alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. “Ni kweli Fikiri ambaye ni mkazi wangu hapa mtaani mwenye mke na watoto ameletwa hapa ofisini kwangu na umati wakimtuhumu kuwachungulia wakati wakioga na waliokuja kuripoti wapo hapa zaidi ya watatu.

“Nilipomuuliza Fikiri alikana kufanya tukio hilo hivyo kwa kuwa walalamikaji hawakuwa na ushahidi wowote, niliamua kuweka ushahidi wa maandishi na kumsainisha. “Baada ya hapo tutaweka mtego, tukimkamata tena tunampeleka Polisi kwani hii ni hatari sana, kundi kubwa walitaka kumshambulia kwa kichapo,” alisema mwenyekiti huyo.

 

Baada ya kusainishwa, Fikiri aliachiwa huru na alipotoka kwenye ofisi hiyo ya mwenyekiti kundi hilo la watu walimsindikiza nyumbani kwake huku wakimzomea, lakini naye kwa hasira aliamua kuwapopoa kwa mawe. Ijumaa Wikienda lilipotaka kuzungumza na mke wa Fikiri aligoma kuzungumza na kutimkia chumbani.

STORI: DUNSTAN SHEKIDELE, Wikienda

Comments are closed.