The House of Favourite Newspapers

Aina Za Magonjwa Ya Moyo

BAADA ya wiki iliyopita kueleza matatizo ya tundu kwenye moyo, leo tutaeleza aina mbalimbali ya magonjwa ya moyo, kitaalamu huitwa Cardiovascular Diseases, yaani magonjwa yote yanayoathiri moyo na mishipa yake.

 

Msomaji anapaswa kujua kuwa magonjwa ya moyo yanajumuisha ugonjwa wa kupanda kwa shinikizo la damu ambalo kitaalamu huitwa High Blood Pressure au Hypertension.

 

Hili ni tatizo sugu la kiafya linalohusisha kuongezeka kwa mgandamizo wa msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu.

Sasa tuangazie magonjwa haya ya moyo kifupi kama ifuatavyo:

UGONJWA WA KORONARI ZA MOYO

Magonjwa ya koronari za moyo kitaalamu huitwa Coronary Heart Diseases. Huu ni ugonjwa wa moyo ambapo mafuta yanaganda ndani ya ateri koronari na kuziba kwa kiasi fulani au kuziba kabisa kwa ateri ya

koronari za moyo, hivyo kusababisha upungufu wa damu katika sehemu ya moyo ambayo hupata damu kupitia mishipa hiyo.

 

Ugonjwa huu ni hatari kwani hudhoofisha misuli ya moyo kiasi cha kusababisha moyo kushindwa kusukuma kiwango cha kutosha cha damu na husababisha Arithmia (Arrhythmias), kwa maana ya ugonjwa unaosababisha mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio wa kawaida.

 

UGONJWA WA MOYO WA ATHEROSKLEROSISI

Ugonjwa huu wa moyo kitabibu huitwa Atherosclerosis) unasababishwa na kitendo cha mafutamafuta kuganda kwenye mishipa ya ateri.

 

Kuganda kwa mafutamafuta huko, kunaweza kuchukua miaka mingi. Kadri miaka inavyosonga mbele, ndivyo mafutamafuta haya yanazidi kuwa magumu na kuzuia msukumo wa damu yenye oksijeni kwenye mirija ya kwenye moyo.

Ikiwa mafutamafuta yataziba kabisa kwenye ateri koronari na kusababisha misuli ya moyo kukosa damu yenye oksijeni, huweza kumsababishia mtu maradhi mengine yanayoitwa Anjina, kwa maana ya maumivu makali ya kifua na Mshtuko wa Moyo (Myocardia Infarction watalaamu wengine huita Heart Attack).

UGONJWA WA MOYO WA ANYURISMU

Anyurismu au kitaalamu Aneurysm ni aina nyingine ya magonjwa ya moyo. Hiki ni kitendo cha mishipa ya ateri kuvimba kama puto kutokana na kuharibika kwa mishipa au kudhoofika kwa kuta za mishipa.

Ikitokea mishipa hii ya ateri ikapasuka, husababisha damu kuvuja kwenye ubongo, hivyo kumsababishia mtu kukumbwa na kiharusi (Stroke).

Kiharusi hufanya mgonjwa kupooza kwani unatokana na kuingiliwa au kupungua kwa usambazaji wa damu kwenye ubongo hali inayosababisha seli za ubongo kukosa oksijeni na virutubishi muhimu.

UGONJWA WA MOYO WA RHUMATIKI

Ugonjwa huu wa Rhumatiki ya Moyo, kitabibu Rheumatic Heart Disease unasababisha kupungua utendaji kazi wa moyo kutokana na moyo kuwa na vivimbe tangu mtoto anapozaliwa (Congenital Heart Diseases), na mara nyingi huweza kusababisha vifo kwa mgonjwa wakati wa utotoni.

UGONJWA WA MOYO WA PVD

PVD kirefu chake ni Peripheral Vascular Disease ni ugonjwa mwingine wa moyo kwenye mishipa ya damu. Ugonjwa huu hutokea kwenye mfumo wa usambazaji wa damu nje ya ubongo na moyo.

Mara nyingi, ugonjwa huu huwapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, hasa wavutaji wa sigara na wenye ugonjwa wa kisukari.

Wiki ijayo tutaeleza ni nini chanzo cha magonjwa ya moyo?

Na MWANDISHI MAALUM Simu: 0754 391743

Comments are closed.