The House of Favourite Newspapers

Ajali ya Ndege Indonesia, Black Box, Miili ya Abiria Vyaonekana

0

NDEGE ya Shirika la Ndege la Sriwijaya iliyokuwa imewabeba watu 62 imepoteza mawasiliano dakika chache baada ya kuruka kutoka mji mkuu wa Indonesia wa Jakarta.

 

Waziri wa Usafirishaji wa Indonesia, Budi Karya Sumadi, leo Jumapili Januari 10, 2021 amesema ndege hiyo ilichelewa kuanza safari yake kwa muda wa saa moja kabla ya kuruka.

Ndege ya aina ya Boieng chapa 737-500 ilipotea kwenye mawasiliano ya rada dakika nne baada ya kuruka na Shirika la Ndege Sriwijaya limesema kwenye taarifa yake kwamba safari ya ndege ilitarajiwa kutumia dakika 90 kutoka Jakarta hadi Pontianak, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kalimantan magharibi kwenye kisiwa cha Borneo.

Kulingana na Mkurugenzi wake Jefferson Irwin Jauwena, ndege hiyo ilikuwa kwenye hali nzuri kabla ya kuruka.

 

Imeelezwa kuwa kulikuwa na jumla ya abiria 56 na wafanyakazi sita. Waziri Sumadi amesema meli kadhaa ikiwemo meli nne za kivita tayari zimesambazwa baharini katika jitihada za kuisaka na operesheni ya uokozi tayari imeanza. Ripoti za vyombo vya habari zinasema wavuvi wameviona vipande kadhaa vya chuma vinavyoaminika kuwa sehemu ya ndege hiyo mchana wa Jumamosi kwenye maeneo ya visiwa.

Mamlaka za nchi hiyo zimeeleza leo kuwa vifaa viwili vya kurekodi sauti na mwenendo wa ndege (Black Boxes) vimeonekana katika eneo ilipodondoka ndege hiyo.

 

“Tumeona vifaa hivi ,” alisema Soerjanto Tjahjanto, Mkuu wa kitengo cha usalama wa safari nchini Indonesia

Msemaji wa Polisi, Yusri Yunus amesema leo  kuwa wamepokea mifuko miwili mmoja ukiwa na sehemu za mwili na mwingine ukiwa na mali zinazoaminika kuwa ni za abiria.

Mamlaka imeweka vituo viwili vya kushughulikia yanayohusiana na ajali hiyo, kimoja kwenye uwanja wa ndege na kingine kipo bandarini. Familia zimekusanyika katika vituo hivyo kusubiri taarifa za wapendwa wao.

 

Ndege hiyo nambari SJ-182 ni mali ya Shirika la Ndege la Sriwijaya Air.

Leave A Reply