The House of Favourite Newspapers

Akon Kuwainua Wasanii Wachanga Afrika

0

Jukwaa la kusikiliza na kupakua muziki online la Boomplay kwa kushirikiana na Hitlab wametangaza shindano la kuvumbua vipaji kidijitali kwa wasanii chipukizi linalomshirikisha nyota wa muziki wa Marekani mwenye asili ya Senegal, Akon.

 

Mashindano hayo ya kwanza na ya aina yake barani Afrika yanatoa fursa ya kurekodi na kufanya kazi na lebo za muziki kimataifa, kutumbuiza kwenye majukwaa ya kimataifa, kuwa chini ya uangalizi wa msanii Akon pamoja na zawadi nyingine mbalimbali.

 

Meneja Mkuu wa Boomplay nchini Tanzania, Natasha Stambuli amesema shindano hilo la kuvumbua vipaji kidijitali kwa wasanii chipukizi, ni la kwanza la kimataifa na fursa ya kipekee kwa wasanii wachanga wenye ndoto za kutoboa kimataifa.

 

“Hii ni hatua muhimu kwetu katika kufanikisha azma yetu ya kukuza wigo wa muziki wa Kiafrika na tunafurahi sana kuhusu fursa ambazo ushirikiano huu wa kimkakati utakavyowasaidia wasanii wetu wanaochipukia wa Kitanzania.”

 

Kuhusu namna ya kushiriki, Stambuli amesema wasanii wanaweza kuwasilisha nyimbo zao kwa ajili ya uchambuzi kupitia mfumo wa teknolojia mbadala wa Hitlab, Digital Nuance Analysis (DNA) Technology, ambayo inapanga kwa viwango nyimbo zilizowasilishwa na kuonesha uwezo katika soko la kimataifa huku miongoni mwa vitu vinavyozingatiwa kuwa ni pamoja na mdundo (beat) na ukamilishaji wa nyimbo (mastering).

 

“Ili kuwasilisha nyimbo, kwa msanii ambaye yupo tayari anapaswa kuchangia shilingi za Kitanzania 2,296 ($0.99) kwa wimbo mmoja, shilingi 9,254 ($3.99) kwa nyimbo tano 5 na shilingi 23,169($ 9.99) kwa nyimbo 15. Unachopaswa kufanya ni kuwasilisha nyimbo zako kupitia ‘link’ ifuatayo https://deas.hitlab.com/?ref=BOOMPLAY.

 

“Mara baada ya kuwasilisha nyimbo, itatokea chati inayopanga ubora wa nyimbo na msanii kupewa alama muda huohuo. Nyimbo ni lazima ziwe na ubora na vigezo vya kupita zaidi ya alama 49 kwenye mfumo wa kidijitali wa DEAS,” amesema Stambuli na kuongeza kuwa shindano hilo litaendeshwa hadi Oktoba 20, 2021 na baada ya hapo, washindi watatangazwa.

Leave A Reply