The House of Favourite Newspapers

Al-Shabaab Ni Nani? -13

0

AlShabaabfighters014.jpgMarekani yatangaza kuua kiongozi wa Al-Shabaab

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Wiki iliyopita nilieleza juu ya kundi haramu la kigaidi la Al-Shabaab lilivyotuma vitisho vya kutaka kuvamia Majiji ya Dar na Mwanza nchini Tanzania kupitia mkanda wa video ulioonesha mwakilishi wa Kundi la Kigaidi la Dola ya Kiislam la Iraq na Lavent (ISIL), akimtaka Kiongozi wa Al-Shabaab kujiimarisha na kufanya mashambulizi kwenye majiji hayo.

SASA ENDELEA…

Katika kipindi hicho, polisi wa Tanzania waliimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya mikusanyiko mikubwa licha ya kuwa magaidi hao hawakuwa wakitabirika.

Wakati Tanzania wakijiweka sawa, polisi nchini Uganda waliripotiwa kufanya oparesheni kubwa ya kutibua jaribio la shambulizi la kigaidi la Wanamgambo wa Al-Shabaab.

Oparesheni hiyo ilifanikiwa kukamata watu kumi na tisa ambao waliohojiwa na polisi kuhusiana na nia yao kutekeleza vitendo vya kigaidi nchini humo.

Baadaye Ubalozi wa Marekani jijini Kampala nchini humo ulionya kuwa kulikuwa na uwezekano wa shambulizi la kulipiza kisasi cha mauaji ya kiongozi wa kundi hilo la Al-Shabaab.

Al-Shabaab walidai kujipanga kutekeleza mashambulizi nchini Uganda kwa kuwa walikuwa wakiilaumu nchi hiyo kwa kutoa majeshi yake kwenda Somalia kupigana chini ya Nembo ya Umoja wa Afrika (Amisom).

Kufuatia tishio hilo, Marekani ilitangaza kuuawa kwa Kiongozi wa Kundi la Al-Shabaab, Ahmed Abdi Godane baada ya shambulizi la angani huko Somalia.

Serikali ya Uganda ilidai ililishtukia kundi hilo la kigaidi kuwa lilikuwa na mpango wa kufanya mashambulizi kwenye mji mkuu wake wa Kampala.

Askari walikaririwa wakisema kuwa kundi hilo lilikuwa limepanga mashambulizi katika miji mingine kadhaa.

Siku kadhaa baadaye, Marekani na majeshi yake ilidai kuwa iliamini kwamba tishio la shambulizi la Al-Shabaab lilikuwa limeondoka.

Waziri wa Habari wa Uganda, Rose Namayanja alikaririwa akiwasihi wananchi kuendelea kuwa waangalifu huku serikali ikifanya uchunguzi wa mashambulizi yaliyokuwa yamepangwa na kundi hilo.

Alisema kuwa watuhumiwa hao kumi na tisa walipatikana na vifaa vilivyohusiana na vitendo vya kigaidi na nia yao ilikuwa wazi sana.

Baada ya kugonga mwamba nchini Uganda, Al-Shabaab walirejesha mashambulizi nchini Kenya ambapo walidaiwa kuua tena watu sita katika Chuo Kikuu cha Garissa ambako shambulio la awali waliua watu 147.

Ilielezwa kwamba, watu watano waliojifunika vitambaa usoni walishambulia kwa mara nyingine chuo hicho kilichopo Kaskazini-Mashariki mwa Kenya.

Wanamgambo hao walidaiwa kuingia kwenye chuo hicho wakati Waislam wakifanya sala yao ya alfajiri.

Maafisa wa polisi walikaririwa wakisema kuwa shambulio hilo lilifanyika kwa muda wa saa kumi.

Taarifa zaidi zilidai kwamba, walinzi wawili waliuawa katika lango la chuo hicho huku maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda chuo hicho pamoja na wanafunzi wakijeruhiwa.

Walioshuhudia tukio hilo walieleza kwamba, kulikuwa na majeruhi wengi ndani ya chuo hicho.

Jeshi la Kenya (KDF), maafisa wa polisi na ambulance walifika eneo la tukio kisha walizama ndani ya majengo ya chuo hicho ambapo walianza kurushiana risasi na washambuliaji hao wa Al-Shabaab.

Hata hivyo, wanafunzi 27 walifanikiwa kutoroka na kukimbilia katika kituo kimoja cha kijeshi kilichopo jirani na eneo hilo.

Tofauti na matukio mengine, Al-Shabaab hawakujitokeza kukiri kutekeleza shambulizi hilo japokuwa Al-Shabaab walishukiwa vikali.

Chuo hicho ndicho taasisi ya kipekee ya masomo ya juu katika eneo hilo kilichofunguliwa mwaka 2011 na kiko takriban kilomita 350 kutoka Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi.

Je, nini kiliendelea? Usikose wiki ijayo.

Leave A Reply