The House of Favourite Newspapers

Aliens wajivinjari anga la Mexico

0

aliensETILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Mpenzi msomaji wiki iliyopita niliuliza swali kuwa unadhani humu duniani tunaishi wenyewe? Nilikuacha utafakari ndipo nikaelezea tukio la Aliens kuonekana katika anga la Jimbo la Arizona nchini Marekani na kuwa tishio jipya kwa wakazi wa eneo hilo na majirani zake.

SASA ENDELEA…

Uchambuzi wa kompyuta kupitia video zilizorekodiwa ulikadiria kuwa chombo walichokuwa nacho Aliens chenye mfano wa sinia kubwa kilikuwa angani katika umbali wa sawa na futi 6,000 ikielezwa kuwa chombo hicho hakikutoa kelele yoyote, kilikuwa kimya kama hakipo.

Ilielezwa kwamba, chombo hicho, baada ya kuganda kwa muda mrefu angani na kabla ya kutoweka ghafla, kilianza kusogea taratibu juu ya eneo la Phoenix. Kilikadiriwa kuwa na mwendo wa kilometa 30 kwa saa. Mara kadhaa kilikuwa kikikata kwenye anga kimyakimya bila muungurumo.

Maeneo mengine ambayo UFO zilishashuhudiwa na kuibua hofu ni pamoja na Venezuela (Oktoba 24, 1886), Uturuki (Mei 2008 – Septemba 2009), Ureno (Agosti 13, 1917, Septemba 13, 1917 na Oktoba 13, 1917).

Maeneo mengine ni Marekani, Aurora, Texas (Aprili 19, 1897), Urusi (Juni 30, 1908), Marekani, Stephenville, Texas, Dublin, Texas, Crawford, Texas (Januari 01, 2008 – Februari 09, 2008), Mexico (Agosti 6, 1997), Brazil (Januari 20, 1996), Australia (Agosti 8, 1993), Uingereza (Aprili 21, 1991), Canada (Novemba 7, 1990), Ubeligiji (Machi 30, 1990) na New Zealand (Desemba 21, 1978).

Kwa takriban miaka hamsini sasa tangu serikali mbalimbali duniani na watafiti walipoamua kulishughulikia suala la UFO na kutafuta majibu ya maswali kuhusiana na asili yake ni nini na tija au madhara yake kwa binadamu ni yapi, hakuna kati ya hao aliyekuja na majibu ya kuridhisha au majibu rasmi kuhusiana na suala hilo.

Kama UFO zitakuwa ni kweli zipo na asili yake hasa ni kutoka nje ya sayari yetu, ukweli huo utakuwa ni changamoto ya namna yake kwa binadamu wote.

Juu ya ukweli kama UFO na Aliens vipo au havipo, asilimia 72 ya Wamarekani wanaamini kuwepo kwa uhai nje ya sayari yetu.

Wanaamini kuna viumbe wengine wanaishi huko. Asilimia 48 wanaamini juu ya kuwepo kwa UFO na asilimia 15 wameona UFO huku asilimia 2 hadi 3 wakiamini kuwa wamewahi kutekwa na viumbe hao na kuingizwa kwenye UFO na baadaye kurejeshwa walipokuwa (duniani).

Pia kumekuwepo na habari nyingi mno kutoka kwenye magazeti na majarida katika nchi za Magharibi. Inaelezwa kwamba watu waliona UFO, waliowaona viumbe hao, mpaka wale waliokamatwa na kupakiwa kwenye UFO. Wakati mwingine inakuwa ni vigumu kuzithibitisha taarifa hizo, wakati mwingine taarifa zinakuzwa kuwa kubwa kushinda tukio lenyewe, wakati mwingine kwa makusudi zinakuwa ni taarifa za kutengeneza au zenye upotoshaji.

Lakini bado kuna wakati tukio moja linakuwa na mashahidi zaidi ya mmoja, linakuwa limeacha ushahidi wenye kuonekana, ushahidi unaoweza kuugusa kwa mkono, ushahidi ambao ni zaidi ya maneno ya shuhuda.

UFO, kwa wanahistoria zimerekodiwa kwenye vitabu vya kihistoria tangu enzi na enzi ya historia ya mwanadamu. Ingawa haipo kwenye mitaala ya somo la historia hivyo ni kama hakuna kitu kama hicho.

Kuanzia mwaka 1991 hadi 1993, Nchi ya Mexico ilifunikwa na taarifa za kuonekana kwa UFO. Julai 11, 1991, watu 17 ambao hawana uhusiano wowote katika maeneo tofauti nchini humo wakiwa na kamera zao, walinasa picha ya sinia kubwa la chuma karibu kabisa na usawa wa jua ambalo muda mfupi nyuma lilikuwa limepatwa na mwezi. Sinia hilo lilikuwa limening’inia angani kwa muda bila kusogea upande wowote ule.

Walionasa tukio hilo hawakujua kama wamepiga picha UFO mpaka watu wengine walipong’amua wakati wanaoneshwa video hizo.

JE, kiliendelea nini? Usikose kufuatilia wiki ijayo hapahapa.

Leave A Reply