The House of Favourite Newspapers

Aliyejijengea Kaburi la Bilioni 1 Afariki

0

MGANGA wa jadi, Dk. Anthony Mwandulami, mkazi wa Kijiji cha Wangama, Kata ya Mtwango wilayani Njombe mkoani Njombe, aliyekuwa anajijengea kaburi kwa gharama aliyodai kufikia Sh. bilioni 1, amefariki dunia.

 

Dk. Mwandulami, aliyejizolea umaarufu mkubwa kutokana na uamuzi wake huo wa kujijengea kaburi, alifariki dunia usiku wa kuamkia Julai 3, jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.

 

Mwaka 2019, mganga wa jadi huyo alisema ameamua kujenga kaburi hilo likitarajiwa kugharimu Sh. bilioni moja kwa manufaa yake kwa kuwa amefanya shughuli nyingi.

“Nimefanya shughuli nyingi na ni mhangaikaji sana, nina familia kubwa. Kwa hiyo, nimeona ni vizuri zaidi kutengeneza maziko ambayo nitazikwa na wake zangu.

 

“Nimejaribu kuchunguza maziko waliyofanyia baba zangu mpaka leo (2019) hayajulikani yapo wapi. Sasa hili ni tatizo. Vizazi vya mbele vinakuwa havijui ndugu walizikwa wapi?

 

“Mfano viongozi wetu wanafanya kazi nzito, hivyo kutengenezewa mazingira ambayo yapo vizuri ni muhimu kwa kumbukumbu ya watu wanaokuja hata miaka 100 mbele,” alifafanua.

 

Katika mahojiano hayo, alitolea mfano shughuli alizokuwa anazifanya Hayati Rais John Magufuli ambazo aliziita kuwa ni historia ambayo haiwezi kupotea.

 

“Nimeona nijifanyie hivi. Nilikaa na wake zangu watatu, tukakubaliana na walinishauri ‘mume wetu tunaona ufanye unaloona linafaa’. Kwa hiyo, ndiyo ninashughulikia sasa (ujenzi wa kaburi),” alisema.

KABURI LILIVYO

Kaburi hilo ambalo limejengwa pembeni ya nyumba yake ya kuishi, kimwonekano ni la ghorofa moja, juu kukiwa na msalaba mkubwa.

 

Mwenyewe alibainisha kuwa wakati wa uhai wake kuwa chumba cha juu (ghorofa) ni kwa ajili ya kuhifadhi picha za kumbukumbu zao na makaburi yapo chini.

 

Katika mahojiano hayo, Dk. Mwandulami alisema amekuwa akipokea wageni kutoka Denmark, Australia, Sweden, Oman, Uingereza na Afrika Kusini, hivyo anaamini kaburi hilo litakuwa ni kumbukumbu kwao kwa kazi ya ubunifu na utafiti wa miti shamba ya kutibu maradhi mbalimbali.

 

Dk. Mwandulami alisema ikishafika mwisho na akiona balaa kwamba dawa zimeshindwa, ipo namna anayojua ataongea maneno tu.

 

“Ninaandika ujumbe hapo kwamba muda wangu tayari umefika, wanangu mniandalie sasa kama nilivyowaahidi kwamba mnitengeneze namna gani ndiyo ninaondoka,” alisema.

 

MAJIRANI WAMLILIA

Jana, Nipashe ilizuru katika Kijiji cha Wangama na kuzungumza na wakazi wake ambao walisema watamkumbuka Dk. Mwandulami juhudi zake za kuchangia maendeleo. Walisema Dk. Mwandulami amewaachia pengo kubwa kwa kuwa alikuwa mtu wanayemtegemea.

 

“Kwenye michango mbalimbali ya kimaendeleo kama ujenzi wa shule, zahanati, alikuwa akijitoa sana. Hili ni pengo katika kijiji chetu,” alisema Felsta Luvanda.

 

Victor Nyagawa, mkazi wa kijiji hicho, alisema kitu cha kipekee alichokishuhudia kwa Dk. Mwandulami ni wakazi wa eneo hilo kuwapatia matibabu bila malipo pale walipougua.

 

‘’Sisi wakazi wa eneo hili ikitokea umeugua, alikuwa anatutibu bure kwenye kituo chake na kama kwake imeshindikana, utapewa fedha kwenda hospitalini.

 

“Kama mimi mama yangu aliumwa macho, akatakiwa kwenda kusafishwa, Dk. Mwandulami alitoa laki tatu (Sh. 300,000) ya kwenda kusafishwa,” alisema Nyagawa.

 

“Tutamkumbuka, hili ni pengo kubwa sana, alikuwa ni zaidi ya daktari kwetu, mkarimu, ana huruma, tutamkumbuka sana kwa mema yake,” alisifu.

 

Sophia Mwinami, aliyekutwa na Nipashe kwenye kituo hicho jana, alisema alifika kwenye kituo hicho kutibiwa na alikuwa anaendelea vizuri hadi umauti unamfika mganga wake.

 

‘’Nilikuja hapa kupata tiba, hali yangu inaendelea vizuri lakini sina tena matumaini kwa kuwa tabibu wangu amefariki dunia.

 

“Kufa ni ibada lakini unaweza kukufuru maana bado sijapona vizuri halafu hili linatokea,” Mwinami alizungumza katika hali ya majonzi.

 

Leave A Reply