ALIYEKATWA MIKONO ASHTUA WENGI!

MARIAMU Staford ni mwanamke mwenye ualibino aliyefanyiwa unyama wa kutisha wa kukatwa mikono yake yote mwaka 2008 akiwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Ntobeye Wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwa imani za kishirikina, lakini amekuwa akishtua wengi kwa mambo anayoyafanya. 

 

Baada ya tukio hilo baya la kulaaniwa duniani kote, mwaka 2009, Mariamu alihamishiwa ‘mafichoni’ mkoani Kilimanjaro na shirika la kutetea watu wenye ualibino la Under the Same Sun (UTTS) kwa ajili ya usalama wake.

Pamoja na hayo yote, Mariamu amekuwa akiuthibitishia ulimwengu kwamba watu wenye ualibino wanaweza kufanya makubwa.

 

MIAKA 10 SASA

Akizungumzia hali ya Mariamu katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika wiki iliyopita mjini Morogoro, Mwanasheria wa Under the Same Sun, Seif Kondo alisema Mariamu anaendelea kufanya mambo makubwa isipokuwa hajaweza kurudi kijijini kwake akihofia usalama wake.

 

“Mpaka leo, miaka kumi imepita Mariamu yupo mafichoni kwa sababu akirudi pale kijijini (Ntobeye Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Tanzania), kuna yule mtu aliyedai alimuona akimfanyia kile kitendo na yeye alimpeleka mahakamani hivyo hawezi kurudi pale,” alisema Kondo almaarufu Babu Kondo.

 

“Mariamu atakapomuona huyo mtu atasema huyu alinikata mikono yangu, sina mikono kwa sababu yake, yule aliyetuhumiwa naye akimuona Mariamu atasema wewe ulinipeleka mahakamani, unadhani hapo patakalika?” Alihoji Babu Kondo akionesha bado hali si shwari dhidi ya watu wenye ualibino.

 

MKASA WA MARIAMU

Mwaka 2008, Mariam akiwa na umri wa miaka 28, alikuwa amelala na mwanaye wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka miwili aitwaye Nio. Katika mkasa wake huo wa kusikitisha, Mariamu alivamiwa na wanaume wawili ambao walimkata mikono yake yote akiamini walikwenda kuuza viungo vyake kwani kilikuwa ni kipindi ambacho viungo vya watu wenye ualibino viliaminika kusaidia watu kupata utajiri.

 

Katika tukio hilo mwanawe huyo aliyekuwa amelala naye hakuguswa, lakini yeye alipoteza mikono yake kisha kukaa hospitalini kwa wiki kadhaa. Kwa mujibu wa Mariamu, aliwatambua waliomkata mikono yake akiwemo jirani yake aliyeishi naye kwa muda mrefu.

Hata hivyo, watuhumiwa wote walikamatwa na kufikishwa mahakamani, lakini hawakutiwa hatiani baada ya kukutwa hawana hatia! Kwa mujibu wa Mariamu, katika hali ya kushangaza na iliyojaa uchungu, kijiji kilimgeuka na kumtuhumu kwa kile walichokiita; “kukisababishia kijiji aibu” kwa kitendo chake cha kwenda mahakamani kusaka haki yake.

 

Baada ya habari zake kuripotiwa juu ya unyama aliofanyiwa Mariamu, mashirika mbalimbali yalijotolea kumsaidia likiwemo Shirika la Under the Same Sun ambapo Kampeni ya Asante Mariamu ilianzishwa.

 

Baadaye Mariamu aliwekewa mikono ya bandia ya chuma na hapo ndipo aliposhangaza dunia baada ya kwenda chuo cha ufundi mkoani Kilimanjaro na kuhitimu cheti cha masomo ya ushonaji. Ili kuwa salama aliendelea kuishi Kilimanjaro ndanindani akishona masweta ambayo amekuwa akiyauza akiwa na maono ya kuyasambaza kwenye maduka makubwa ya nguo nchini na mitandaoni.

 

Mariamu ana mpango wa kuendelea kusoma hadi afikie ngazi ya digrii bila kujali kitendo cha ukatili alichofanyiwa akiamini kuwa hakiwezi kumkatisha tamaa. Mbali na kielimu, Mariamu ana maono ya kujijenga kiuchumi ili kuwa na uwezo wa kujitegemea na kumkuza mwanaye, Nio katika mazingira salama.

 

Malengo yake mengine ni kujenga ya familia yake katika ardhi ambayo alisaidiwa kuipata na marafiki zake na wadau mbalimbali ambapo pia atafungua duka lake la nguo anazofuma kwa mikono aliyowekewa.

 

Ndoto yake ya muda mrefu ni kuzindua taasisi yake ya Asante Mariamu katika mikoa mbalimbali nchini kwa ajili ya kutoa elimu na ushauri kwa watu wenye ulemavu. Mwaka jana Mariamu alishangaza wengi baada ya kuongoza wenzake kupanda Mlima Kilimanjaro na kuifanya dunia kutambua kuwa wenye ualibino wanaweza.

WAZIRI MKUU Ashtukia Mchezo wa Maafisa Tarafa” Rudisheni Siku ya Usafi”


Loading...

Toa comment