ALIYEKUWA MUME WA DAVINA AVUNJIWA MJENGO

ALIYEKUWA mume wa staa wa filamu za Kibongo, Halima Yahya ‘Davina’, Abdallah Shakoor ambaye pia ni mzazi mwenzake na staa huyo juzikati yalimkuta mazito baada ya kuvunjiwa mjengo wake wenye thamani ya shilingi milioni 250.

 

Nyumba hiyo pamoja na nyingine ikiwemo ya shemeji yake Yahaya Dossa zilizopo Kigamboni eneo la Chadibwa Dar, zilibomolewa na tingatinga kufuatia mgogoro wa muda mrefu wa viwanja hivyo ambapo umesababisha Shakoor kulia kama mtoto.

 

Akizungumza na paparazi wetu Shakoor alisema yeye pamoja na ndugu zake hao waliuziwa viwanja hivyo mwaka 2002 na aliyekuwa mkazi wa eneo hilo, Mwinyi Kombo ambaye kwa sasa ni marehemu. “Baada ya kutuuzia tulifuata taratibu zote za kisheria za umiliki wa ardhi na tukazikamilisha na kupata hati hizo na kuanza kujenga.

Mimi nimejenga nyumba hii iliyobomolewa (anaionesha) na shemeji yangu Dossa yeye ndiye mwenye lile ghorofa unaloliona limeshaanza kubomolewa. “Huyo mzee alituuzia hili eneo ndugu 16 ambao tuliona tupanunue ili tufanye kama kijiji chetu lakini ndiyo hivyo tena haya yametufika sasa hatuna la kufanya.”

 

Shakoor aliongeza kuwa, wakiwa wameshajenga tangu kipindi hicho 2016 waliletewa barua na kuambiwa viwanja vyao vina mgogoro wakatajiwa watu wawili; Mtemi Naluyaga na Orestic Ngulumi kuwa walikuwa wakipambana mahakamani kila mmoja akisema eneo hilo ni mali yake. “Baada ya kusikia hayo tulianza kupigwa na butwaa na mbaya zaidi aliyetuuzia tayari alishafariki hivyo hatukuwa na mtetezi zaidi ya hati zetu.”

 

Aidha, alisema kuwa katika malumbano ya mahakamani Mtemi alishinda kesi na kuja kuwataka wabomoe nyumba zote ambapo walimwambia hawamfahamu wala kesi yao haikuwa ikiwahusu.

 

“Tulimwambia hivyo kwa kuwa sisi tuliuziwa viwanja hivyo na mtu mwingine kabisa na tuna hati za serikali za kumiliki eneo hilo kwa hiyo baada ya kumueleza tukaamua kufungua kesi Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi uliotolewa wa kuvunjiwa nyumba zetu na mtu tusiyemfahamu,” alisema. Shakoor alidai kuwa, kabla kesi hiyo haijatolewa uamuzi walishangaa kupigiwa simu na kuambiwa kuwa nyumba zao zinabomolewa.

“Tukiwa kwenye mihangaiko yetu tulishangaa kupigiwa simu na watu waliokuwa nyumbani na kuambiwa kuwa nyumba zetu zilikuwa zikibomolewa hivyo ikabidi turudi haraka ambapo tulikuta nyumba zetu zikiendelea kubomolewa.  “Yaani ndugu mwandishi roho iliniuma sana kuona nyumba yangu na za ndugu zangu zikibomolewa, mbaya zaidi ikiwa hata rufaa yetu bado haijatolewa uamuzi.

 

“Nilitaka kuzua jambo baya ambalo wasingelisahau lakini wale mabaunsa na askari waliokuwa wakisimamia zoezi hilo walianza kunishambulia na kwenda kuniweka ndani mimi na huyu shemeji Dossa lakini baadaye walituachia,” alisema Shakoor.

STORI: Richard Bukos Dar es Salaam

Toa comment