The House of Favourite Newspapers

Anayedaiwa kuuawa ndani ya teksi ni huyu

0

Stori: Dustan Shekidele
Morogoro:
Lile tukio la mwanamke anayedaiwa kuuawa ndani ya teksi limeacha majonzi makubwa kwa familia yake kufuatia mwili wake kutopatikana hadi sasa ambapo ndugu zake wamemuelezea kiundani ndugu yao huyo.
Akihojiwa na mwandishi wetu, msemaji wa familia hiyo, Agustino Dominick alimuelezea mwanamke huyo anayedaiwa kuuawa ajulikanaye kwa jina la Ulumi huku akifafanua kwa undani tukio lilivyotokea.

“Ulumi katika maisha yake hajabahatika kupata mtoto, mimi ni mkwe wangu, mke wangu anamwita mama mdogo, baada ya kustaafu kazi ya uuguzi mkoani Singida alihamia hapa Morogoro,” alisema Dominick na kuongeza:
“Siku zote dereva wake wa teksi alikuwa ni mmoja tu, Omari Selemani Mwanamtwa na sisi kama familia tulikuwa tukimtambua, hata aliponunua nyumba yake Omari alikuwa ndiyo shahidi yake.

“Siku ya tukio mama mkwe alikuwa na safari ya benki, kama kawaida alikwenda na Omari.”
Akiendelea kuelezea tukio hilo, Dominick alisema baada ya kuona muda unasonga na mama yake harejei nyumbani alimpigia simu ambapo iliita bila kupokelewa licha ya kupiga zaidi ya mara 10.

“Mke wangu aliniambia twenda kuripoti polisi. Tulienda kituo kikuu na polisi walitupa maelekezo ya kwenda hospitali eneo la mapokezi, wodini na mochwari ambapo hatukufanikiwa tukaenda  Stendi ya Msamvu tukamtafute Omari lakini hatukumkuta.

“Leo ni siku ya 15 tunaomboleza tunaamini Omari akikamatwa ataonesha alipouweka mwili wa mama yetu, polisi watusaidie,” alisema Dominick.

Tukio hilo lilitokea Machi 7, mwaka huu ambapo Machi 8 gari la Omary lilikutwa katika kituo cha mafuta kilichopo kandokando ya Barabara ya lringa, likiwa limetapakaa damu na baiskeli inayodhaniwa kuwa ni ya Ulumi ikiwa kwenye boneti.

Leave A Reply