The House of Favourite Newspapers

Auawa kikatili kwa kuchomwa visu baa

0

NA IGENGA MTATIRO
Risasi Jumamosi
Mara: Ryoba Marwa Hamba (24), mkazi wa Kijiji cha Nyangoto, Tarime mkoani Mara ameuawa baada ya kudaiwa kuchomwa visu sehemu mbalimbali za mwili wake, huku chanzo cha tukio hilo kikiwa hakijulikani.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Ryoba alifikwa na mauti usiku wa Machi 20, 2016 katika baa moja maarufu kijijini hapo ambapo inadaiwa kuwa marehemu alishambuliwa na watu kadhaa waliokuwa na vitu vyenye ncha kali na kumsababishia mauti.

“Inaonesha alikuwa anapigana na wenzake, sijui walianzia nini, wakamchangia na kumzidi nguvu, wakamchomachoma kwa visu mpaka alipofikwa na mauti,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutochorwa jina gazetini.
Tukio hilo lilithibitishwa na Jeshi la Polisi na kupewa namba NYM/RB/541/2016 huku mtu mmoja anayedaiwa kuhusika na tukio hilo, aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Boaz au maarufu kama Man’genyi Gichere Sonora, mkazi wa Kijiji cha Nyangoto akikamatwa na jeshi la polisi.

Habari zaidi zinaeleza kuwa baada ya kukamatwa, Emmanuel alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya mauaji katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime lakini mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji na badala yake, imehamishiwa Mahakama Kuu Mwanza itakapoendelea kusikilizwa.

Kwa mujibu wa baba wa marehemu, Israel Marwa Hamba, kabla ya tukio hilo, Oktoba 21, 2014, mwanaye alipatwa na tukio jingine ambalo almanusura likatishe uhai wake baada ya kudaiwa kupigwa risasi na walinzi wa mgodi mmoja wa dhahabu uliopo mkoani humo wakati akiokota mawe ya dhahabu katika eneo la mgodi.

Inaelezwa kwamba alienda kuponea Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam baada ya kushindikana kupona katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.
“Naona ni Mungu tu hakupanga mwanangu aishi miaka mingi duniani kwani aliandamwa na majanga muda mwingi,” alisema mzee huyo.

Leave A Reply