The House of Favourite Newspapers

Apigwa Risasi ya Mguu Akidhaniwa Nyani

0

 

TATU Bakari Hassan, mkulima mwenye miaka 55 mkoani Pwani, amejeruhiwa mguu wake wa kulia kwa kupigwa risasi akiwa shambani kwake baada ya kudhaniwa kuwa  ni nyani ambapo jeshi la polisi mkoani humo linamshikilia mkulima Mhina Mrisho Ally (47) anayedaiwa kumjeruhi mkulima huyo.

 

 

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa, amesema pia kwamba mtuhumiwa Mrisho alipokwenda kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na bunduki mbili aina ya gobore ambazo anazimiliki kinyume na sheria.

 

 

Wakati huohuo, jeshi hilo linawashikilia wahamiaji haramu sita, raia wa Malawi, waliokuwa wakisafirishwa kutoka Mbeya kwenda Dar es salaam, kinyume na sheria huku wakiwa wameingia nchini bila vibali.

 

 

Wahamiaji hao haramu wamekamatwa eneo la Tanita, Kibaha,  pamoja na dereva wa gari namba T.703 DTR aina ya Toyota Hiace (jina limehifadhiwa) mkazi wa Uyole Mbeya. Wankyo alieleza kwamba wahamiaji hao walikuwa wanapelekwa Dar es Salaam kufanya kazi ya kuuza baa na kusuka.

 

 

Alitoa siku saba kwa wale wote wanaomiliki silaha bila vibali kuzisalimisha silaha hizo na wakibainika katika operesheni za kipolisi basi hatua kali zitachukuliwa. Pia aliwakemea madereva wanaohusika kusafirisha wahamiaji haramu kuacha mara moja na wakikamatwa sheria itachukua mkondo wake.

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Leave A Reply