The House of Favourite Newspapers

Asha Boko Atamani Mzee Majuto Arudi Duniani!  

0

UKIZUNGUMZIA vipaji vikubwa vya uchekeshaji ambavyo havijawahi kuchuja Bongo, huwezi kuacha kumtaja Asha Boko.

 

Ni mchekeshaji mkongwe ambaye amekuwa akifuatiliwa na mashabiki wa tasnia ya filamu na vichekesho kutokana na kipaji kilicho ndani yake na jinsi anavyotumia umbo lake kubwa kwa kuvaa uhalisia.

Jina lake halisi ni Tatu Yusuph, zao kutoka kundi kongwe la sanaa la Kaole akiwa na waigizaji wengine wakubwa na wenye majina kwa sasa.

 

Asha Boko amewahi kutamba na sinema kama Mgeni wa Kijiji, Namtoa Mwanangu Suna, Mama Shughuli, Gusa Unase, Nani Chizi na nyingine kibao.

Mbali na kucheza filamu hizo, pia ameshiriki kwenye Tamthiliya ya Kapuni ambayo imekuwa ikifanya vizuri kupitia Chaneli ya Maisha Magic Bongo ndani ya DSTV.

 

IJUMAA WIKIENDA linakusogeza karibu na Asha Boko kwenye mahojiano maalum (exclusive interview) ambapo amefunguka mengi usiyoyajua, ila kubwa zaidi ni kuhusiana na kutamani uwepo wa aliyekuwa nguli wa vichekesho Bongo, Alhaji Amri Athuman ‘King Majuto’ ambaye ametangulia mbele ya haki;

 

IJUMAA WIKIENDA: Mashabiki wangependa kufahamu Asha Boko ni mtu wa aina gani?

ASHA BOKO: Ni mtu wa watu ambaye anapenda kuishi na watu vizuri, anapenda kukosolewa pale anapokosea.

IJUMAA WIKIENDA: Ni mwigizaji gani aliyekuvutia hadi ukaamua kuingia kwenye uigizaji?

 

ASHA BOKO: Ni Mzee Majuto (marehemu), nilikuwa nampenda sana na kufuatilia jinsi anavyoigiza. Alikuwa ananivutia kiasi cha kuamua kuanza kuigiza.

IJUMAA WIKIENDA: Ukiambiwa uchague mwigizaji mmoja ambaye ametangulia mbele ya haki na umrudishe duniani, utamchagua nani?

ASHA BOKO: Kwa kweli hakuna nitakayemchagua zaidi ya Majuto.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa nini Majuto na siyo wasanii wengine?

ASHA BOKO: Ni mtu ambaye alikuwa ana upendo na watu, alikuwa anahitaji kila mmoja wetu afanikiwe. Yeye ndiye amenifanya mpaka sasa nipo hapa na kujulikana.

 

IJUMAA WIKIENDA: Ni kitu gani hasa unakumbuka kutoka kwake?

ASHA BOKO: Kipindi cha uhai wake, aliahidi kunifanyia mambo mengi sana, lakini Mungu alimpenda zaidi, natamani angerudi kwa mara nyingine duniani.

 

IJUMAA WIKIENDA: Je, familia yako inachukuliaje kipaji chako?

ASHA BOKO: Namshukuru sana Mungu watoto wangu wananisapoti. Wamekuwa mstari wa mbele kunisapoti. Huwa wananifariji na wanapenda ninachokifanya, kwa sababu ndiyo kazi ambayo inafanya niwasomeshe wao.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa sasa una watoto wangapi?

 

ASHA BOKO: Wawili, maana tangu tulivyovamiwa na majambazi na mume wangu akauawa, sijawahi kuwa na mtoto mwingine. Mwanangu mkubwa yupo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ninamshukuru Mungu kwa hili.

IJUMAA WIKIENDA: Pole kwa kufiwa na mumeo.

ASHA BOKO: Asante.

 

IJUMAA WIKIENDA: Ni muda sasa tangu mumeo afariki dunia, je, uliwahi kuwaza kuolewa na mwanaume mwingine?

ASHA BOKO: Bado sijawaza kuolewa, nipo nawalea watoto wangu.

IJUMAA WIKIENDA: Wewe ni mkongwe kwenye uigizaji, je, unazungumziaje uigizaji wa sasa ukilinganisha na ule wa zamani?

 

ASHA BOKO: Kwa sasa namshukuru Mungu tumepiga hatua kubwa na huwa tunahakikisha kila siku mashabiki wetu wanapata ladha tofauti.

IJUMAA WIKIENDA: Umeonekana kukubalika kwa mashabiki wako, je, mipango ya kazi za nje ya nchi ikoje?

ASHA BOKO: Nimewaza sana, naamini kila ndoto ya msanii wa hapa Bongo ni kufanya kazi na wasanii wa nje ya nchi. Kwa upande wangu siku yangu haijafika tu, siku ikifika nitafanya, kila kitu huwa anapanga Mungu.

 

IJUMAA WIKIENDA: Wewe ni kiraka maana kila uhusika unaweza, je, ni uhusika gani ambao unakupa changamoto sana?

ASHA BOKO: Nikipewa uhusika wa kuigiza masuala ya mapenzi, ni kitu ambacho kinanishinda. Sipendi maana huwa inaniwia vigumu kwa sababu mimi ni mtu mzima jamani.

 

IJUMAA WIKIENDA: Ni uhusika gani kwenye filamu ukipewa unautendea haki?

ASHA BOKO: Nikipewa uhusika wa kumchamba mtu, mbona watazamaji watafurahi kwa sababu huwa nampania kama ni kweli, kumbe ni kuigiza tu.

IJUMAA WIKIENDA: Je, uko kwenye menejimenti au?

 

ASHA BOKO: Hakuna mtu anayenisimamia, najisimamia mwenyewe.

IJUMAA WIKIENDA: Ni changamoto gani unazipitia kwenye kazi yako?

ASHA BOKO: Changamoto zipo nyingi tu, ila kwa mimi sichukulii kama ni changamoto, ni sehemu ya maisha yangu, hivyo napiga moyo konde na maisha mengine yanaendelea.

 

IJUMAA WIKIENDA: Kazi ya sanaa imekupa mafanikio gani?

ASHA BOKO: Mafanikio ninayojivunia, kwanza nimepata umaarufu, najulikana na watu wengi hata mtoto mdogo ukimwambia akuelezee Asha Boko anakwambia. Nimefanikiwa kujenga kibanda changu, sikai nyumba ya kupanga.

MAKALA: Khadija Bakari, Bongo

Leave A Reply