The House of Favourite Newspapers

Askari Waliofariki kwa Ajali Njombe Waagwa

0

MAMIA ya wananchi wamejitokeza jana, Jumanne, Fenruari 4, 2020, katika viwanja vya jeshi la polisi mkoani Njombe kuaga miili ya askari watatu waliofariki katika ajali mapema alfajiri ya tarehe tatu ambapo ajali hiyo ilihusisha basi la abiria kampuni ya Sharon lenye namba za usajiri T349 CXD na gari la polisi lenye namba za usajili PT 3734.

Askari waliofariki katika ajali hiyo ni namba H 4401 Marianus Said Hamissi, namba H6802 PC Michael Mwandu na askari namba H 7486 PC Hery Athmani,  ambapo wote wamesafirishwa kuelekea makwao kwa ajili ya maziko.

 

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari hao,  Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Cristopher Ole Sendeka, amesema  serikali imepoteza vijana muhimu ambao wamefariki wakati wakienda kulitumikia taifa na kuwataka askari wengi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Ajali hii imeondoa vijana wetu watatu, wawili wapo Moi Muhimbili tumewakimbiza jana kwa ndege na wengine wapo kwenye hospitali yetu ya Kibena na hakika vyombo vyote vitasimamia kujua ukweli wa tukio hili na aliyefanya dhambi hii kwa uzembe atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Ole Sendeka.

 

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issa,  amewashukuru wakazi wa mkoa wa Njombe kwa kujitokeza kwa wingi  na kujitolea michango  kuhakikisha askari wote waliofariki wanasafirishwa kuelekea kwao kwa ajili ya maziko.

 

“Wananchi mmeonyesha ni jinsi gani mna upendo na vijana wenu, na hawa waliofariki kwa kweli wamefariki wakiwa wanaenda kutimiza jukumu la kisheria, tunawashukuru sana,” alisema Issa.

 

Mmoja wa wakazi mkoani hapa, Solanus Mhagama, amesema amesikitishwa na kifo cha askari hao ambao walikuwa bado vijana wadogo na hivyo kuiomba serikali kuweka matuta pamoja na kutanua barabara hiyo ili kuepusha ajali katika eneo hilo ambalo lina mlima mkali.

 

Ajali hiyo iliyosababaishwa na mwendokasi wa gari la abiria ilipelekea vifo vitatu vya askari wa polisi kikosi cha kutuliza gasia mkoani Njombe huku wengine tisa wakiendelea na matibabu katika hospitali ya mjini  Njombe Kibena na hospitali ya taifa Mhimbili.

 

Ibada ya kuagwa miili hiyo imehudhuriwa na viongozi wa dini mbalimbali ambapo wametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazosababishwa na uzembe.

 

Leave A Reply