The House of Favourite Newspapers

Askofu Niwemugizi: Magufuli Aliagiza Nirejeshewe ‘Passport Yangu’

0

ASKOFU wa Kanisa Katoliki jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi amesema aliyekuwa Rais wa Tanzania marehemu, John Magufuli aliagiza arejeshewe hati yake ya kusafiria na alimtamkia mara mbili kuwa kiongozi huyo wa kiroho ndiye atakayemzika.

 

 

Hati ya kusafiria ya Niwemugizi ilichukuliwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2017 pamoja na ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe na mkurugenzi wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze wote ikielezwa kuwa uraia wao ulikuwa ukichunguzwa.

 

 

Akizungumza leo Alhamisi Machi 25, 2021 katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria Parokia ya Chato, Askofu Niwemugizi ambaye hakutaja muda maalum wa agizo la kurejeshewa hati hiyo, amesema Magufuli aliagiza idara ya uhamiaji kumrejeshea.

 

 

Niwemugizi asema maisha, kifo cha Magufuli ni funzo kwa Watanzania; “Kwa kweli niwaambie mara mbili, Magufuli aliniambia, ‘wewe ni Askofu wangu utanizika. Mwaka ule 2015 akaniambia hivyo, mara ya pili akamwagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji anirudishie passport akaniambia wewe ni Askofu wangu utanizika.”

 

 

“Mimi nikamwambia mzee hakuna anayejua atakayemtangulia mwenzake. Yule atakayetangulia anayebaki atamzika mwenzake. Maneno hayo sasa yametimia mwenzangu ametangulia,” amesema Askofu Niwemugizi.

 

 

Amebainisha kuwa tangu Magufuli alipochaguliwa kuwa Rais alifika katika kanisa hilo na kumwombea kama mwanajimbo mwenzao akisema wakati wote aliwakilisha vizuri jimbo hilo. Huku akitaja vifungu vya Biblia, amewaeleza waumini wa kanisa hilo kuhusu nini maana ya kifo na kujiandaa.

 

 

“Baadhi yenu mnamkumbuka mwanamuziki Remmy Ongala, aliimba sana juu ya kifo. Kati ya nyimbo nyingi alizoimba ni ule wa kifo hakina huruma na wimbo mwingine aliimba kama ingewezekana kukata rufaa ya kifo na yeye angekata. Mimi naamini sana Chato sana na Ngara kama tungeweza kukata rufaa ili ndugu yetu aendelee kututumikia, tungekata,” amesema.

 

 

Amesema kwa mujibu wa Biblia kifo ni matokeo ya dhambi kwani kilianza baada ya Adam na Hawa kula tunda la mti waliokatazwa na Mungu.

 

 

“Katika kifo na ufufuko wa Yesu kifo kimeshindwa, lakini kifo cha kwanza siyo tatizo, kwani kila mtu lazima afe. Kifo kibaya ni kile cha pili ambapo roho inapotengana na Mungu. Hayati Magufuli kifo cha kwanza ameondoka je cha pili atakiepuka? Tuamini Magufuli amepumzika,” amesema.

 

 

Askofu Niwemugizi amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan akisema anasubiri atekeleze ahadi yake ya kutekeleza aliyofanya Hayati Magufuli.

 

 

“Mimi nimemsikia akisema kule Dodoma kwamba yale aliyoyatamani Magufuli yakiwa katika nchi ya Tanzania yeye atayakamilisha. Kati ya aliyotamani Magufuli nakumbuka mwaka 2009 nafikiri nilikuwa hapa alimwambia Waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda kuwa alitamani kuona Chato inakuwa makao ya mkoa, sasa sijui mheshimiwa Samia atalikamilisha,” amesema.

Leave A Reply