The House of Favourite Newspapers

Zijue Athari za Pombe Kwenye Uhusiano au Ndoa

Mwandishi : Masele Chapombe | AMANI| Sindano za Mastaa

UHALI gani mpenzi msomaji wangu? Ni matumaini yangu una afya njema. Msomaji wangu wa Sindano za Mastaa, wiki jana ulikuwa na staa wa filamu za Kibongo, Daud Michael ‘Duma’. Leo uko nami staa wa sinema na vichekesho Bongo, Crispin Masele a.k.a Masele Chapombe. Leo nitakufungukia kinagaubaga athari za pombe kwenye uhusiano wa kimapenzi, uchumba na ndoa. Nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kipaji changu cha kuigiza kama mlevi ingawa katika uhalisia huwa si mlevi kama ambavyo wengi wamekuwa wakiniona au

kunidhania. Huwa naonja mara mojamoja ila kwenye runinga huwa nafanya kazi ya sanaa. Pombe si mbaya ila ukizidisha ni hatari kwa afya na maisha yako kwa jumla. Wapo wapenzi wengi ambao mapenzi yao yamevunjika kwa sababu ya ulevi wa kupindukia. Japokuwa jinsi zote wanaweza kuwa walevi, lakini kwa asilimia kubwa nawazungumzia wanaume ambao ndiyo hasa wana jukumu la kulinda, kutunza, kupenda na kumridhisha mwandani wake.

MIKIKIMIKIKI YA FARAGHA

Utafiti unaonesha kuwa baadhi ya watu wanapokuwa wamelewa kupita kiasi basi hata ile mikikimikiki ya faragha hupungua. Kitendo cha mmojawapo kushindwa kumridhisha mwenza wake wanapokuwa uwanja wa taifa wa sita kwa sita, kwa kushindwa kumaliza dakika tisini za mechi, hali hiyo inaweza kuhatarisha mustakabali wa uchumba au ndoa yako.

KUCHEPUKA

Upo usemi unaosema kuwa baadhi ya watu wakilewa basi pombe walizokunywa hukimbilia maeneo hatarishi, huwafanya wawe na ‘apetaiti’ ya kushiriki tendo la ndoa, tena wakati mwingine bila kinga. Mpenzi msomaji nayafungukia haya ili kukufanya ujifunze na ikiwezekana uachane na unywaji wa pombe wa kupindukia. Mbaya zaidi uwezekano wa kutumia kinga ni mdogo mno, jambo ambalo huhatarisha afya yako na familia yako kwa jumla.

KUMFANYA ACHEPUKE Wapo wanaokunywa pombe wakifika nyumbani husahahu majukumu ya kuwaridhisha wenza wao na matokeo yake wakifika ni kujitupa kitandani na kulala fofofo. Hili ni tatizo kubwa mno, kama unaishi na mwanamke anaweza kuvumilia kwa muda mchache, lakini kama utaendelea na tabia hiyo bila kujirekebisha basi fahamu kuwa unamsababishia kutafuta mchepuko.

KUTOKUFANIKIWA

Inapofika hatua pombe inachukua sehemu kubwa ya maisha yako ni dhahiri hata muda wa kuzungumza na mkeo au mwenza wako juu ya maendeleo ya familia yenu, unakuwa haupo. Huwezi kufanikiwa kwa kuingia baa na shilingi laki moja, unakunywa bia, kula mapochopocho, kuwapa ofa za kinywaji marafiki na michepuko yako kisha utegemee kufanikiwa.

KUKUSHUSHIA HESHIMA

Pombe ambayo umezoea kuinywa kwa kuhisi inakupa faraja, inaweza kukushushia heshima kwenye penzi, ndoa yako au mtaani, kwa sababu ukishalewa unafanya mambo ya hovyo, mambo ambayo ukiambiwa ukiwa hujalewa unakataa na kuamini huwezi kuyafanya.

KUWA MKALI

Mtu mwingine pombe humfanya anakuwa mkali, hata kitu kidogo tu kikikosewa na mwenza wake au mtoto wake, basi ni kipigo ni matusi mwanzo mwisho. Pombe inakutenganisha na watoto wako kwa sababu wanaogopa kumuomba baba au mama fedha ya daftari kwa kuhofia kukaripiwa, hili si sawa kama unapenda kuwa na familia nzuri na bora.

KUTOJALI FAMILIA

Pombe unayokunywa ikikutawala, basi hutakuwa na muda wa kujali familia, mpenzi, mkeo au mumeo. Muda mwingi unautumia kazini na kwenye mabaa, watoto hawapati muda mzuri wa kuongea na baba yao kwa sababu ukirudi ni usiku wa manane, wao wakiwa wamelala na unaondoka alfajiri wakiwa bado wamelala. Yako wapi mapenzi na familia yako? Kwa leo naishia hapa lakini usikose kusoma Sindano za Mastaa kila wiki ili kubadilishana mawazo na mastaa wako. Bye! Je, unapenda wiki ijayo msanii gani atoe Sindano za Mastaa? Tuma maoni yako na ushauri kupitia namba 0679979785.

Comments are closed.