The House of Favourite Newspapers

Baada ya Kuoana Kimya Kimya… Sherehe ya Lulu & Majizzo Usipime!

0

 

BAADA ya kufunga ndoa isiyokuwa na mbwembwe, taarifa zinaeleza kuwa, muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ anatarajia kuangusha bonge la sherehe sanjari na mumewe, Francis Shiza ‘Majizo’, RISASI limetonywa.

 

 

Lulu na mumewe huyo ambaye ni Mkurugenzi wa EFM Radio na ETV, walifunga ndoa hiyo wiki kadhaa zilizopita katika Kanisa la Mt. Gasper Mbezi Beach jijini Dar. Baada ya kumaliza kufanya tendo hilo takatifu kanisani, watu walitegemea kuona shamrashamra hasa ukizingatia umaarufu wa wawili hao lakini mambo yakawa tofauti.

 

 

WALIKWENDA HOTELI

Walipotoka kanisani, walipanda gari lao na kwenda kumpumzika hotelini kabla ya kuendelea na mishemishe zao za kila siku.

 

 

TUJIUNGE NA CHANZO

Kikizungumza na RISASI chanzo cha kuaminika kilicho karibu na familia, kimesema zoezi la sherehe lilishindikana kutoka na mazingira kubana hasa kwa kuzingatia, mwezi wa toba (Kwaresma) ulikuwa unaanza.

 

“Si unajua siku waliyofunga ndoa, kesho yake tu ndio mfungo wa Kwaresma ulikuwa unaanza na kwa kawaida, Wakatoliki huwa hawafanyi sherehe kwenye kipindi cha Kwaresma. “Kipindi cha Kwaresma, Wakatoliki huwa wanakitumia kufunga, kusali na kusaidia wasiojiweza na sio kufanya sherehe,” kilisema chanzo hicho.

 

 

NI BAADA YA KWARESMA

Chanzo hicho kilisema, sherehe ya wawili hayo inatarajia kufanyika baada ya mfungo huo wa Kwaresma na itakuwa baab’kubwa. “Itakuwa ni ya kukata nashoka, wewe vuta picha wale wote ni maarufu unategemea nini?” kilihoji chanzo hicho.

 

CHAZIDI KUTIRIRIKA

Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, sherehe hiyo waalikwa watapewa mualiko maalum wa kuhudhuria na haitakuwa na michango kama ambavyo wengi wamezoea. “Yani wewe unapewa tu mualiko unakuja ukumbini sio mambo ya kuchangishwa, yani wewe unatakiwa tu uwe unajulikana na wahusika, wanakuita basi mambo yanakwenda kuwa safi,” kilisema chanzo hicho.

 

 

KURUSHWA LIVE

Kuonesha uspesho wake, chanzo hicho kiliweka wazi kuwa sherehe hiyo itaruka live kwa luninga ambazo tu zitakuwa zimechaguliwa na si kila luninga. “Yani hapo naona sanasana labda luninga yao ya TVE ndiyo itakayorusha lakini si nyingine yoyote maana wao ndio watakuwa na haki miliki za kuonesha,” kilisema chanzo hicho.

 

 

MASTAA KAMAWOTE

Chanzo hicho kilimalizia kwa kusema, kwa kuzingatia Lulu ni muigizaji na Majizo ni mdau mkubwa wa burudani, kwenye sherehe hiyo kutasheheni mastaa kutoka kada mbalimbali. “Yani wanamichezo, wanasiasa, waigizaji, wasanii wa Bongo Fleva na sanaa nyingine zote siku hiyo patakuwa hapatoshi, tuombe tu uzima,” kiliweka nukta chanzo hicho.

 

 

TUJIKUMBUSHE

Safari ya Lulu na Majizo ilianza kitambo kiasi cha watu wengi kutotegemea kama wawili hao wanaweza kufikia hatua ya kufunga ndoa.

 

PETE ZAIDI YA MIAKA MITATU

Pete ya uchumba alikaa nayo kwa zaidi ya miaka mitatu tangu alipovishwa mwaka 2018 huku baadhi ya mashabiki wake wakimponda kila kukicha kuwa anatakiwa aolewe. Kutokana na maoni ya mashabiki hao, Lulu alikuwa akijikuta akipaniki na kuwajibu vibaya kiasi cha kuibua mjadala na mashambulizi makali.

 

ILIBUMA?

Matangazo ya kufungwa kwa ndoa ya Lulu na Majizo yalianza kusikika katika Kanisa Katoliki la Mbezi-Beach jijini Dar, mwezi Oktoba, mwaka jana. Kwa mujibu wa matangazo hayo, ndoa ya Lulu na Majizo ilipangwa kufungwa Novemba 2, mwaka jana, lakini ghafla kukaibuka sintofahamu. Baada ya sintofahamu hiyo kupita, ndoa hiyo ilifungwa rasmi Februari 16, siku moja kabla ya Mfungo wa Mwezi wa Kwaresma kuanza.

 

 

KABLA YA MAJIZO

Kabla ya Lulu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Majizo, alikuwa akitoka na aliyekuwa kinara wa filamu za Kibongo, marehemu Steven Kanumba, ambaye baadaye aliingia matatani kwa kuhusika na kifo chake.

 

Kanumba alifariki dunia Aprili 7, 2012 kwa kile kinachotajwa kuwa, ni baada ya kutokea ugomvi wa kimapenzi kati yake na Lulu, ambaye alikwenda nyumbani kwa Kanumba usiku wa tukio hilo.

 

 

Kufuatia kifo cha Kanumba, Lulu aliingia kwenye msukosuko wa kisheria, hadi Novemba 2017 alipokutwa na hatia ya kuua bila kukusudia na mahakama kumfunga jela miaka miwili. Hata hivyo, Mei 12, 2018, staa huyo alitoka jela na kutakiwa kumalizia kifungo chake kwa kufanya kazi za kijamii kwa amri ya Mahakama Kuu.

 

 

Kufuatia mauaji hayo ya kutokusudia ya Kanumba, Lulu alijikuta kwenye mgogoro na mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa. Mara kadhaa mama Kanumba amenukuliwa akimlaani Lulu, kwa kile alichokuwa akikitaja kuwa ni kuhusika kwake na kifo cha mwanaye na baadaye kujitenga naye.

Stori Mwandishi Wetu, Risasi

Leave A Reply