The House of Favourite Newspapers

Baba P… Baba Pili… Baba Pilima!-17

0

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA:
“He! Mume wa mama Pilima?”
“Ndiyo…”
“Mbona hata mimi pia imekuwa hivyo…”
“Wewe lini?”

“Muda si mrefu ndugu yangu.”
Simu ya mama Pilima iliita akiwa nje ya baa hiyo, alipoangalia mpigaji ni mume wake…
SASA JIACHIE KIVYAKO…

Aliipokea huku akitetemeka…
“Halo baba Pilima…”
“Najua umeona ushatani wako ulipokuwa. Umekuwa mwaminifu miaka yote unakuja kuanguka mbeleni huku mke wangu…”
“Nisamehe baba Pilima…”

“Kwanza ujasiri wa kutembea na wanaume wawili umeutolea wapi mke wangu?”
“Baba Pilima ni hadithi ndefu, wale akina kaka ni mapacha. Walitumia nafasi hiyo kunipata wote nikiwa sijui kama ni mapacha,” alisema mama Pilima akitumia sauti ya chini sana yenye kuonesha majuto ni mjukuu…

“Sikiliza mama Pilima, mimi kutoka moyoni mwangu nimekusamehe!”
Mama Pilima alianguka chini nje ya kituo cha mabasi, watu wakaanza kutafutana. Habari za kuanguka kwake zilifika hadi ndani ya Baa ya Sewa ambapo, baba Pilima feki ni mmoja wa watu waliosikia, lakini hakujua ni nani!

Alipotoka kuangalia na kumkuta ni mama Pilima alishtuka sana. Lakini kwa sababu ya mambo yaliyotokea hakutaka kumsaidia wala kuendelea kusimama kuendelea kuangalia pale…
“Mh! Huu ni msala. Jamaa yake akitokea inaweza kuwa balaa,” alisema moyoni baba Pilima feki huku akiondoka zake eneo hilo.

Baba Pilima alishangaa sana mkewe kukatika hewani ghafla halafu huku akisikia kishindo kikubwa cha puu! Alipojaribu kumpigia hakuwa hewani…

“Khaa! Sasa huyu amekumbwa na kitu gani tena?” alijiuliza baba Pilima.
Baadhi ya vijana wa kihuni waliinyakua simu ya mama Pilima na kutokomea nayo wakiwa wameshaizima na ndiyo maana mume wake hakumpata tena hewani.

Kutokana na tukio hilo la aina yake, baba Pilima mwenyewe aliamua kurudi nyumbani kupumzisha akili siku hiyo huku akimuwaza mkewe na alichokifanya. Lakini bado ndani ya moyo wake aliamini, yaliyotokea yamekuwa funzo kwa mwanamke huyo.
***
Ndani ya dakika kumi, mama Pilima naye aliamka. Au alizinduka. Ama fahamu zilimrejea, akakaa na kuangalia kulia na kushoto, mbele na nyuma na kubaini nini kilimtokea muda mfupi nyuma.
Mkoba wake ulikuwepo, lakini simu hakuiona. Miongoni mwa watu waliokuwa wakimfuatilia pale chini ni wanawake wenzake na watu wazima tu, vijana wote, wakiwemo wa kihuni walikuwa hawana habari…
“Simu yangu,” alisema mama Pilima…

“Watakuwa wameikwapua vibaka,” walisema watu.
Mama Pilima alisimama kwa kujizoazoa, akapanda basi na kukaa siti ya nyuma kabisa akiwa peke yake. Baadhi ya sehemu za nguo zake zilichafuka kutokana na kuanguka…

“Kweli baba Pilima anaweza kunisamehe kwa kosa kubwa kama hili? Hata siamini! Labda nilimsikia vibaya,” alisema mwanamke huyo akiwa kweli haamini kama amesamehewa.

Alipofika nyumbani, alimkuta mumewe, baba Pilima, wifi yake pia alikuwepo sebuleni. Msichana wa kazi akiendelea na kazi za kupika. Watoto, akiwemo Pilima walikuwa hawajarudi toka walikokwenda.
Wifi mtu alishtuka sana kumwona mama Pilima amechafuka vile…

“Ha! Wifi…umekutwa na jambo gani? Mbona umechafuka?”
Mama Pilima alimwangalia mumewe badala ya aliyemuuliza swali. Alijua mumewe atasema yote…
“Wifi nilianguka nikapoteza fahamu,” alisema mama Pilima na kuanza kulia.
Ikawa hekaheka nyingine, wifi mtu huyo akiwa anataka kujua kwa undani kuhusu wifi yake kuanguka ghafla na kupoteza fahamu…

“Haa! Kaka! Wewe unajua lolote?”
“Nilikuwa naongea naye, lakini ghafla akapotea hewani. Nilipokuwa nampigia tena, hakuwa hewani. Nadhani ndiyo alianguka hapo.”

“Wifi…”
“Abee…”
“Pole sana. Sasa simu iko wapi?”
“Imeibiwa wifi,” alisema mama Pilima.
Baba Pilima alimshika mkono mke wake mpaka chumbani. Alimvua nguo, akamvalisha kanga na taulo na kumtaka akaoge.

Baada ya kuoga, mama Pilima na mumewe wakakaa chumbani…
“Mume wangu, asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu. Kwa haya yaliyonikuta mimi nimefunzwa tayari. Nataka kusikia kauli yako kwa mara ya pili kama kweli umenisamehe.”
“Nimekusamehe mama Pilima. Ila likijirudia jambo hilo tena, itakuwa tiketi yetu ya kutengana moja kwa moja,” alisema baba Pilima.

Mama Pilima alipiga magoti, akaweka mikono pamoja kaka anayesali, akamsihi mumewe kuwa na amani. Ujinga ule hautajirudia tena.
“Naomba iwe hivyo katika maisha yako yote.”

“Nakuahidi itakuwa hivyo baba Pilima.”
***
Kwa upande wa wale mapacha, baba Pilima feki na baba Pili walikwenda kukutana sehemu. Wakaongelea lile tukio, wakakubaliana kuzitupa laini zao na kununua mpya ili wasitafutwe. Walijuta na kujuta na kujuta!

MWISHO.
Usikose kufuatilia chombezo jipya kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, siku ya Jumatatu.

Leave A Reply