The House of Favourite Newspapers

Penzi Kabla Ya Kifo-17

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Mwanamke bilionea Afrika, Candy Marcel anaishi katika maisha yenye mateso matupu, hana furaha kwa kuwa hana mtoto, mbali na kutokuwa na mtoto, amekutana na mwanaume aliyetokea kumpenda mno nchini Morocco, huyu aliitwa Rasheed. Hakumwambia ukweli, aliogopa mno mpaka aliporudi nchini Tanzania.SONGA NAYO…

Maisha yake yalitawaliwa na majonzi tele, moyo wake haukuacha kuuma hata siku moja, kila alipokumbuka kwamba hakuwa na uwezo wa kushika mimba, moyo wake ulimuuma kupita kawaida. Hakuacha kulia, hakuacha kuomboleza, kila siku alijiona akipita katika tanuru la moto, alipowaona wanawake wakiwa na watoto wao, moyo wake ulichomwa na kitu chenye ncha kali.

Siku ziliendelea kukatika, mbali na kuumia kwa kuwa hakuwa na mtoto lakini upande wa pili moyo wake ulisumbuka kwa kumuwaza mwanaume aliyekuwa akimpenda, mwanaume aliyekuwa nchini Morocco, Rasheed. Mapenzi yalimuendesha, hakuacha kumfikiria na mara nyingi alihisi kwamba mwanaume huyo alikuwa malaika wa nuru.

Kwa kuwa kila mwezi alikuwa na ratiba ya kwenda katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kuangalia tatizo, hata siku iliyofuata, alikuwa ndani ya gari na rafiki yake kipenzi, Candy na kuanza kwenda huko hospitali, lengo kubwa likiwa ni kuonana na daktari wake bingwa na kumuuliza zaidi juu ya tatizo alilokuwa nalo.

Hawakuchukua muda mrefu wakaingia ndani ya eneo la hospitali hiyo. Kila mtu aliyeliona gari lile lililoelekea sehemu ya mapokezi akabaki akiliangalia tu, lilikuwa gari la thamani kubwa ambalo haikuwa rahisi kumilikiwa na watu wa kawaida hasa katika nchi kama Tanzania.

Elizabeth na Candy wakateremka na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani ya jengo la hospitali hiyo. Hakukuwa na mtu aliyegundua kwamba yule mwanamke aliyevalia juba jeusi na nikabu alikuwa Elizabeth, hivyo wakaishia kuwaangalia tu mpaka walipopotea machoni mwao.
“Nimerudi,” alisema Elizabeth, alikuwa akizungumza na Dk. Kisiju.
“Karibu sana! Unataka nikufanyie nini leo?”

“Tatizo langu lilelile, ninahitaji kupata mimba,” alisema Elizabeth.
“Ila si tulishaangalia na hatukukuta tatizo?”
“Kutokukuta tatizo napo ni tatizo! Naomba uniangalie tena,” alisema Elizabeth.
“Basi subiri.”

Dokta Kisiju akaanza kushughulika na vipimo vya Elizabeth, japokuwa alimpima mara kwa mara na kutokugundua tatizo lolote lile lakini hakuwa na jinsi, aliendelea kumshughulikia zaidi kiasi kwamba mpaka anamaliza na kuangalia tena vipimo, ilikuwa ileile kwamba hakuweza kuona tatizo lolote lile.

Bado kichwa cha Elizabeth kilichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kiliendelea mwilini mwake, vipimo vyote alivyopimwa, hakuonekana kuwa na tatizo lolote lile, swali likaja, kwa nini hakupata mimba?
Hakuwahi kutoa mimba, hakuwahi kufanya mchezo wowote mchafu ambao aliamini kwamba ungeharibu kizazi chake, kitendo cha kutokushika mimba bado kiliendelea kuwa kitendawili ambacho hakuweza kukitegua kabisa.

Hakuyaacha machozi yake kububujika mashavuni mwake, kazi ilikuwa ni ileile kwamba aliumia siku zote za maisha yake. Candy ndiye alikuwa mtu wake wa karibu aliyemfariji kutokana na hali aliyokuwa nayo.
“Futa machozi Eliza…”

“Hakuna tatizo!”
Alishazoea kulia, alishazoea kuumia, hakuwa na jinsi, hakutaka kuendelea kukaa ndani ya ofisi ile, walichokifanya ni kutoka kwa ajili ya kurudi nyumbani huku kile walichokuwa wamekifuata hospitalini hapo, matokeo hayakubadilika bali kilikuwa ni kilekile cha siku zote.

Walipofika sehemu iliyokuwa na lifti, wakasimama nje kwa ajili ya kuisubiria ili waweze kuingia ndani na kushuka chini. Hapo, kulikuwa na wagonjwa wengi waliokuwa wakipita, wengine walibebwa katika machela, walikuwa hoi, wengine kwa kuwaangalia tu, ungeweza kuhisi kwamba wasingeweza kufika kesho, walikuwa hoi.

Wakati wamesimama hapo, mara akatokea nesi mmoja akikisukuma kiti cha walemavu, katika kile kiti kulikuwa na msichana mdogo aliyepooza, alikuwa ameikunja shingo yake kwenda upande wa kulia huku kiganja chake kikiwa kimeelekea chini na udenda kumtoka mdomoni.

Alipomuona msichana yule mdogo, huruma ikamuingia moyoni mwake, hakutaka kuvumilia, alichokifanya ni kumsogelea kisha kumwangalia kwa sekunde kadhaa, hata yule nesi aliyekuwa akimsukuma katika kiti kile alibaki akimshangaa.

“Anaumwa nini?” aliuliza Elizabeth.
“Amepooza, amekuwa kwenye hali mbaya mno,” alijibu nesi yule.
“Poleni sana! Kwa hiyo hana matumaini ya kupona?”
“Mmmh! Kwa kweli sijui.

Je, kilifuatia nini? Usikose mwendelezo wa simulizi hii wiki ijayo.

Leave A Reply