Ateketeza nyumba kwa kuhisi mkewe anachepuka

Na Dustan Shekidele

WIVU mbaya! Mwana-ndoa Alex Bandoma anadaiwa kuchoma moto nyumba waliyopanga huku sababu ya kufanya hivyo ikidaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi kufuatia kunasa meseji aliyoamini ni ya mchepuko iliyoingia kwenye simu ya mkewe, Sabina John (pichani).

Alex Bandoma anayedaiwa kuchoma nyumba baada ya kuhisi mkewe kuchepuka.

Tukio hilo la kushangaza lilijiri wikiendi iliyopita, saa 2:00 usiku kwenye nyumba namba 180 waliyokuwa wamepanga iliyopo Mtaa wa Reli, Kata ya Mazimbu mjini hapa.Mwanahabari wetu alifika eneo la tukio na kushuhudia umati huku baadhi ya waathirika wa tukio hilo wakipekua vyumba vyao vilivyoteketea na kukusanya mabaki ya vitu.

Nguo zikiwa zimeteketea baada ya nyumba kuchomwa moto.

Mmoja wa wapangaji hao, Upendo lssa Timbwanga aliliambia gazeti hili: “Hawa watu kwa muda mrefu walikuwa kwenye mgogoro wa mapenzi. Kila mmoja akimshutumu mwenzake si mwaminifu.“Kabla ya tukio, Alex alirudi nyumbani akitokea kazini. Baada ya muda nikasikia mzozo kwenye chumba chao, Alex akidai kunasa meseji ya mapenzi kwenye simu ya mkewe ambapo wakati anaandaa chakula aliacha simu mezani, meseji ikaingia.

“Meseji ilisema; ‘mbona umenigandisha mpaka muda huu hujatokea au niondoke?’ Akamwita mkewe na kumuuliza meseji hiyo ametumiwa na nani usiku huo. ”Sabina alimjibu alitumiwa na mwanamke mwenzake jambo lililopingwa na Alex. Wakaanza kuzozana, Alex akataka kupiga namba hiyo, Sabina aligoma, ndipo ugomvi uliposhika kasi mpaka kutwangana wakigombea simu hiyo.

“Sisi kama wapangaji wenzao, tuliingia chumbani na kuwaamua. Baadaye walikubaliana kutengana baada ya kila mmoja kudai kuchoshwa na mwenzake hivyo walifikia uamuzi wa kugawana vitu.

”Lakini baada ya muda ulizuka mzozo tena kila mmoja akitaka kuchukua tivii, deki na king’amuzi. Katika mzozo huo, Alex alivunja tivii, Sabina akajibu mapigo kwa kuvunja deki na king’amuzi.”Upendo aliendelea kusema kwamba, Sabina aliamua kwenda kumwita mwenyekiti wa serikali ya mtaa, Khadija Kombo lakini akamkuta msaidizi wake, Habiba Abdallah ambaye aliwapigia simu wajumbe wenzake na kuelekea eneo la tukio.

Mpangaji huyo alisema katika hali ya kushangaza, wakati Sabina anahangaika kuwatafuta viongozi hao, nyuma, Alex alikuwa akikusanya vyombo vya ndani na kuvichoma moto kwa kutumia mafuta ya taa.


Majirani wakiwa eneo la tukio.

Ilisemekana kwamba, Sabina aliporudi na viongozi hao walishtuka kuona moto mkubwa unawaka kwenye chumba chao ambapo Alex alichomoka na kukimbia huku moto huo ukishika kasi na kunasa kwenye paa la nyumba na kuunguza nyumba iliyokuwa na wapangaji wanne na stoo ya kuhifadhia vyakula.

Sabina naye, baada ya kuona nyumba hiyo ikiteketea, alimchukua mwanaye na kukimbia kusikojulikana huku mwenye nyumba akishika kichwa kwa mshangao.Akizungumza na gazeti hili, kaimu mwenyekiti wa mtaa huo, Habiba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la wivu wa mapenzi lililosababisha kuchomwa moto nyumba hiyo.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!


Loading...

Toa comment