The House of Favourite Newspapers

Beki Nkana: Ni kweli Nakuja Yanga

0

BEKI wa kati, Mkenya, Musa Mohammed amekiri kufanya mazungumzo na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo kutokana na kumalizika kwa mkataba wake na Nkana ya Zambia.

 

Musa ambaye ni nahodha wa zamani wa Gor Mahia, aliyewahi kukipiga katika Klabu ya KF Tirana ya nchini Albania kabla ya mwaka 2018 kujiunga na Nkana ya Zambia ambayo ilikuwa ikinolewa na Beston Chambeshi.

 

Akizungumza na Championi Jumatano, moja kwa moja kutoka Nairobi nchini Kenya, beki huyo alisema kuwa ni kweli amefanya mazungumzo ya kujiunga na Yanga na atakuwa tayari kujiunga nao ikiwa mipango itaenda sawa huku akitoa angalizo kwa washambuliaji wa Simba, John Bocco na Meddie Kagere kwa kuwa anawajua vizuri.

 

“Yanga kweli nimefanya nao mazungumzo kupitia wakala wangu ndiyo waliongea nao kila kitu na wakala alinieleza walipofikia ingawa mambo bado hayajakaa sawa kwa sababu ya hili janga la Corona.

 

“Naamini ninayo nafasi kubwa ya kujiunga na Yanga kwa sababu ni timu kubwa halafu naijiua vizuri lakini hata mkataba wangu na Nkana unamalizika Juni mwaka huu hivyo kwangu ni sawa, siwezi kuwaogopa Simba nawajua vizuri hasa washambuliaji wao Kagere na yule Bocco wasitarajie urahisi ikiwa nitafanikiwa kuwepo,” alisema Mohammed.

Stori: Ibrahim Mussa, Championi Jumatano

Leave A Reply