The House of Favourite Newspapers

Bella achangwanywa na ‘totoz’ wa Kibongo

0

christian bellaaWiki iliyopita Bella alisimulia namna ndoto yake ya kuwa juu zaidi katika kazi yake ya muziki ilivyomfanya kulazimika kuachana na Bendi ya Akudo Impact akiwa na malengo ya kuanzisha bendi yake mwenyewe.

Hiyo ilikuwa ni mwaka 2012 na kabla ya kuanzisha bendi hiyo, Bella alisema alilazimika kuchukua mapumziko na kwenda nchini Sweden kumjulia hali mke wake ambaye alikuwa mjauzito. Akiwa huko, Bella alimshuhudia mkewe huyo wakati wa kujifungua!

Je, nini sababu hasa iliyomfanya Bella kulazimika kumshuhudia mkewe akijifungua?

Songa naye mwenyewe…

KABLA ya kuelezea kilichosababisha kutakiwa kumshuhudia mkewe wakati akijifungua, Bella anasimulia kuhusu changamoto za wanawake wa Kibongo waliokuwa wakimtaka kimapenzi alizokuwa anakutananazo wakati akiwa kwenye Bendi ya Akudo Impact pamoja na tetesi za kumchukulia mchumba wake, mwimbaji maarufu wa Muziki wa Dansi nchini, Msafiri Diouf.

Bella anaanza kwa kusema suala hilo la kuwa ‘sukari’ kwa warembo lilikuwa ni changamoto kubwa sana kwake.

Anadai changamoto ilikuwa kubwa kwa sababu, kwanza asilimia kubwa ya wanawake hao aliokuwa anawakosha walikuwa wanamchanganya pia kutokana na uzuri wao pamoja na maumbo yao yaliyojazia ambayo ni tofauti na waliyonayo wale wa huko nyumbani kwao Kongo kwani wengi wao ni wembamba!

“Unajua jina langu mimi nilianza kulitengeneza nikiwa kwenye Bendi ya Akudo Impact, sasa tangu hapo wanawake wengi walikuwa wananishobokea hatari hasa waliokuwa wanakuja kuhudhuria kwenye matamasha yetu tuliyokuwa tunafanya zaidi ya mara moja kwa wiki.

“Ukweli ni kwamba kabla changamoto hiyo sijaweza kuimudu ilinitesa sana, nilijikuta nikipagawa nitoke na yupi na nimuache yupi kati ya hao walionitaka, si unajua wanawake tena wa Kibongo, wakali hatari, lakini taratibu nilikwenda ninayazoea mazingira ukafika wakati nikaliona suala hilo kuwa la kawaida nikaamua kutulia na huyo niliyekuwa naye kwa sababu pia siku zote hunionesha mapenzi ya dhati,” anasema Bella.

Bella anazidi kufunguka kuwa; kuhusu tetesi za kuwa mwanamke wake huyo aishiye Sweden aliyefanikiwa kupata naye mtoto kuwa alikuwa ni wa Msafiri Diouf hazina ukweli wowote na kuhusu suala hilo huwa hapendi kabisa kulizungumzia maana kama lina ukweli mtu wa kulizungumzia ni mkewe mwenyewe au Msafiri Diouf basi!

Ukiachana na hayo yote Bella anasema sababu hasa iliyomsababisha kulazimika kumshuhudia mkewe katika kila hatua wakati wa kujifungua ilikuwa ni baada ya mwanamke wake huyo kuhitaji hivyo.

“Aisee wanawake ni watu wa kuwaheshimu sana na ni ukweli kuwa hakuna kama mama. Shida wanayoipata wakati wanatuzalia watoto ni kubwa sana. Kile nilichokiona hakiwezi kufutika akilini mwangu, ooh…” Bella aliongea hayo na kujikuta akishindwa kuendelea, akainama na kuanza kufuta machozi.

Sekunde kadhaa zikakatika akiwa ameinama, nikaamua kumuacha ili kwanza atulie. Alipoinua uso alianza kuuimba kwa hisia kali tena kwa sauti ya chini wimbo wake wa Nani Kama Mama aliomshirikisha msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz;

Oyee nani kama mama, heshima kwa mama,

Yale mateso ulinibeba miezi mitisa tumboni mwako,

Pole sana mama,

Nikupe nini,

Heshima kwa mamaaa (mamaa),

Uliteseka siku ya kunitoa duniani,

Nikupe niniii (mamaa),

Thamani ya malezi yako siwezi kuilipaaaa…

Nani kama mamaaaa…

Bella alikomea hapo kuimba na kuinamisha tena kichwa chini, ikabidi nichukue jukumu la kumtuliza ili aendelee kusimulia.

“Pole sana Bella kwa kuumizwa na kumbukumbu hiyo,” ninamwambia.

“Asante kaka, hili suala limenikumbusha mbali sana, daima nitamheshimu sana mke wangu na wanawake wote duniani, ninamshukuru pia kwa kunizalia mtoto mzuri wa kiume aitwaye Hance,” anasema Bella na kuendelea kuwa;

Hayo yalipita na baadaye akaamua kwenda nchini Marekani alikokaa kwa muda wa takriban mwaka mmoja na ‘ushee’. Anasema akiwa huko alianza kufikishiwa maneno na washkaji zake waliokuwa Bongo kuwa alikitelekeza chumba alichokuwa akiishi bila kulipa kodi kisha kukimbilia mbele kwa ajili ya kusaka maisha!

Je, nini kitaendelea kwenye maisha ya Bella? Maneno hayo yana ukweli ndani yake? Bella atayajibu vipi? Kwa mengine mengi usikose wiki ijayo!

Leave A Reply