The House of Favourite Newspapers

BIBI HARUSI AFARIKI DUNIA GHAFLA!

DAR ES SALAAM: “Mamaaa….Mirabel umeondoka mamaaaa, umetuachaaa….ndoa yako imeyeyuka Mirabel, tangulia Mirabel, tangulia rafiki, uuuuwiiii…”

Hayo ni maneno ya simanzi yaliyokuwa yakitoka kinywani kwa mwanamke mmoja aliyekuwa amevaa nguo nyeupe na kitambaa cheusi kichwani akitajwa kuwa ni ndugu wa karibu wa mwanadada Mirabel Noel Yatera, mkazi wa Goba jijini Dar aliyefariki dunia ghafla ikiwa ni siku chache kabla ya harusi yake.

NI SIMANZI KUBWA

Mirabel ambaye ni maarufu jijini Dar kutokana na kazi ya kuuza maua ya asili kwa ajili ya sherehe mbalimbali akiwa na duka lake maeneo ya Msasani jijini Dar, alifariki dunia Julai 25, mwaka huu huku chanzo cha kifo chake kikiwa hakijulikani.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, ndugu wa Mirabel aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa familia alisema kuwa, kifo cha ndugu yao huyo kimewashtua sana kwani kabla ya mauti kumfika hakuwa akiumwa.

“Ni msiba mkubwa kwa familia kwa kweli, Mirabel ameondoka ikiwa ni siku chache kabla ya ndoa yake. Sikuwa na taarifa za kuumwa kwake, nilikuja kusikia tu kwamba alizidiwa akiwa kazini kwake huko, wengine wanasema alikuwa kwenye duka la rafiki yake aitwaye Doreen lililopo Kinondoni, akapelekwa hospitalini na walipofika akawa ameshaaga dunia.

ILIKUWA AFUNGE NDOA HIVI KARIBUNI

Ndugu huyo alidai kuwa, Mirabel ilikuwa afunge ndoa mwezi ujao na kwamba alikuwa kwenye maandalizi ya sherehe hiyo lakini kabla ya kutimiza ndoto yake hiyo, Mungu akamchukua.

“Ilikuwa aolewe mwezi ujao, taratibu zilikuwa zikiendelea lakini ndiyo hivyo yametokea hayo, kikubwa tumuombee tu, tulimpenda lakini Mungu amempenda zaidi,” alisema ndugu huyo.

KUMBE NI NDUGU WA NANDY

Awali wakati habari za kifo cha Mirabel zikianza ‘kutrendi’ mtandaoni, wengi walionesha kumpa pole mwanamuziki Faustina Charles ’Nandy’ bila kufahamika zaidi ana uhusiano gani na marehemu ambapo Risasi Jumamosi lilipomtafuta alieleza kuwa, ni dada yake.

“Jamani Mirabel ni dada yangu, mtoto wa mama yangu mkubwa, nimeumia sana kwa msiba huu jamani, daah,” alisema Nandy kwa sauti ya kwikwi ikionesha kuwa, amelia kwa muda mrefu.

Aidha, marehemu amejijengea jina kubwa jijini Dar kutokana na biashara yake ya kuuza maua ya shughuli mbalimbali ambapo inaelezwa kuwa, hata maua aliyopambiwa kichwani mwanamama Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ kwenye Video ya Wimbo wa Iyenaiyena ya Mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond’ yeye ndiye aliyewauzia.

“Mirabel mbona ni maarufu sana na kuna hata baadhi ya mastaa walikuwa wameipania harusi yake kwa kuwa amekuwa akiwauzia maua. Juzijuzi tu hapa alimpelekea maua Aunt (msanii wa filamu, Aunt Ezekiel) kwenye bethidei yake. Kwa kifupi msiba huu umewagusa wengi na ndiyo maana mitandaoni umeona amepostiwa sana,” alisema Imelda John, rafiki wa karibu wa Mirabel.

MAZISHI NI MOSHI

Shughuli za kuuaga mwili wa marehemu zilifanyika juzi Alhamisi kwenye Kanisa la KKKT, Goba jijini Dar kabla ya kuusarifisha kwenda Moshi kwa mazishi.

Gazeti hili linatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliofikwa na msiba huu na Mungu ailaze roho ya marehemu Mirab

 STORI: Neema Adrian, Risasi Jumamosi

Comments are closed.